Mechi zitakazoamua maisha ya Solskjaer Utd

21Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mechi zitakazoamua maisha ya Solskjaer Utd

KATIKA mchezo dhidi ya Tottenham, Ole Gunnar Solskjaer alionekana kama amepagawa. Aliweza kuwabana wapinzani wake kwenye kipindi cha kwanza kwa mbinu zake, ambazo baadaye zilimwezesha kupata bao lililowapa ushindi.

Ole Gunnar Solskjaer

Hata hivyo, wakati Spurs walipokuwa wanalishambulia zaidi goli lao kipindi cha pili, Solskjaer alionekana kuogopa. Alijaribu kuchanganya vitu, lakini golikipa wake, David De Gea alikuwa msaada mkubwa kwake na kwa United.

Ushindi kwenye dimba la Wembley umewafanya United sasa kuwa kwenye mbio za kuwania kumaliza katika nafasi nne za juu kwenye ligi.

Huku Solskjaer akiwa amepewa nafasi hiyo ya ukocha kwa muda hadi mwishoni mwa msimu baada ya kufukuzwa kwa Jose Mourinho, sasa anaonekana kuitaka nafasi hiyo moja kwa moja.

Pamoja na yote, hapa tunakuchambulia michezo mitano inayomkabili raia huyo wa Norway ambayo inaweza kumtengenezea majaliwa yake mazuri zaidi ya kupewa kazi hiyo kwa mkataba wa kudumu.

 

5. Arsenal (ugenini) – Ligi Kuu: 09/03/2019

Wakati ambao Manchester United watasafiri kwenda kwenye Uwanja wa Emirates kuikabili Arsenal, msimamo wa Ligi Kuu ya England unaweza kuwa tofauti kwa pande zote mbili. United kwa sasa wamecheza mechi saba bila kufungwa na wamecheza na Liverpool tu kati ya timu kubwa tano kabla ya kuwavaa  'Washika Bunduki' hao.

Kwa upande wa Washika Bunduki, wamepoteza mechi zao tatu kati ya sita kwenye Ligi Kuu, na kabla ya kuwakaribisha United hapo kwenye dimba la Emirates, watakuwa na kibarua dhidi ya Tottenham na Manchester City.

Wakati ikiwa ni vigumu kufikiri kwamba United inaweza kuendelea na kiwango chake hiki hadi Machi, ni upuuzi kudhani kwamba Arsenal haitaweza kuanza kushinda. Katika mchezo huo, unaweza kuwa kwenye utawala wa mabao na hakuna anayeweza kudhani.

Solskjaer atakabiliwa na mchezo mgumu kwa sababu United akili zao wamezielekeza kwenye kuwania nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ili wamalize nafasi nne za juu. Na Arsenal ni miongoni mwa timu zinazowania nafasi hiyo. Kasi ya ushambuliaji ya kikosi hicho cha Emery itahitaji mbinu mpya dhidi ya raia huyo wa Norway.

 

4. Chelsea (nyumbani) – Ligi Kuu: 27/04/2019

Mchezo dhidi ya Chelsea umepangwa mwishoni mwa Aprili, na mbio za kuwania nafasi nne za juu zitakuwa zimekwisha. Hata hivyo, Blues kwa sasa wapo nafasi ya nne, nafasi ambayo Solskjaer lazima aipiganie kwa ajili ya kuendelea kubakia kuwa kocha wa Manchester United mwishoni mwa msimu.

Chelsea kwa sasa wana pointi 47 katika mechi 23 walizocheza na wamefunga mabao 40, huku wakiruhusu mabao 19. United kwa sasa wana pointi 44, pointi tatu nyuma yao na wamefunga mabao 46 na kuruhusu mabao 33. Na kwa kuwa ukweli ni kwamba United imeizidi Chelsea kwa mabao ya kufunga tangu Solskjaer achukue mikoba, ina maana kwamba wamefanya vizuri.

Kikosi cha Maurizio Sarri kilianza Ligi Kuu England kwa kucheza mechi 12 bila kufungwa, ambapo walifunga mabao 27 na walishinda michezo nane. Hata hivyo, Chelsea tayari imepoteza mechi nne. United walipocheza pale Stamford Bridge walitoka sare ya 2-2 chini ya Mourinho, hata hivyo, Solskjaer atakuwa na nafasi nzuri ya kuifanya timu yake icheze kwa kiwango cha juu.

 

3. Arsenal (ugenini) – Kombe la FA: 25/01/2019

Kiufundi michuano ya Kombe la FA ndiyo nafasi ngumu zaidi kwa United ya kupata taji msimu huu. Ingawa United bado wapo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la FA ndio nafasi nzuri zaidi kwa Solskjaer kuwa na nafasi ya kumaliza msimu huu akiwa na taji litakalomwezesha bodi ya United kuwa na nafasi nzuri ya kumpa mkataba wa kudumu katika kikosi hicho.

United imeanza Kombe la FA chini ya uongozi wa raia huyo wa Norway msimu huu, kitu ambacho kitampa Solskjaer hamasa ya kuweza kupata mafanikio. United imeshinda mchezo wake wa raundi ya tatu dhidi ya Reading mwanzoni mwa mwaka huu na wamepangwa kucheza na Arsenal kwenye raundi ya nne, ambapo mchezo huo utapigwa mwishoni mwa Januari hii.

Washika Bundiki hao wameshinda mashindano hayo kwa rekodi yao mara 13, moja zaidi ya United, kitu kinachofanya mchezo huo kuwa wa kuvutia zaidi. Msimu uliopita, United walikuwa na nafasi nzuri kwenye mashindano hayo, walifungwa na Chelsea kwenye fainali Mei. Wakati huu, Solskjaer atakuwa akicheza michuano hiyo kwa umakini mkubwa, hii itakuwa ni moja ya nyakati za kuvutia zaidi akiwa kocha wa United.

 

2. Manchester City (nyumbani) – Ligi Kuu: 16/03/2019

Wakati linapokuja suala la Manchester ‘Dabi’, inaonekana wazi kwamba United wamekuwa wanaonewa zaidi kwa siku za hivi karibuni. Manchester United inachukia kufungwa na Manchester City, hasa wakiwa nyumbani na watu wachache wanajua zaidi kuliko Ole Gunnar Solskjaer. Kuibuka kwa Man City katika siku za hivi karibuni kumewafanya Mashetani Wekundu kunyanyaswa, hivyo mchezo huu utakuwa na kila aina ya upinzani, huku Man United wakitaka kumaliza ubabe kwa vijana wa Pep Guardiola.

United ilikwenda kwa City Novemba mwaka jana walichapwa 3-1 na tofauti ya ubora wa timu hizo mbili ilionekana wazi. Na mchezo huu utakuwa mtihani mkubwa kwa Solskjaer kuhakikisha kwamba anaibuka na ushindi. Lakini kucheza dhidi ya kocha mwenye uzoefu wa kutosha kama Guardiola, kunahitaji mbinu za ziada kuweza kufanikiwa kumfunga.

Mchezo wa kwanza wa ‘Dabi’ ya Manchester kwa Solskjaer unaweza kuwa mtihani utakaompa mafanikio au kumporomosha. Matokeo mazuri hapa yatamfanya kuwa na uhakika wa kupewa mkataba wa kudumu.

 

1. Liverpool (nyumbani) – Ligi Kuu: 24/02/2019

Moja ya mchezo wenye upinzani mkubwa kwenye Ligi Kuu ya soka Ulaya ni huu. Mchezo wa kwanza United ilichapwa na kikosi hicho cha Jurgen Klopp wakati wakiwa chini ya kocha Jose Mourinho. Ulikuwa ni mchezo wa mwisho wa Mreno huyo kukaa kwenye benchi la United na ndio ulikuwa moja ya sababu ya kutimuliwa hapo Old Trafford.

Wakati kwa sasa wakiwa wamepitwa pointi 16 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, hakuna kitu ambacho Solskjaer atakuwa akikitarajia zaidi ya kuhakikisha anaibuka na ushindi dhidi ya Liverpool.

Solskjaer sio mgeni kwa timu hizi mbili zinapokutana uwanjani, kwa kuwa hata wakati wake wa uchezaji anaujua vizuri upinzani mkubwa uliopo. Kwa vyovyote atakuwa akichukia kuwa kocha kwenye mchezo huu dhidi ya Liverpool. Solskjaer atakuwa na hamasa kubwa ya kuhakikisha anapata matokeo mazuri kwenye mchezo huo.

Liverpool hadi sasa imepoteza mchezo mmoja tu kwenye ligi na imefungwa mabao 13 katika mechi 23 walizocheza. Wamefunga mabao nane zaidi ya United na washambuliaji wao watakuwa na kitu fulani cha kuhitaji kufunga zaidi.

Lakini Solskjaer amethibitisha kwamba anaweza kutoa changamoto kwa kuiwezesha United kupata matokeo mazuri msimu huu, hivyo ni mchezo unaotarajiwa kuwa na upinzani mkubwa zaidi.

Habari Kubwa