Mechi 5 za kuamua ubingwa Yanga

11Feb 2019
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mechi 5 za kuamua ubingwa Yanga

UKIACHILIA mbali matokeo ya jana dhidi ya JKT Tanzania katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga ni kwamba Yanga imecheza mechi tatu mfululizo na kuambulia pointi mbili.

Katika mechi hizo imetupa pointi saba ambazo kama ingezipata ingejiweka vizuri kwenye mbio za kusaka na kuurejesha ubingwa wa  Ligi Kuu ambao msimu uliopita ulichukuliwa na mahasimu wao wa jadi, Simba.

Kwa sasa Yanga bado inaongoza Ligi Kuu ya Tanzania, lakini iko kwenye shinikizo kubwa kutoka kwa timu za Simba na Azam ambazo ndizo zinaonekana kuutaka ubingwa kwa maneno na kwa vitendo.  Hiyo ni baada ya kupoteza pointi hizo, hasa kwenye mechi za mzunguko wa pili ambao unaonekana kuwa mgumu, Yanga inatakiwa iwe makini na baadhi ya mechi ambazo huenda kwake zikawa ngumu  zaidi. Hizi ndizo zinaweza zikaamua kama Yanga inaweza kuwa bingwa msimu huu...

 

1. Yanga vs Simba

Mechi hii ya watani wa jadi kwa mujibu wa ratiba ya awali itachezwa Ijumaa ya Februari 16 wiki hii.

Hata hivyo, kwenye ratiba mpya ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), kwenye mtandao haipo, badala yake baada ya mechi za Februari 11  leo Jumatatu, inaonyesha kuwa mechi nyingine ya ligi itakuwa  Februari 22 kati ya Simba na Azam FC. Hata hivyo siku yoyote mechi hiyo itakapochezwa, kama Yanga inataka kutwaa ubingwa msimu huu, hii ni moja kati ya mechi muhimu kwake kushinda kwa sababu itakuwa imechukua pointi tatu kwa timu ambayo inagombea nayo  ubingwa.

Pia ushindi wowote dhidi ya watani wa jadi, unaweza kusababisha ari kwa wachezaji wake, pamoja na kuwafanya wapinzani wao kuingia  kwenye mzozo wa wao kwa wao kutokana na kwamba wanaamini  timu yao si ya kufungwa na Yanga.

Kwa maana hiyo, wanachama, mashabiki wa wapinzani wao wataanza  kukata tamaa na hata wachezaji wa Simba watakuwa hawana tena ari  ya kupambana na hiyo itakuwa ni faida kwa Yanga. Vinginevyo kama itapoteza mechi hiyo, basi inaweza kutoa tena nafasi kwa Simba.

 

2. Yanga vs Mtibwa Sugar

Yanga kama kweli inataka kutwaa ubingwa msimu huu, basi moja ya mechi ambazo kwake ni ngumu na inatakiwa kushinda ili kufanikisha lengo lake ni dhidi ya Mtibwa Sugar.

Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa Aprili 17, mwaka huu kwenye  Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Umuhimu au ugumu wa mechi hiyo unakuja kutokana na kwamba Mtibwa inapocheza kwenye Uwanja wa Jamhuri inakuwa 'siyo ile' inayocheza kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba na Yanga hupata tabu sana kushinda kwenye uwanja huo, hivyo kama itapata ushindi basi itakuwa imepata pointi tatu kwenye moja ya  mechi ngumu na kuisogeza karibu zaidi na ubingwa, lakini kama ikipoteza au sare, bado itakuwa kwenye wakati mgumu.

 

3. Yanga vs Azam

Kivumbi na jasho kitakuwa Aprili 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakati Yanga itakapopambana na Azam FC.

Kwa Yanga ni moja kati ya mechi ngumu ambazo kama ikipita hapo, basi itakuwa karibu zaidi na ubingwa.

Mara nyingi mechi kati ya Yanga dhidi ya Azam huwa ni ngumu, lakini zaidi timu hizo zote zinaonekana kuusaka ubingwa kwa udi na uvumba,  hivyo haitokuwa mechi rahisi hata kidogo.

Sare yoyote au kupoteza mechi hiyo kwa Yanga, basi ubingwa unaweza ikausikia kwenye bomba.

 

4. Yanga vs Mbao FC

Yanga itakutana na Mbao FC kwenye mechi ya Ligi Kuu katika Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.

Timu za Simba na Yanga huwa kwenye wakati mgumu kukutana na Mbao FC kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Timu hiyo iliitoa Gor Mahia kwenye michuano ya SportPesa,  hivyo imeendelea kuwa tishio. Kwa Yanga hii ni moja kati ya mechi zenye milima na mabonde, ambazo  wanachama na mashabiki wake wanaitazama kwa jicho la pekee.

Ushindi kwenye mechi hii ni muhimu kuelekea mbio za ubingwa na kufungwa au sare basi hali itakuwa ni ngumu.

 

5. Yanga vs Azam FC

Hii ni mechi ya mzunguko wa pili kati ya Yanga dhidi ya Azam FC. Hii itakuwa ni moja kati ya mechi tano ngumu zaidi kwa Yanga kwenye  kipindi hiki kilichobaki.

Kama Yanga inashinda mechi hizo tano, hapana shaka hakutokuwa na kizuizi cha kutwaa ubingwa, lakini kama itatetereka, basi hata msimu  huu ubingwa inaweza kuusikia kwenye bomba.

Habari Kubwa