Mbunge anapotangaza kujichimbia jimboni

13Jan 2021
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Mbunge anapotangaza kujichimbia jimboni
  • *Anaahidi hatawaacha ‘yatima’ wapigakura

HOFU ya wananchi na kilio cha kukimbiwa na wabunge waliowachagua kwa awamu kadhaa imemlazimisha Mbunge Jumanne Sagini, kupinga kambi jimboni Butiama kuwahudumia wapigakura wake.

Anaiambia Nipashe kuwa hatua hiyo inalenga kuwaondolea hofu wananchi, ambao walidhani huenda baada ya kumchagua angeingia mitini.

"Wakati wa kuomba kura niliahidi kuwa karibu tena kushirikiana nao kutatua kero zao na kuwaletea maendeleo na hilo nimeanza kulitimiza kwa kuwatembelea kila kata," anasema Sagini.

Katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, Sagini ni miongoni mwa wana CCM, waliopita bila kupingwa na kuwa mbunge wa Butiama, akitanguliwa na Nimrod Mkono, aliyeongoza jimbo hilo kwa miaka 20 ambalo awali lilikuwa Musoma Vijijini, lakini 2015 liligawanywa na kupatikana jingine la Butiama.

Anasema baada ya kiapo amepiga kambi jimboni mwake, ili kusikiliza kero za wananchi na kushirikiana nao kuzitatua ikiwa ni moja ya ahadi zake alizoahidi wakati wa kampeni na anatarajia kuzuru kata zote zikiwamo Bisumwa, Buhemba, Bukabwa, Buruma na Busegwe.

"Nimefanya ziara katika jimbo langu ili pia kuhamasisha jamii katika shughuli za maendeleo, kwani ushirikishwaji ni muhimu, mbunge kukaa mbali na wananchi wangu kwa muda mrefu si jambo jema," anasema.

KERO ALIZOTATUA

Anasema: “Butiama kama yalivyo majimbo mengine, inakabiliwa na matatizo mbalimbali ambayo yanahitaji utatuzi mfano kilimo cha mihogo kinakabiliwa na ugonjwa unaosababisha wakulima wasipate tija," anasema mbunge huyo.

Anasema, hali hiyo imemfanya anunue magunia 80 ya mbegu ya mihogo aina ya mkombozi yenye thamani ya zaidi ya Sh. 2,000,000 na kuwagawia wakulima na kwamba Butiama inategemea mihogo, viazi vitamu na viazi lishe, mahindi, mpunga na mtama, lakini matatizo yanabakia kwenye mihogo.

"Wataalamu wa kilimo wanasema, mbegu ya mkombozi inahimili magonjwa na inaweza kutoa magunia kati ya 16 hadi 20 katika ekari moja, tofauti na nyingine zinazotoa magunia matano hadi sita kwa ekari," anasema mbunge huyo.

Aidha, anafafanua kuwa michezo kwa sasa ni ajira, na kwamba ameshagawa mipira 40 kwa timu mbalimbali katika kata 18 za jimbo hilo ikiwa ni maandalizi ya mashindano ya mpira wa miguu ili kuinua vipaji vya soka.

"Nitaendelea kuibua michezo mbalimbali jimboni, kwa kuwa michezo kwa sasa ni ajira, na nitatafuta baiskeli 20 kwa rafiki zangu ili kuanzisha mashindano ambayo ni sehemu ya ajira," anasema.

Anataja ujenzi wa shule ambao ameshirikiana na wananchi akitoa mifuko 255 za saruji kwenye kata za Kamugegi na Nyamimange ili kuboresha miundombinu ya shule kata hizo.

VIPI MAJI JIMBONI?

Anasema, Wizara ya Maji imesaini mkataba wa kujenga mradi mkubwa wa maji kutoka Mugango Musoma Vijijini hadi Kiabakari jimboni humo unaotarajia kukamilika baada ya miezi 24 na kuanza kuhudumia wananchi 200,000 kwenye vijiji 19 vilivyopo wilaya za Musoma na Butiama.

"Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Antony Sanga, ameshasema kuwa mradi huo ukikamilika utatoa huduma ya maji kwa wananchi kwa miaka 20 kwa utoshelevu, na utazalisha lita zaidi ya milioni 17 kwa siku katika awamu ya kwanza," anasema mbunge huyo.

Anamkariri Katibu Mkuu kuwa mahitaji ni lita milioni 12 kwa siku, na kwamba kwa awamu ya pili uzalishaji utakuwa lita zaidi ya milioni 35, huku baadhi ya vijiji vikiongezwa kwenye mradi huo.

"Baadhi ya vijiji vya jimbo langu vitanufaika na mradi huo, wakazi wa Butiama wataondokana na adha ya maji inayowakabili kwa sasa baada ya mradi huo kukamilika," anasema.

Anafafanua kuwa ilikuwa ni aibu kuona maji yanakwenda mbali zaidi ya kilometa 400 mikoa ya mbali, huku wananchi wa Butiama na Musoma wanakosa huduna hiyo wakati wanazungukwa na Ziwa Victoria.

"Nimshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa uamuzi wake wa kuleta mradi huu haraka iwezekanavyo baada ya kuapishwa, hakika amejibu ombi na kilio cha wananchi, niombe pia kata zinazopakana na mto Mara ikiwamo kata ya Buswahili na Bukabwa ikiwezekana ziangaliwe nazo ziwekwe kwenye mradi awamu nyingine, wananchi wapelekewe huduma ya maji," anasema.

HISTORIA YA BUTIAMA

Sagini anatamani kuiona Butiama mpya akieleza kuwa ni sehemu muhimu kwa taifa kwani ndiko kilipo Kijiji cha Mwitongo alipozaliwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1922 na ni wilaya ilioanzishwa rasmi Machi 2012 ikiwa ni sehemu ya kuvutia utalii hasa wanaozuru Makumbusho ya Mwalimu Nyerere pamoja na kujifunza historia yake.

Anakusudia kushirikiana na wapigakura wake ili kuifanya iwe ya kisasa na yenye maendeleo makubwa. Sensa ya mwaka wa 2012, inataja idadi ya wakazi kuwa ni 241,732 wanaojishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara.

Habari Kubwa