Meneja wa Bandari 24 za Viktoria na simulizi ya kukokotoa bilioni 2/-

17Jan 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Meneja wa Bandari 24 za Viktoria na simulizi ya kukokotoa bilioni 2/-
  • Adai ameapa na lazima kutimiza
  • Sh. bilioni 8 zimeshaingia mfukoni
  • Vyanzo kuu 6, vidogo 18; mikoa 4

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) katika bandari zake za Ziwa Viktoria, imejipanga kuzitumia kuleta mapinduzi ya kiuchumi.

Bandari ndogo ambazo TPA inazisimamia kwa karibu.

Miongoni mwa mipango iliyojiwekea katika kufikia malengo hayo, ni kwenda sambamba na uboreshaji unaofanyika katika bandari zote zilizopo Ziwa Victoria.

Meneja wa Bandari hizo, Morris Mchindiuza, anasema tayari wameshatumia Sh. bilioni 16.5 katika miradi yake ya kimkakati kuboresha miundombinu ya Bandari za Ziwa Viktoria, ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

Anasema kiasi hicho cha fedha, kimetumika katika kipindi cha miaka miwili lengo, dira kuu ni kuziongezea uwezo bandari hizo ambazo ni muhimu katika kukuza uchumi wa nchi, ndani ya safari kuelekea uchumi wa kati kitaifa.

Mchindiuza anasema mikoa inayozungukwa na mikoa, ina bandari kuu sita na ndogo 18, zinazojumuisha bandari kuu za ziwa, ikiwamo ni pamoja na Mwanza Kaskazini, Mwanza Kusini, Nansio, Kemondo Bay, Bukoba na Musoma.

Mchindiuza anasema, kwa sasa miradi mingi inaendelea kutekelezwa na ipo iliyokamilika kwa asilimia 100 na mingine iko katika hatua za mwisho.

MAKUBWA?

Meneja Mchindiuza anataja anayoyaita ‘mambo makubwa’ yaliyofanyika katika maboresho hayo, ni pamoja na ujenzi wa magati, maghala, madaraja ya kuunganisha reli na meli, nyumba za kupumzikia abiria, vyoo, vyumba vya walinzi na ununuzi wa mitambo ya kuhudumia shehena.

Pia mengine anajumuisha uboreshaji mradi mkubwa wa bandari kavu ya Fela, uliopo katika hatua ya utwaaji wa eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 1,178 kutoka kwa wananchi ambao tayari hatua hiyo imekamilika, wakazi jirani kulipwa fidia kiasi cha Sh. bilioni 5.6.

Miradi mingine anaitaja ni ujenzi wa magati na thamani yake katika mabano; Lushamba (Sh. bilioni 1.2), Ntama (Sh. bilioni 2.2), Mwigobero (Sh. milioni 605) na Nyamirembe (Sh. bilioni 4.1).

Mchindiuza anataja ukarabati mwingine anautaja ni ujenzi wa jengo la ofisi na abiria awamu ya pili Sh. milioni 143.8, ujenzi wa gati la Magarini Sh. bilioni 1.7 na ukarabati wa daraja la Link Span katika Bandari ya Kemondo Bay Sh. milioni 815.7.

MATOKEO CHANYA

Meneja huyo anasema maboresho yameanza kuleta matokeo chanya, kwani katika kipindi cha miaka miwili, tayari shehena pamoja na mapato vimeongezeka maradufu.

"Katika kipindi cha miaka mitano 2014/15 hadi 2018/19 shehena iliyohudumiwa katika Bandari za Mwanza imekuwa ikipanda kwa wastani wa asilimia 0.5 kutoka tani 129,767 mwaka 2014/15 hadi tani 157,808 mwaka 2018/19," anasema Mchindiuza na kuongeza:

"Katika kipindi cha miezi minne ya kwanza ya mwaka 2019/20 Julai hadi Novemba mwaka jana tumehudumia tani 76,168 ikiwa ni sawa na asilimia 99.14 ya lengo la kuhudumia tani 76,833."

Pia anataja sababu zingine za kupanda shehena zinazosafirishwa ni kuendelea kuimarika reli ya kati, zikiwamo shehena za mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda Uganda, sambamba na kufunguka biashara katika ushoroba wa wanyama Ukanda wa Kati.

Mchindiuza anasema, jitihada za masoko zilizofanyika kurejesha wateja wakubwa waliokuwa wanatumia barabara ina nafasi katika mageuzi hayo ya kimasoko, sasa wakiumia huduma za meli, hatua iliyoiongezea TPA mapato kutoka Sh. bilioni 1.133 katika mwaka wa fedha 2014/15 hadi Sh. bilioni 1.422 mwaka 2018/19.

MATARAJIO

Mchindiuza anasema, matarajio yajayo ni kwamba katika mwaka uliopo wa fedha uliopo mkakati waliojiwekea ni kuingiza mapato ya Sh. bilioni mbili na katika robo ya kwanza ya mwaka huo, ambayo ni kati ya Julai hadi Novemba mwaka jana walikusanya Sh. milioni 802.

Anasema matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika makusanyo, yamesaidia kuongeza mapato katika bandari wanazotumia mfumo huo, ambazo ni: Kemondo Bay na Mwaloni, Kyamkwikwi, Mwanza Kaskazini na Kusini, Isaka, Mwigobero Bukoba na Mwalo wake na Nansio.

Mikakati mingine anaitaja ni kuhakikisha wanafikia lengo kubwa la bandari, kuwa lango kuu la uchumi wa nchi katika ukanda huo wa Ziwa Victoria ni kukomesha utitiri wa bandari bubu katika eneo hilo.

Anasema, tathmini waliyoifanya hivi karibuni, bandari bubu katika ziwa hilo zinafikia 300 katika kuhakikisha bandari hizo za Kanda ya Ziwa na zinaongeza ukusanyaji mapato, kutokana na huduma inazotoa, wameamua kuzitambua.

Meneja anasema katika kuzihakiki na kuzitambua bandari hizo, zipo baadhi ambazo zitafutwa kabisa na nyingine ambazo zitakidhi vigezo zitaingizwa katika mfumo maalum wa usimamizi.

“Hapa vinaangaliwa vitu vingi, eneo linapokuwa bandari hiyo bubu, mazingira kama ni salama au si salama, na zile ambazo zitakuwa na sifa zitarasimishwa na kuingizwa kwenye mfumo maalum wa usimamizi,” anasema Mchindiuza.

Anaongeza: “Tumebaini kwamba bandari hizi ndizo zimekuwa zikitumika kupitisha bidhaa haramu na kwa sababu tumepakana na nchi nyingi jirani katika ziwa hili, hatuwezi kuruhusu hali hii iendelee. Tunazirasimisha na zitasimamiwa na mamlaka zote ikiwamo zinazohusika na afya na nyinginezo zitakuwapo katika kila bandari.”

Mchindiuza anasema, mbali na kudhibiti bandari bubu, pia TPA imepewa jukumu ya kuendeleza bandari, kuendesha, kutangaza huduma zake kwa kushirikiana na sekta binafsi katika uendeshaji wake.

Anasema meneja wa bandari zilizopo ukanda huo, amejiwekea malengo kuleta mageuzi ya kiuchumi, kupitia bandari katika ukanda wa ziwa hilo.

“Unajua kipindi cha nyuma bandari nyingi zilikufa, lakini serikali ya awamu ya tano imeamua kuzifufua, na kwa jambo hilo sisi watendaji wa TPA tumeamua kupambana, kuendeleza juhudi hizi alizozianzisha Rais wetu Dk. John Magufuli.

“Kwa Ziwa Viktoria nimejiwekea malengo ya kuhakikisha bandari zetu zinaboreshwa na kuwa za kisasa kwa lengo kubwa moja la kuleta mapinduzi ya kibiashara,” anasema Mchindiuza.

“Hili ni lengo ambalo nimeapa na lazima litimie, lazima tuhakikishe bandari zote zinafufuka na kufanya kazi saa 24, miundombinu hii tunayoiboresha, naamini hakuna mfanyabiashara atayeshindwa kufanya kazi na sisi na tumewaandalia mazingira mazuri ya kibiashara katika bandari zote za ziwa hili,” anasema.

Mchindiuza anasema, TPA inaweka mkakati kukusanya mapato ya ndani kwa kuhakikisha wafanyabiashara wa uhakika ambao wanatumia bandari, kwa sababu usafirishaji wa majini una gharama nafuu zaidi.

Habari Kubwa