Mchengerwa: Wanaodharau kamati yangu wamekosa hoja

10Feb 2016
Beatrice Shayo
DAR
Nipashe
Mchengerwa: Wanaodharau kamati yangu wamekosa hoja

“WANAOIDHARAU kamati yangu na kudhani haina wabunge wazoefu kuhusu masuala ya sheria wamekosa hoja ya msingi, mimi nimefanya kazi katika Idara ya Mahakama kwa zaidi ya miaka 14 na hii kamati itakuwa ni ya kipekee ambayo itafanya vizuri kwa kuwa ninazifahamu sheria,”

Hayo ni maneno ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa Mchengerwa ambaye ni Mbunge wa jimbo la Rufiji (CCM), anasema amejipanga vizuri katika kamati hiyo na kwamba jina lake halijakosewa kupangwa katika kamati hiyo kwa kuwa anaijua vizuri sheria na amewahi kuifanyia kazi.

Kabla ya kujikita katika masuala ya siasa anasema mwaka 2009 hadi 2015 alikuwa ni katibu wa Jaji Kiongozi wa Tanzania katika kipindi cha miaka sita. Anasema kabla ya hapo alishawahi kufanya kazi katika mahakama mbalimbali ikiwemo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam katika kipindi hicho cha miaka 14.

“Hii nafasi niliyopewa ipo nyumbani siyo kweli sina uwezo unajua huwezi kujiita mwanasheria bila kuifanyia kazi sheria,” anasema “Haiwezekani mtu mmoja uachwe kwenye kamati hiyo hiyo ambayo umewekwa lazima kuwepo na mabadiliko ili na wabunge wapya waweze kujifunza kila mbunge ana haki ya kuwekwa kwenye kamati ambayo atakuwa amepangiwa,” anasema Anasema Mbunge akiingia bungeni kwa mara ya kwanza siyo kigezo cha kutokujua sheria ama kushindwa kuiongoza kamati husika.

“Wapo wabunge ambao wanajiita ni wanasheria wakati hawajawahi kuifanyia kazi sheria, huwezi kujiita mwanasheria bila kuifanyia kazi sheria,” anasema Mchengerwa Akielezea uzoefu wa kazi alipokuwa serikalini anasema alishawahi kusimamia kesi mbalimbali zikiwemo za EPA, kuhujumu uchumi na jinai, hivyo anayesema kamati haina wazoefu nashindwa kumuelewa ametumia kipimo gani kutambua suala hilo.

Akizungumzia suala la upatikanaji wa Katiba Mpya, anasema kamati imejipanga vizuri kuhakikisha serikali inaharakisha suala hilo.

Anasema mbali na kushughulikia suala hilo, kamati imejipanga kuangalia sheria nyingine zenye matatizo ikiwemo sheria ya usafiri barabarani ambayo inatumia vifungu vya zamani katika utozwaji wa faini.

Mchengerwa anasema tayari ameshaziandaa sheria zaidi ya 20 ambazo wanatarajia kuzifanyia maboresho na siyo kujikita zaidi kwenye kutembelea miradi, kwani watazingatia sheria.

Aidha, anasema atatoa msaada wa sheria za jinai kwa kuwa ana utaalamu wa mambo hayo na kuishauri serikali iwe inatumia ushahidi wa kisayasi.

Anasema Tanzania imebahatika kuwa na maabara kubwa ya kisasa ya upimaji wa vinasaba, hivyo kamati itashauri kuona uwezekano wa kulisaidia taifa kwa kuitumia ili kuepusha watu kusingiziwa kesi.

Akielezea sababu ambayo ilimfanya kuacha kazi yake na kwenda kujiunga na siasa, anasema aliona ni vizuri kuwatumikia wananchi kwa njia nyingine.

Mchengerwa anasema ni vizuri kuwatumikia wananchi moja kwa moja ikiwa kuwaondolea kero ya maji, matatizo ya afya, elimu, barabara na miundombinu.

Mbunge huyo ambaye ni mwanafunzi wa shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema anazipigania changamoto hizo ili kuzipunguza ama kuzimaliza.

Kuhusu upatikanaji wa huduma za afya katika jimbo lake, amasema amepata mfadhili kwa ajili ya kuibomoa hospitali ya wilaya na kuijenga upya na kuweka vifaa vya kisasa kama ilivyo kwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

“Wapo tayari kufanya hivyo tunasubiria ruhusa ya serikali ili kuingia makubaliano ya muda fulani ya ukusanyaji wa mapato na baada ya hapo serikali itafaidika,” anasema Anasema siyo rahisi kwa serikali kujenga hospitali zote za wilaya na kwamba wafadhili hao ambao wanatokea nchi ya Uturuki wapo tayari kufanya kazi hiyo.

Anasema hospitali hiyo ya wilaya imejengwa tangu mwaka 1960, lakini kwa bahati mbaya imekuwa ikitoa huduma chini ya kiwango. Anasema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo za uhaba wa vyumba kwa ajili ya wazazi pamoja na chumba cha wagonjwa mahutihuti.

Kamati ya Mchengerwa ni miongoni mwa kamati ambazo baada ya kuundwa zililalamikiwa na wadau mbalimbali kwamba wamewekwa watu wasiokuwa na uzoefu wa masuala ya sheria.

Hata hivyo, Spika wa Bunge alisisitiza kwamba wabunge wote wapo sawa na kwamba hakuna aliye juu na mwenye uwezo wa kuongoza kamati kuliko wengine.

Habari Kubwa