Mechi 7 zitakazoamua bingwa EPL

11Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mechi 7 zitakazoamua bingwa EPL

LIGI Kuu ya England inaendelea kuchanja mbuga ikielekea tamati yake Mei mwaka huu. Mbio za kuwania ubingwa huo zimekuwa  za moto.

Manchester City baada ya kuwa nyuma ya Liverpool kwa muda mrefu, jana ilitarajiwa kuifikia tena kileleni mwa msimamo mwa ligi hiyo kama ingepata matokeo dhidi ya Chelsea.

Hata hivyo, Man City itakuwa mbele kwa mechi moja zaidi ya Liverpool ambayo ina kiporo na hivyo ina nafasi ya kuipiku zaidi.

Lakini mbio za ubingwa za safari hii zinaonyesha kuwa na ushindani mkubwa, huku Tottenham nao wakifukuza mwizi kimyakimya wakiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo huo.

Hivyo, hapa tunachambua mechi saba za ligi hiyo zinazoweza kutoa taswira halisi ya ubingwa unakwenda kwa timu gani...

 

7. Bournemouth vs Man City (Machi 2, 2019)

Manchester City itacheza na kikosi hicho cha kocha, Eddie Howe katika dimba la Vitality ukiwa ni mchezo wao wa 29. Ingawa Bournemouth wana michezo mingine migumu dhidi ya Chelsea na Everton.

Manchester City imepoteza mechi nne za Ligi Kuu msimu huu na moja tu ndio wamefungwa na timu kubwa sita za juu.

Wakati unaweza ukawa mchezo mgumu kwao, kwani City msimu huu udhaifu wao umeonekena zaidi kwenye mechi dhidi ya timu ndogo, na wamejikuta wakifungwa kirahisi.

Zaidi ni kwamba Bournemouth imekuwa na matokeo mazuri zaidi kwenye uwanja wake wa nyumbani wakiwa wamefungwa mara tatu tu. Ushindi wao mnono dhidi ya Chelsea ulionyesha kwamba, wako imara zaidi wanapocheza kwenye uwanja wao wa Vitality.

Hata kama Bournemouth wanaweza wasiwe na upinzani mkubwa wanapowakabili City kati ya sasa na mwishoni mwa msimu, lakini kwa uhakika kabisa vijana hao wa dimba la Etihad watakuwa na kazi ya ziada ya kufanya.

 

6. Everton vs Liverpool (Machi 3, 2019)

Wikendi ambayo Bournemouth watakuwa wakicheza na Manchester City pia kutakuwa na mchezo wa ‘dabi’ ya Merseyside.

Mchezo wa kwanza wa wapinzani hawa wa jiji moja, ulishuhudiwa Liverpool wakiibuka na ushindi dhidi ya Everton kwa bao la utata la dakika za mwisho la Divock Origi.

Kwa wakati huu, Liverpool wana tatizo kubwa kwenye safu yao ya ulinzi na mabeki wake ambao ni majeruhi hawatarajiwi kuwa fiti kabla ya mchezo huo dhidi ya Everton. Hivyo Everton wanaweza kuwa na nafasi nzuri ya kulipiza kisasi dhidi ya Wekundu hao katika Uwanja wa Goodison Park.

Kwenye karatasi, Everton inaonekana kutokuwa imara zaidi ya Liverpool. Lakini mchezo huo wa ‘dabi’ mara zote unakuwa na matokeo ya kushangaza.

Ushindi kwa Liverpool kwenye mchezo huo, unaweza kuwapa nafasi nzuri zaidi ya kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutwaa taji la ligi hiyo.

 

5. Man United vs Man City (Machi 16, 2018)

Mchezo huu wa ‘dabi’ ya Manchester ni moja kati ya mechi inayokuwa na ushindani mkubwa zaidi kwa timu za jiji moja. Ingawa Manchester City waliichapa Manchester United kwenye mchezo wa kwanza pale Etihad, lakini sasa mambo yanaonekana kuwa tofauti kabisa.

Tangu kuondoka kwa Jose Mourinho, United imerudi kwenye kiwango kizuri zaidi chini ya kocha wa muda, Ole Gunnar Solskjaer na hadi sasa hajapoteza mchezo wowote. 'Mashetani Wekundu' hao wameonyesha kuwa na safu imara zaidi ya ushambuliaji, ambayo ilikosa meno kipindi cha Mourinho.

Pamoja kwamba, ‘dabi’ hii itakuwa na ushindani mkubwa, lakini staili ya uchezaji ya United imeimarika zaidi ya ile ya City.

United safu yake ya ushambuliaji ikiongozwa na Marcus Rashford na Anthony Martial inaweza kuwa na nafasi kubwa ya kupenya ngombe ya mabeki kama John Stones, Kyle Walker na Nicolas Otamendi. Hivyo Guardiola kwa namna yoyote akitaka kupata ushindi kwenye mchezo huu ni lazima abadilishe baadhi ya mbinu zake.

 

4. Chelsea vs Tottenham (Februari 27, 2019)

Mchezo wa Chelsea dhidi ya Tottenham umekuwa mmoja wa michezo yenye gumzo kubwa jijini London kwa miaka mingi.

Kwa sasa Spurs wachezaji wake wengi muhimu wanakabiliwa na majeraha, wakiongozwa na nyota wao muhimu, Dele Alli na Harry Kane.

Na kuelekea mchezo huo, wachezaji bado watakuwa hawajarejea uwanjani, hivyo Spurs itakwenda Stamford Bridge ikikabiliwa na changamoto kubwa.

Katika msimamo Tottenham wapo nyuma ya Liverpool kwa pointi tano na wao wana matumaini ya kuwa kwenye mbio za ubingwa. Hivyo, upinzani wao na Chelsea ni muhumu zaidi kuliko ilivyokuwa miaka mitatu iliyopita.

Kwa kipindi cha miaka michache iliyopita, Spurs imejijengea heshima kubwa ya kupambana na timu kubwa na kuzitoa nishai, hivyo pia wanaweza kufanya tofauti dhidi ya Chelsea.

Kama Spurs itawazuia wapizani wao hao kutoka London Magharibi, pengine wanaweza kujiweka kwenye nafasi nzuri zaidi katika tatu bora.

 

3 Liverpool vs Tottenham (Machi 31, 2019)

Wakati timu tatu za juu zote zikiwa kwenye nafasi nzuri katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu, Spurs kwa uhakika kabisa ndiyo yenye ratiba ngumu zaidi hasa wakati watakapoikabili Liverpool pale Anfield.

Wakati timu hizo zilipokutana kwenye mchezo wa kwanza, Liverpool walipata ushindi wa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Wembley. Na ushindi mwingine kwa Liverpool unaweza kuimarisha mbio zao za ubingwa, huku wakiondoa kabisa tishio la Tottenham.  

Mchezo huo utapigwa mwishoni mwa Machi, na wakati huo ndio wachezaji wengi watakuwa wakirudi kutoka chumba cha majeruhi na kuwa fiti.

Kama timu zote zitakuwa na vikosi imara, faida itakuwa kubwa zaidi kwa Liverpool. Kwanza watakuwa wakicheza nyumbani, mchezo huo utakuwa muhimu kwa Liverpool kushinda.

Bado, katika miaka iliyopita, mchezo unaozikutanisha timu hizi umekuwa mgumu kwa Liverpool kushinda.

Zaidi ni kwamba, ushindi kwa Spurs utawaweka kwenye nafasi nzuri ya mbio za ubingwa. Wakati timu hizo mbili zitakapokutana, tayari zitakuwa zimeshacheza mechi 31.

 

2. Man United vs Liverpool (Februari 24, 2019)

Hawa ndio wapinzani halisi wa soka la Uingereza. Liverpool kwa sasa ipo juu ya Manchester United kwenye mbio za ubingwa, lakini zinapokutana mambo yanakuwa tofauti kabisa.

Katika ratiba ya mechi ngumu na zenye ushindani, mchezo huu ndio upo jirani zaidi. Kwa wakati huu, Liverpool inakabiliwa na wachezaji wake wengi kuwa majeruhi na Klopp atakuwa na wakati mgumu kwenye safu yake ya ulinzi.

Hivyo, United wataingia uwanjani wakiwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kupata ushindi dhidi ya Liverpool.

Ingawa ushindi kwa United utaipa nafasi Manchester City kwenye mbio za ubingwa, lakini Mashetani hao nafasi pekee wanayoweza kuishika ni ile ya nne kwenye msimamo.

 

1. Man City vs Tottenham (Aprili 20, 2019)

Bingwa mtetezi atakutana na Spurs kwenye Uwanja wa Etihad ukiwa ni mchezo wa 35 kwenye Ligi Kuu. Zaidi ni kwamba mchezo huu utakuwa wa kupigania nafasi ya juu, hasa kama Spurs itakuwa imerudi kwenye mbio za ubingwa.

Mara ya mwisho Ligi Kuu ya England kushuhudia timu tatu zikipigania ubingwa kwa pamoja ilikuwa ni msimu wa 2013-14, wakati Steven Gerrard alipofanya makosa yaliyoipa nafasi City.

Katika mchezo huo wa 35, angalau wote watakuwa na kitu fulani chakuonyesha. Kwani kila moja itakuwa na wakati wa kuonyesha ubora wake kuelekea kwenye mbio za mwisho mwisho za ubingwa.

Katika timu hizo tatu, ni City pekee ndiyo yenye uzoefu wa kushinda taji la Ligi Kuu hivi karibuni.

Hivyo mchezo huo utakaopigwa kwenye dimba la Etihad katikati ya Aprili utaweza kutoa sura kamili.

Na mwisho wa siku ndio pia mchezo utakaomtambulisha bingwa mtarajiwa wakati ligi hiyo itakapofikia tamati Mei 12, mwaka huu.

Habari Kubwa