Mchango kusajili jina la biashara katika kujenga soko la ushindani

23May 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mchango kusajili jina la biashara katika kujenga soko la ushindani

KATIKA biashara, ushindani ni vigumu sana kuuepuka, hii ni kwa sababu katika biashara yeyote mtu atakayoanzisha ni lazima kuna watangulizi au kuna wengine ambao watakuja baada ya kupendezwa nayo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Godfrey Nyaise

Kwa mjasiriamali au mfanyabiashara yeyote ni vyema kufahamu bayana kwamba ili biashara ikue ni lazima wigo wake katika soko uongezeke kwa kadri muda unavyokwenda.

Wigo wa soko hupimwa kwa kuangalia biashara inayotoa huduma au kuuza bidhaa zake kwa kiwango kikubwa kushinda zingine za namna moja.

Mfano kama soko la uuzaji maji ni asilimia mia moja na Wafanyabiashara katika soko hilo wapo watatu yani A, B na C.

Mfanyabiashara A. ameshika soko kwa asilimia arobaini huku wafanyabiashara B na C wakishika kwa asilimia thelathini kila moja, basi kwa hatma hii mfanyabiashara A ndiye anafanya vizuri zaidi.

Makala hii itaangazia mikakati kadhaa ambayo mfanyabiashara anaweza kuitumia ili kuweza kujiongezea nafasi katika soko la bidhaa anayouza au huduma anayotoa.

Ubunifu

Mmoja kati ya wataalam wa masuala ya masoko duniani, Leslie Kramer, anaeleza kwamba ili mfanyabiashara apate nafasi katika soko ni lazima awe mbunifu katika njia za kufikisha bidhaa au huduma yake kwa wateja wapya.

Ubunifu huu pia ni kutumia mbinu katika biashara yake ambazo hazijawahi kutumiwa na wapinzani katika soko hilo.
Kuimarisha uhusiano na wateja

Siri moja ya biashara ni kuhakikisha idadi ya wateja haipungui, mfanyabiashara mzuri hujenga uhusiano mzuri na wateja wake ili wasije kuhamia kwa mfanyabiashara mwingine.

Wahenga walisema mteja ni mfalme, anapenda siku zote kusikilizwa na kupewa huduma ya kumridhisha.

Hivyo mfanyabiashara unatakiwa kujenga uhusiano mzuri na wateja kwa kuwasikiliza na kufanyia kazi maoni yao, jitihada hizi zinatakiwa ziende sambamba na kuvutia wateja wapya.

Kwa kufanya hivi tarajia matokeo mawili, moja ni kuwalinda wateja wa biashara yako na mbili utavutia wateja wapya kila siku hivyo biashara itaendelea kukua siku hadi siku.

Tengeneza mkakati wa kuongeza wigo wa soko

Mkakati huu unasimamia vitu viwili vikuu, moja ni malengo na mbili ni muda wa kuyafikia hayo malengo. Unaweza kuwa wa mwaka mmoja na ukagawa utekelezaji wake kwa awamu nne, kila awamu ikiwa na miezi mitatu.

Mkakati huu utasaidia kupima na kufahamu kama malengo uliyoweka kutekeleza ndani ya kila awamu umefanikiwa au hapana na kujua sababu hasa ni zipi.

Kuipatia jina biashara yako

Jina la biashara ni utambulisho wa biashara fulani, Jina hili huipatia biashara uwezo wa kutambulika na kukumbukwa na wateja katika namna mbalimbali.

Wateja wanaweza kuitambua biashara yako kwa kutajiwa jina pekee hata kama hawajawahi kufika lakini pia wanaweza kuitambua biashara kwa kuelekezwa na watu wengine na wakafika sehemu ilipo biashara hiyo.

Jina la biashara pia ni muhimu kwa ajili ya kuitangaza biashara yako kupitia njia mbalimbali na watu wakaifikia kwa urahisi.

Ni muhimu pia kuzingatia kwamba sifa kuu ya Jina la biashara ni upekee, haitakiwi kufanana jina la mtu mwingine, kwa sababu hii itawachanganya wateja wanaotaka huduma.

Mara baada ya kupata Jina la biashara, namna nzuri ya kulinda upekee ni kufanya usajili katika Mamlaka husika ili kupewa haki ya kutumia jina hilo katika biashara peke yako.

Kwa Tanzania mamlaka inayohusika na usajili wa jina la biashara ni Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ambayo inatoa huduma hii kwa njia ya mtandao.

Meneja Uhusiano wa (BRELA) Robetha Makinda, anasema kigezo pekee kwa ajili ya kusajili jina la biashara ni kuwa na namba ya utambulisho wa Taifa kutoka NIDA.

Anasema anayehitaji kusajili jina la biashara atatakiwa kufungua akaunti katika nfumo wa usajili kwa njia ya Mtandao ya (ORS), hivyo atatembelea tovuti ya www.brela.go.tz .

Aidha, anasema baada ya kufungua akaunti atatakiwa kuandaa ombi lenye taarifa zake za biashara na kutuma BRELA ambapo atalipia kiasi cha Sh. 20,000/- pekee.

Kisha atapata cheti ambacho kinampatia haki ya umiliki wa jina hilo la biashara.

“Wahenga walisema “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo” kwa muktadha huu biashara ni kama mtoto, njia ambazo zinatumika kuilea biashara ndizo zitakazo ifanya ikue, idumae au ifilisike.” anasema.

Habari Kubwa