Mechi tatu zilivyompeleka Kessy Stars

20Mar 2017
Adam Fungamwango
Nipashe
Mechi tatu zilivyompeleka Kessy Stars

MECHI tatu alizocheza kwa kiwango cha juu, zimemfanya beki wa Yanga, Hassan Kessy, kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars.

beki wa Yanga, Hassan Kessy.

Ni mechi hizo tu ndizo zilizomfanya kumnyang'anya namba Juma Abdul kwenye kikosi cha Yanga na hata timu ya taifa.

Mechi ya kwanza ilikuwa ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa ambayo alionyesha uwezo wa hali ya juu na kumshawishi kocha azidi kumpa nafasi.

Hakufanya makosa, kwani mechi ya pili ilikuwa ni Kombe la FA dhidi ya Kiluvya United, na alikuwa mmoja wa wachezaji waliotia fora na kuifanya Yanga kuondoka na ushindi wa mabao 6-1.

Mechi nyingine ilikuwa ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Zanaco, Yanga ilipotoka sare ya bao 1-1. Siku mbili baadaye, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga alitaja jina la Kessy kuwa ni mmoja wa wachezaji waliochaguliwa kwenye kikosi hicho kipya.

Awali, ilionekana ni kazi sana kwa beki huyo kuichukua namba kutoka kwa Abdul, lakini majeraha yalimfanya beki huyo kukaa muda mrefu bila kucheza na hata aliporejea dimbani, kiwango chake bado hakikuridhisha.

Tangu kujiunga na Yanga, Kessy alikuwa bado hajapata namba ya kudumu kama ilivyokuwa Simba. Alijiunga na Yanga msimu huu akitokea Simba, japo kulikuwa na mizengwe mingi na matatizo mengi ya kisheria na kikanuni kwenye usajili wake.

Hatimaye, Shirikisho la Soka nchini (TFF), ikamuidhinisha kuichezea Yanga, licha ya malalamiko kutoka Simba, ingawa baadaye timu yake mpya iliamriwa kuwa imlipe.

Mwenyewe anasema, kasi, kupiga krosi na pasi za uhakika zenye ubunifu ni staili ya uchezaji wake na kipaji binafsi.

"Kilichonifanya nifike hapa ni siri ya mpira na wazazi," anasema na kuongeza.

"Mchango wa wazazi uko poa, wananipa ushauri kabla ya kucheza mechi mpaka ninapokuwa mapumziko, nawashukuru kwa mchango wao," anasema beki huyo.

Kwenye kikosi cha timu ya taifa, Kessy atakutana na beki Shomari Kapombe ambao wote ni wazaliwa wa Morogoro na wamelelewa kwenye 'academy' moja ya Morogoro Youth Academy kwa miaka tofauti, ikiwatoa pia kina Miraji Adam, Ayoub Kitala, na Edward Cristopha.

Hata hivyo, Kessy anasema alianza kucheza soka akiwa kama winga wa kulia, lakini alipojiunga na timu ya taifa ya Vijana chini ya miaka 20, iliyokuwa inafundishwa na marehemu Sylvester Marsh mwaka 2009, alimrejesha kucheza beki wa pembeni kutokana na mfumo wa kocha huyo.

Baada ya kupata mafanikio kutokana na kipaji chake alijiunga na Timu B ya Mtibwa Sugar.

Hata hivyo, kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa anaonyesha haikupita muda mrefu akapandishwa kwenye kikosi cha kwanza.

Alianza kushawishi makocha na viongozi wa klabu nyingi, lakini ni Simba iliyofanikiwa kumsajili kwenye kipindi cha dirisha dogo msimu wa 2014. Akawaharibia kabisa kina William Lucian ‘Gallas’ na Masoud Nassor ‘Cholo’ ambao rasmi aliwaweka benchi.

Alisoma shule ya msingi Mchikichini Morogoro kabla ya kujiunga na Sekondari ya Jitegemee jijini Dar es Salaam.

Habari Kubwa