Mbunge Maige adokeza wapi Veta inasimamia pengo ajira

29Nov 2019
Shaban Njia
Kahama
Nipashe
Mbunge Maige adokeza wapi Veta inasimamia pengo ajira
  • Nafasi ya mabinti; Veta Mwakata nao…

VYUO vya Maendeleo ya Ufundi Stadi maarufu ‘Veta’ vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini, vimekuwa vikichangia kwa asilimia kubwa kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana na hasa mabinti, waliomaliza elimu ya msingi na sekondari na hawajapata mwelekeo wa kimaisha, ikiwamo ajira.

Wanafunzi Chuo cha Ufundi Mwakata, wakionyesha ujuzi wao, namna mfumo wa umeme unavyofanya kazi. PICHA: SHABAN NJIA.

Veta inatoa mafunzo ya stadi na fani mbalimbali, wengi ni wale waliomaliza elimu msingi na kidato cha nne na hawakufanikwa kuendelea na ngazi za juu. Ni mtazamo unaoenda mbali, hata kwa wale walioko mitaani kwa sababu moja na nyingine ‘wanaelea.’

Aidha, Veta imekuwa ikitengeneza wataalamu mbalimbali na kuna wakati inawatoa walio bora zaidi kuliko hata waliofika vyuo vya juu zaidi katika stadi hizo.

Kwa mabinti, wamekuwa wakipewa ujuzi katika stadi kama utumiaji vyerehani, mitindo, udereva, upishi na umeme, vyote vikiwasaidia kupunguza wimbi la wasichana kutojihusisha na uuzaji miili yao, kama namna ya kujikimu kimaisha.

MBUNGE MSALALA

Ezekiel Maige, ni Mbunge wa Jimbo la Msalala, anasema kuwa, vyuo vya ufundi vimekuwa vikichangia kwa kiwango kikubwa kupunguza wimbi la vijana mitaani wasiokuwa na ajira kwa kujiajiri kutokana na fani waliyoipata kwenye vyuo hivyo.

Pia, anasema vimepunguza wimbi la vijana kutojihusisha na uhalifu, vijana wengi wanaomaliza elimu, mbali na wachache wanaoingia katika uhalifu, bado vijana wanajihusisha ama kwenye ufugaji au kilimo kisicho na tija.

Anasema, wamekuwa wakitumia nguvu kubwa katika kuandaa mashamba, lakini wanaishia katika mavuno kidogo na wapo wanaokata tamaa, ilhali endapo wangepata elimu ya kilimo wangepata hatua kubwa ya mafanikio, hata kuwa wakulima wakubwa.

“Vyuo vyetu vya ufundi kwa kiwango kikubwa vimepunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana wetu. Wanahitimu elimu ya msingi na sekondari na kukosa alama za kuendelea na masomo na wanaanza kuranda mitaani, kusubiri kulelewa na wazazi wakijiingiza kwenye vitendo vibaya,” anasema Maige.

UFUGAJI SAMAKI

Maige anawataka wasimamizi wa vyuo vya ufundi kuanzisha mafunzo ya ufugaji wa samaki, nguruwe, ng’ombe wa maziwa na kilimo, ili wanavyuo hao waweze kujikita katika mazingira ya kilimo chenye tija na ufugaji wa kisasa.

Anasema, kuna vijana wanaosomea fani za umeme au udereva wa magari na wamekuwa wakikosa nafasi za kuonyesha ujuzi wao ndani ya jamii, shida kuu ni kukosa sifa za kupata ajira, kulingana na alama alizozipata kwenye mitihani yake ya mwisho.

“Kila mtu anaenunua gari, anafahamu kuendesha vizuri tofauti na kipindi cha nyuma, walikuwa wakitafuta madereva wa kuwaendesha. Hii ni kuogopa kuingia kwenye gharama, ni vyema tukaanzisha fani za ufugaji samaki, nguruwe, ng’ombe wa maziwa na kilimo cha kisasa ili wajikite huko,” anasema Maige.

MIKOPO/UJASIRIMALI

Anasema, wasimamizi wa vyuo vya ufundi wanatakiwa kuanzisha vikundi vya ujasiriamali kwa wanavyuo na kuwapatia mikopo itayowapa mitaji, pindi vijana wanapohitimu masomo, lengo ni kujiajiri.

Maige anasema, sehemu kubwa ya wanavyuo wameshindwa kujiajiri, kutokana na ukosefu wa mitaji na badala yake wanahamisha maisha ‘vijiweni’ na kuranda mitaani, wakianza kuwa wanachama wa vikundi visivyofaa.

“Tuna vijana wengi mitaani wamemaliza vyuo vya ufundi, lakini wameshindwa kujiajiri kwa kukosa mitaji. Ili waweze kujiajiri kulingana na fani zao, tunatakiwa kuanzisha vikundi vya ujasirimali, ambavyo vitakopeshwa na halmashauri na chuo kitakuwa mdhamini wao,” anasema Maige.

”Halmashauri zimekuwa zikitoa mikopo yenye riba nafuu kwa vikundi vya wajasirimali na kinamama, vijana na watu wenye ulemavu na wengi wanaopewa mikopo hiyo, hawana elimu ya kile wanachoendea kukifanya, kama ambavyo wangepatiwa wanavyuo vya ufundi,” anaongeza.

MKUU UFUNDI MWAKATA

Padre Jose Eriyanicka, ni mwanzilishi wa Chuo cha Ufundi Mwakata (S.F.S VTC) kilichopo katika Kata ya Mwakata, ndani ya Halmashauri ya Msalala, anasema mbali na kutoa ujuzi wa fani za kifundi, pia wanatoa ajira kwa vijana wanaofanya vizuri masomoni, wanaokuwa walimu.

Anasema katika kukabili changamoto ya ajira zao, wanatarajia kuanzisha fani za ufugaji na kilimo, sambamba na vikundi vya ujasirimali vinavyoendana na fani zao, waweze kujiajiri wanapohitimu.

Padre Jose anasema hadi sasa wamekwama kuanzisha fani za ufugaji samaki na ng’ombe wa maziwa, nguruwe na kilimo kwa sababu hawana vyanzo bora na maji ya uhakika, kwani maji wanayoyatumia, wanayatoa umbali wa kilomita 10, yakisombwa na magari.

Anafafanua kwamba, mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria, umepita nyuma ya chuo hicho ukielekea Kata ya Isaka na endapo watauganishiwa maji hayo, itakuwa rahisi kuanzisha fani hizo tajwa, wanavyuo kujifunza kwa vitendo na nadharia.

Mratibu Mafunzo wa chuo hicho, Charles Maganga, anasema, zaidi ya wanavyuo 177 wamehitimu fani mbalimbali na wengine tisa walisitisha masomo kutokana na ukosefu wa ada, utovu wa nidhamu.

Habari Kubwa