Mbunifu tanuru rafiki la ‘taka za hedhi’

23Feb 2021
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Mbunifu tanuru rafiki la ‘taka za hedhi’

WASICHANA na wanawake bila kujali wanapoishi iwe mjini au vijijini wanahitaji pedi, maji, faragha  ya kujisitiri wakati wa hedhi pamoja na sehemu ya  kuhifadhi taulo walizotumia ili zisichafue mazingira pamoja na kuwadhalilisha.

Katika maeneo tofauti ikiwamo vyuo, taasisi na baadhi ya shule za msingi au sekondari hakuna vyombo vya  kuhifadhia pedi zilizotumika na utaratibu bora wa kuziteketeza pia ni changamoto.

Aidha, hedhi salama inatatizwa na ukosefu wa maji shuleni, vyuoni na katika vituo vya afya na zahanati na hiyo ni changamoto inayosababisha wanafunzi wasichana kukosa masomo kati ya siku 40 hadi 50 kwa mwaka (vyuoni na shuleni).

August Mbuya, mhandisi wa rasilimali maji na  umwagiliaji  kutoka Chuo cha Maji,  jijini Dar es Salaam, anasema amezitazama changamoto za wanawake na sasa ana jibu la kuwasaidia kwenye eneo la kuhifadhi taulo zinazotumiwa wakati wa hedhi na kuzitekeza.

Anasema katika masomo yake ameangalia namna bora ya kulinda utu wa mwanamke, akisema:“Mimi ni mwanaume lakini  nikaamua kuja na suluhisho la masuala ya wanawake, wakati nikiwa mwaka wanne chuoni nilibuni banda salama kulinda utu wao.”

“Nimesoma Sekondari ya Old Moshi ambayo ni ya wavulana. Tulikuwa na utaratibu wa kutembeleana  shule kwa shule hasa kidato cha tano na sita. Nilipotembelea shule za wasichana muda mwingi nilifanya tathmini nikipendelea kufuatilia masuala yao kujua namna watakavyosaidiwa ili kuongeza ubora kwenye masomo yao.”

Mbuya (25) akizungumza na NIPASHE hivi karibuni, Dar es Salaam, anaeleza kuwa kwa msingi huo alibuni mambo ya kuwasaidia wanawake kwa kutumia ubunifu na utafiti.

“Changamoto zao kubwa nilipozungumza na wasichana ilikuwa ni vyoo na namna bora ya kuhifadhi na kuharibu taka au taulo za hedhi. Nikawa natamani kupata ufumbuzi ni namna gani naweza kubuni mazingira ya kuwasaidia.”

“Nikabaini kuwa katika siku zao za hedhi ambazo ni kati ya tatu na tano wengine wanakumbana na changamoto zikiwamo za  mazingira.

Mwingine anakuwa katika siku zake kipindi cha mtihani wa taifa, mitihani ya kawaida, au vipindi vya darasani, hayo matukio yote yakanifanya niwe mdadisi,” anasema Mbuya.

VYOO KUZIBA

Anakumbusha kuwa kuna wakati walizungumzia kuhusu vyoo kuziba kila wakati na katika mazungumzo hayo walimwelezea kuwa vinaziba mara kwa mara na kuona kuwa ilikuwa kero kubwa kwao.

Anasema alipofanya maombi ya chuo kikuu alivutiwa na kusoma masuala ya maji na lakini wazo la kubuni mbinu  ya kuboresha mazingira ya vyoo kuziba kutokana na kukosa sehemu ya kuhifadhi pedi na badala yake kuzirusha vyooni likapotea katika fikra.

“Ila mwaka wa tatu lilinijia tena na  nilipotembelea shule ya Kibasila ya Dar es Salaam, hospitalini na  taasisi zenye mikusanyiko baadhi changamoto nilizikuta ni hizo hizo,” anasema Mbuya.

Kutatua kero hiyo  Mbuya anasema alibuni ‘incinerator’ au tanuru linalojengwa kwa matofali ambayo hutumika kuchomea taka akilenga taulo za hedhi,” anasema Mbuya.

“Asilimia 40  hadi 60 ya vitu au taka zinazofanya mfumo wa maji taka kuziba, inatokana utupwaji wa pedi katika vyoo ,” anasema.

KUTUMIA BANDA SALAMA

Mbuya anasema amefanya utafiti miundombinu ya majitaka iliyopo Dar es Salaam amebaini hilo na kwamba , utupaji wa pedi chooni si jambo jema wala kuzifukia ardhini kote kunachafua mazingira,” anaeleza Mbuya.

“Iwapo mwanamke akitumia pedi za kila mwezi hadi kumaliza nimebaini zina uzito takriban gramu 300 na hata  nusu kilo.”

Anaongeza:”Kwa mfano chuo kina wanafunzi wa kike 1,000 ukizidisha kwa gramu 300 kila  mwezi wanazalisha kilo 300,000 za pedi sawa na tani 300. Na Tanzania bado hatuna mfumo wa kurejeleza (recycling) pedi, hizi kilo ni nyingi, ndiyo sababu ya kubuni banda salama.”

UFUMBUZI

Injinia Mbuya anasema kuliko na kundi kubwa la wanafunzi kama mabwenini  kuna kilo nyingi za pedi zinazotumika na utupaji wake unaweza usitunze utu wa mwanamke iwapo zitazagaa ovyo jalalani bila kuteketezwa.

Anasema hata kutupwa kwa kuchanganya na taka nyingine katika vyombo vya kuhifadhia taka si sahihi kwa kuwa haziozi.
Pia anaeleza ilivyo tatizo kwa wahudumu wa usafi kwenye maeneo ya shule hizo au taasisi, kwa kuwa taulo nyingine zinaanza kuoza na iwapo gari la kubebea taka halijafika kuzizoa  kwa wakati sehemu zinapohifadhiwa kunanuka.

“Kwanza wahudumu hawapo katika maeneo ya shule za umma iwe sekondari au msingi, labda shule binafsi, lakini nao wanakumbwa na changamoto kwani vyombo vya kuhifadhia pedi vikijaa hawana pa kuzipeleka hadi gari la taka litakapofika baada ya siku tatu au wiki.”

Anasema linahitajika eneo ili kutupa taka za hedhi mara tu chombo kinapojaa na kupunguza harufu chooni.

Utamaduni wa kila mwanamke alivyofundishwa, ni kuhifadhi ipasavyo mahali sahihi taka hizo baada ya kuzitumia, aidha kwa kuchoma ili mwingine asione.

Anaeleza kuwa ndiyo maana wanapokuta chombo kimejaa wanazitumbukiza chooni mwishowe kinaziba, lakini wapo wanaozifukia hasa kwenye eneo binafsi, kwa wanafunzi si rahisi, hata kuchoma wanahitajika kuni.

Katika utafiti alioufanya tangu akiwa shule hadi chuo, alipohitimu aliamua kuja na suluhisho la kuwa na eneo la kuteketeza pedi, aliloliita banda salama.

Anasema  wazo hilo alilipata akiwa kwenye  mafunzo ya vitendo ambayo mwanachuo analazimika kuyafanya.

“Mwanzo nilikuja na majina tofauti, niliamua kusema banda salama ili kulinda utu wa mwanamke, kwa hiyo nikaamua kuwa na jina rahisi ili kukubalika katika eneo lolote.”

BANDA RAFIKI

Mbuya anasema banda hilo ni rafiki wa mazingira kwa kuwa chanzo cha nishati ya kuteketeza pedi hizo ni gesi ya kinyesi inayotoka kwenye vyoo vya shule au taasisi iwe hospitali au  chuo.

Mbunifu huyo anasema iwapo hakutakuwa na usimamizi makini banda hilo linaweza kuwa na madhara kwa muda mrefu lakini atatoa mwongozo kulisimamia.

“Banda hilo litazalisha mbolea maana baada ya taka hizo kuchomwa majivu yanaweza kutumiwa kupanda mazao kama mboga bustanini.” Anasema.

MATARAJIO

Mbuya ambaye mwishoni mwa mwaka jana jijini Dodoma alipokea tuzo ya ubunifu wa wazo hilo aliloliwasilisha mbele ya wadau wa maji ikiwamo wizara, baada ya mchakato wa kupatikana washindi wa ubunifu, alipata tuzo ya ubunifu.

Anasema tuzo hiyo alipewa na Association of Tanzania Water Suppliers (ATAWAS) ambao huandaa mkutano wa wadau wa maji kitaifa.

Pamoja na kuwapo kwa changamoto ya ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu, Mbuya anasema baaada ya kuhitimu masomo yake kwa miaka minne chuo cha maji, anafikia kuanzisha taasisi yake na kuajiri.

“Nikiwa chuo nilipata ushirikiano mdogo kutoka kwa wenzangu kuhusu wazo hili, walinicheka na kuniita ‘jamaa wa pedi’ sikuchukuliwa kama changamoto.

Watu wamezoea kuwa na ‘mawazo ambayo ni ya kawaida. Tukiwa vyuoni, nikaamua kuja na suluhisho kwa wasichana katika kukabiliana na changamoto za hedhi na kulinda utu wao, hata kulinda mazingira,” anasema Mbuya.

Anaeleza kuwa kampeni za kugawa pedi bure kwa wanafunzi, anaziunga mkono ingawa kunahitajika vitu vingine kwenda sambamba ikiwamo namna ya kuzitupa.

Mbuya anashauri Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTEC), kuweka wataalamu wake vyuoni ili kushirikiana na wabunifu kuboresha na kusaidia utekelezaji wa mawazo wa wanachuo vyuoni.

“COSTEC ikiwa vyuoni ni rahisi kuliendeleza wazo, badala ya kusubiri nihitimu hadi kuja kuwasilisha wazo nikipata shughuli za kiuchumi siwezi kulifanyia kazi nitakosa muda,” anasema Mbuya.

Habari Kubwa