Mbunge auawa Uingereza huku kampeni kura ya maoni EU zikiahirishwa

18Jun 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mbunge auawa Uingereza huku kampeni kura ya maoni EU zikiahirishwa

MAUAJI ya Mbunge Jo Cox (41), maarufu kama ‘Britain first’ wa chama cha Labour cha Uingereza, yamesababisha kuahirishwa kwa muda kampeni za kura ya maoni iliyokuwa iamue hatima ya Uingereza kubakia au kutoka kwenye ushirikiano wa mataifa ya Umoja wa Ulaya (UE).

Mwanamama Cox alipigwa risasi juzi na kusababisha sintofahamu , huzuni na mshangao kila kona miongoni mwa wafuasi wake na Uingereza kwa ujumla, hivyo kusababisha kuahirishwa kwa kura hiyo ya maoni, inayotarajiwa kupigwa Alhamisi ijayo.
Mbunge huyo kijana aliyekuwa anakampeni kwa nguvu nguvu zote Uingereza ijiondoe EU alipigwa risasi wakati akijiandaa kukutana na wapiga kura wake wa Birstall karibu na jiji la Leeds Kaskazini mwa Uingereza.

Mbunge huyu alichomwa kisu na kupigwa risasi pia , kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa jiji la West orkshire,mtuhumiwa mwanaume mwenye miaka 52, anashikiliwa na polisi, pamoja na silaha iliyopatikana.

“Hadi sasa hatupo kwenye nafasi ya kuzungumzia kiini cha mauaji haya kwa wakati huu,” alisema Kaimu Mkuu wa Polisi Dee Collins.
Shuhuda mmoja alisema alimuona mtu mmoja akichomoa silaha kutoka kwenye mfuko aliokuwa ameubeba na kufyatua risasi.“Nilimuona mwanamama amedondoka chini na mikono yake ikiwa kwenye magoti huku damu ikiwa imetapakaa usoni mwake,” alisema shuhuda huyo, Hichem Ben-Abdallah, alipozungumza na wanahabari.” Alisema na kuongeza kuwa japo hakupiga kelele lakini ilikuwa bayana alipata maumivu makali.

Mume wa Cox Brendan kwa huzuni alisema: “Alikuwa akitamani mambo mawili yafanyike nayo ni watoto wetu wanakuzwa katika upendo mkubwa na jingine ni sisi sote tuungane kupinga ukatili na chuki kama hizo ambazo ndizo zimesababisha kifo chake.”

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, amesema mauaji ya mbunge huyo mwenye watoto wawili ambaye aliwahi kushiriki kwenye kampeni za Rais wa Marekani Barack Obama, mwaka 2008 ni huzuni.

“Tumempoteza nyota wetu, alikuwa mpiga kampeni muhimu, alikuwa na moyo mkuu. Ni habari zenye mstuko mkubwa” alisema Cameron, ambaye ni mwanachama wa Chama cha Conservative, kinachoongoza serikali.

Wadadisi wa mambo wanasema huenda mauji yake yanaweza kuhamasisha wapiga kura kusema ‘ndiyo’ Uingereza iendelee kubakia ndani ya EU.

Haikufahamika mara moja athari za mauaji hayo kwenye ‘referandamu’ ambayo imepangwa kufanyika Alhamisi ijayo Juni 23 zitakuwa vipi, kwani hadi kufikia sasa umeigawanya Uingereza kwenye wapinga EU wanaotaka Uingereza ijitoe kwenye umoja huo na kambi nyingine inayotaka ibaki.

Wachunguzi wa mambo wanahisi kuwa huenda mauaji hayo yataongeza ari ya ‘kubakia ndani ya EU’ kampeni zake hivi karibuni ambazo katika siku za hivi karibuni imezidiwa nguvu na zile zinazohimiza kujiondoa au ‘leave EU” kwa mujibu wa kura za maoni.

Kifo cha Cox pia kinaelezewa kuwa kimechangia kuinua thamani ya Pauni dhidi ya Dola. Waziri wa Fedha George Osborne, pamoja na Gavana wa Benki Kuu ya Uingereza, Mark Carney, waliondoa baadhi ya taarifa za mipango iliyokuwa inaandaliwa na serikali kabla.

MAUAJI
Taarifa za vyombo vya habari zilinukuu maelezo ya mashuhuda yakielezea mauaji hayo ya kumpiga risasi mwanasiasa huyo aliyepewa jina la “Britain first”, kwa kuonyesha msimamo wa kizalendo na mtetezi wa wanyonge mitaani.

Huko West Yorkshire , polisi ilisema taarifa walizo nazo ni kwamba tukio hilo linachukuliwa kama la ndani ya sehemu hiyo lakini athari zake ni kubwa na matokeo yake yatakwenda mbali zaidi.

Wakati hayo yakitokea umiliki binafsi wa silaha nchini Uingereza ni utaratibu unaodhibitiwa mno lakini pia, hata matukio ya kuwapiga risasi na kuwaua watu mashuhuri wakiwamo wanasiasa yanatokea japo si mara kwa mara.

Mbunge wa Uingereza ambaye alitangulia kuuliwa kabla ya Fox alikuwa Ian Gow, aliyefariki kutokana na bomu lililokuwa limewekwa chini ya gari lake na waasi wa Irish Republican Army (IRA), mwaka 1990 akiwa nyumbani kwake huko kusini ya Uingereza.

Kuanzia juzi bendari ya Uingereza maarufu kama ‘Union Jack’ ilikuwa inapepea nusu mlingoti kwenye ofisi za Bunge jijini London, wakati huko Birstall maelfu ya waombolezaji walishiriki kwenye ibada ya mkesha.

Washirika na marafiki zake walieleza huzuni na simanzi kufuatia msiba huo , katika Chuo Kikuu cha Cambridge, alikofanya kazi kwa miaka miaka 10 kwenye shirika la kijamii la Oxfam , akisimamia masuala ya utetezi wa masuala ya ubinadamu mambo ya wanawake, huzuni na vilio vimetawala.

Cox alishinda ubunge kwenye uchaguzi wa mwaka jana akiwawakilisha wapiga kura wa jimbo la Kaskazini ya Uingereza la Batley na Spen.

“Tumempoteza mwanamke shujaa na maarufu na mbunge hodari lakini demokrasia yetu itaendelezwa “ anasema Kiongozi wa Chama cha Labour , Jeremy Corbyn , katika taarifa iliyorushwa na televisheni.

“Na sasa tukiomboleza kazi alizofanya tutaendeleza mambo mema aliyofanya ili tupate dunia yenye haki ambayo wakati wa maisha yake alijitahidi kuifikia.”

Taarifa za polisi ziliongeza kuwa pamoja na kifo hicho kuna mwanaume mwenye miaka 77aliyeshambuliwa na kupata majeraha japo si ya kutishia maisha.

Televisheni ya BBC TV jana ilirusha taarifa na picha zinazoonyesha mtuhumiwa mwanaume mwenye upara, akikamatwa na polisi.Kaimu Mkuu wa Polisi Collins, alinukuliwa akisema “uchunguzi mkali pamoja na kukusanya ushahidi mwingi ni kazi inayoendelea kwa sasa.

MASHAMBULIZI KWA WABUNGE
Shambulio la karibuni la mbunge lilikuwa mwaka 2010, wakati mbunge kupitia chama cha Labour na waziri mstaafu Stephen Timms, alipochomwa kisu tumboni akiwa ofisini kwake na East London na mwanafunzi mwenye miaka 21, aliyekuwa amekerwa na uungaji mkono wake wa vita ya Iraq mwaka 2003.

Kadhalika mwaka 2000, mwanasiasa wa kiliberali aliyekuwa diwani aliuawa kwa kupigwa upanga uitwao ‘samurai’akiwa ofisini kwake huko magharibi ya UIngereza, kwenye ofisi ya mbunge Nigel Jones, ambaye pia aliumiza sana kwenye shambulio hilo.

Habari Kubwa