Messi anapomfunika Ronaldo ni hapa tu

11Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Messi anapomfunika Ronaldo ni hapa tu

BAHATI mbaya kwa wachezaji wa kizazi chao ni kwamba, wachezaji hawa wawili ndio wamekuwa bora zaidi kwenye historia kati ya wengi wao.

Lionel Messi

Ni wachezaji wa wakati wote, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, wametengeneza ushindani na upinzani mkubwa zaidi kuliko katika mchezo mwingine wowote.

Wawili hao wametawala soka kwa muda mrefu, na kubadilisha kabisa taswira ya mchezo wenyewe na kuwa wa kuvutia na kisasa zaidi duniani.

Rekodi zimewekwa, rekodi zimevunjwa na kwa vyovyote wataendelea kuweka rekodi zaidi, huku kila mmoja akijinyakulia tuzo binafsi nyingi zaidi na mataji ya kutosha. Wanapostaafu wanatakiwa kujengewa makumbusho, ingawa tayari Cristiano amejengewa nchini kwake kwa heshima.

Ushindani kati ya wachezaji hawa wawili, umeibua mijadala mingi zaidi kila sehemu ya dunia kwa mamilioni ya mashabiki.

Pengine inaweza kuwa vigumu kuamua nani ni mchezaji bora kuliko mwenzake kwani kila mmoja uwezo wake dimbani umekuwa msaada mkubwa kwa timu anayoichezea.

Lakini katika makala haya, tunachambua ukweli wa mambo matano yanayoonyesha Messi ni mfungaji bora zaidi kuliko Ronaldo...

 

5. Ana uwiano bora wa mabao kwa mchezo

Wakati Ronaldo akiwa ana mabao mengi zaidi katika mechi zote alizocheza kuliko Messi (677 kwa 646), lakini ukweli ni kwamba Mreno huyo alianza kucheza soka miaka miwili kabla ya Messi, hivyo yeye ana mechi nyingi zaidi kuliko nyota huyo wa Argentina.

Messi amecheza jumla ya mechi 792 kwa klabu yake ya Barcelona na timu ya Taifa ya Argentina hadi sasa tangu aanze kucheza soka na amefunga mabao 646, ikiwa ni sawa na uwiano wa mabao 0.81 kwa mchezo.

Na Ronaldo ana mabao 677 katika jumla ya mechi 945 alizocheza ngazi ya klabu ya nchi yake na hiyo ina maana kwamba ana uwiano wa kufunga mabao 0.71 kwa mchezo.

Wakati uwiano wao wa kufunga mabao ni wa kuvutia, ukweli ni kwamba Messi ana uwiano mzuri zaidi wa kufunga mabao 10 katika kila mechi 100 kuliko Ronaldo.

 

4. Ana kalenda bora ya mwaka ya mabao

Hapo zamani, Gerd Muller alikuwa mshambuliaji bora duniani wakati alipokuwa akifunga mabao wakati wa kipindi chake cha uchezaji kati ya mwaka 1960 na 1970.

Mwaka 1972, Mjerumani huyo alifunga jumla ya mabao 85 kwa klabu na nchi yake na kumfanya kuwa mchezaji bora kwa idadi ya mabao aliyofunga yeye mwenyewe kwa mwaka mmoja.

Rekodi hii ilikaa kwa muda wa miaka 40, hadi Messi alipokuja kuivunja na kuongeza mabao mengine sita na hivyo, kumfanya kuwa mchezaji mwenye mabao mengi zaidi kwa kalenda ya mwaka mmoja kwenye historia.

Wakati kalenda ya mwaka ya mabao ya Messi imesimama kwa mabao 91, Ronaldo aliweza kufikisha mabao 69 kwenye kalenda yake ya mwaka ya mabao.

Na hii inaonyesha Messi ni mfungaji bora zaidi kuliko Ronaldo.

 

3. Messi ana rekodi bora mechi alizokutana na Ronaldo

Kwa misimu tisa, Messi na Ronaldo walicheza pamoja kwenye Ligi Kuu ya Hispania, La Liga, kwa upande wa Barcelona na Real Madrid. Klabu zote mbili sio tu zilishindana kwenye mashindano ya ndani, lakini pia nje ya nchi.

Hata hivyo, wote Ronaldo na Messi walikuwa na rekodi zaidi kwenye mchezo unaozikutanisha timu hizo, El Clasico. Kwa mara ya kwanza wakikutana kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2008, huku Barcelona wakitolewa na Manchester United.

Mechi iliyofuata kwa wawili hao kukutana ilikuwa msimu uliofuata kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2009 na Barcelona wakalitwaa taji kwa kulipiza kisasi na kuwafunga Man United, huku Messi akiwa mmoja wa wafungaji.

Tangu hapo, wakawa wanakutana kwenye El Clasico au kwenye mechi za kimataifa, huku Messi akiibuka mshindi mara 16 dhidi ya mara 10 ya Ronaldo, wakati mechi tisa zikimalizika kwa sare.

Kwenye idara ya upachikaji mabao, Messi pia ameweka rekodi ya kufunga mabao 22 katika mechi 35 walizokutana wawili hao, huku Ronaldo akifunga mabao 19.

Hivyo katika rekodi ya walipokutana wao kwa wao Messi amemzidi zaidi Ronaldo.

 

2. Ana rekodi bora binafsi kwa msimu

Hapo zamani, washambuliaji wachache mno waliweza kufunga mabao 30 kwa msimu mmoja, huku kufikisha mabao 40 lilikuwa jambo gumu na hata wale waliofanikiwa kufikisha idadi hiyo, ilikuwa ni mara moja au mara mbili tu kwenye kipindi chote cha maisha yao ya uchezaji.

Lakini kwa soka la sasa Ronaldo na Messi kufikisha mabao 40 kwenye ligi limekuwa jambo la kawaida tu. Wote wawili wamefunga angalau mabao 40 kwenye mechi za mashindano yote kwa kipindi cha misimu nane, huku pia wakifikisha mabao 50 na 60.

Ronaldo alifikisha mabao 70 kwa msimu mmoja katika ngazi ya klabu kwenye mashindano yote, wakati Messi alifikisha mabao 73 kwa msimu wa 2011/2012 (huku 50 akifunga kwenye La Liga, 14 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na tisa kwenye mashindano mengine).

Msimu bora kwa Ronaldo ulikuwa ni ule wa 2014/2015 wakati alipofunga mabao 61, huku 48 akifunga kwenye La Liga, 10 kwenye Ligi ya Mabingwa na matatu kwenye mashindano mengine.

 

1. Messi ana rekodi ya kufunga mabao mengi La Liga kwa msimu

Kwa muda mrefu wawili hao wamekuwa wafungaji bora wa wakati wote wakishinda tuzo ya Viatu vya Dhahabu mara nyingi tu. Wakati Ronaldo alikuwa wa kwanza kuweka rekodi ya kufunga mabao 40 kwa msimu wa 2010/2011, akishinda kwa mara ya kwanza tuzo ya Kiatu cha Dhahabu kwenye La Liga kati ya tatu alizoshinda, Messi alikwenda mbali zaidi kwa kufunga mabao 50 kwenye La Liga na kuweka historia hadi sasa.

Habari Kubwa