Mfuko wa Mkapa wanavyopambana kujaza nafasi wazi za sekta ya afya

22Jul 2021
Nimi Mweta
Dar es Salaam
Nipashe
Mfuko wa Mkapa wanavyopambana kujaza nafasi wazi za sekta ya afya

WALIOFUATILIA tukio la kuenziwa hayati Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kwa kongamano lililoandaliwa na mfuko wa jina lake (BMF), walisikia takwimu ya kushangaza kuwa asilimia 70 ya nafasi katika zahanati, vituo vya afya na hospitali ngazi tofauti ziko wazi.

Hayati Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, alipokuwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Mfuko Benjamin Mkapa. PICHA ZOTE: MTANDAO.

Washiriki wa kongamano walielezwa kuwa nafasi hizo ni asilimia 50 ya nafasi zilizoko wazi katika utumishi wa umma wa jumla, hali ambayo inamaanisha kuwa serikali inajitahidi zaidi kujaza nafasi sekta nyingine kabla ya kufanya hizo sekta ya afya.

Kilichoelezwa ni jinsi mfumo huo unavyotumika kupunguza pengo hilo na siyo uwezo wa kulijaza.

Moja ya vianzio vya kutazamia kuwa pengo hilo linaweza kujazwa kwa ukamilifu kiasi fulani, ni matazamio kuwa yatakuwapo mazingira kwa vikundi na asasi huria kama Mfuko wa BejaminMkapa, ambazo kwa sehemu kubwa zina vianzio vya misaada kutoka kwa wafadhili, ili kufanya kazi zao bila matatizo.

Bado yako mazingira wezeshi kwa kiwango fulani kwa kutazamia kuwa asasi hizo zinaweza kuendesha shughuli zao kukidhi haja au matazamio, iwe kwa malengo yao wenyewe au miongoni mwa sehemu ya jamii wanayoihudumia.

Hata hivyo, mtu anaposikiliza bajeti zilizotajwa kwa mfano kwa upande wa Taasisi ya Benjamin Mkapa, siyo rahisi atazamie kuwa juhudi za asasi huria zinaweza kuziba mapengo ya wazi ya raslimali, uwezo serikalini.

Moja ya maeneo ambayo viongozi wa asasi hiyo ya Benjamin Mkapa, waligusia masuala kadhaa ya aina hiyo katika ufafanuzi wa shughuli zake katika sekta ya afya (ilianza na kusaidia mapambano dhidi ya UKIMWI na hasa kubadili mwelekeo wa jinsi watu wanavyoelezwa kuhusu afya zao, na ushauri unaofuata).

Rais Mstaafu Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alikiri kuwa utaalamu wa BMF uliisaidia wizara husika kubadili mwelekeo katika eneo hilo na kuwezesha ‘mwito na miitikio’ kuwa bora zaidi kati ya wahudumu au wataalamu sekta ya afya na wanajamii wanaohitaji huduma hizo.

Awali, kuulizia habari za maambukizi ya ukimwi ilikuwa ‘sumu.’ Kama ilivyo kawaida kwa sekta nyingine kama kilimo, viwanda, elimu, sayansi au teknolojia na nyingine kadhaa, suala la umuhimu unaotolewa kwa sekta ya afya liliwekewa mkazo, lakini si rahisi kusema kama serikali ingekuwa na majibu yoyote ya haraka kwa suala hilo.

HATUA IMEPIGWA?

Mtiririko wa takwimu, hata hivyo inaonyesha Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza kasi ya vifo vya uzazi, yaani vya mama na watoto wachanga na kwa upande mwingine kuna changamoto ya utapiamlo unaoathiri watoto wa chini ya miaka mitano.

Viwango vya vifo kuendelea ikiwa ni zao la uduni wa akili bado vinaleta shaka. Kinachojitokeza ni kwamba , ingawa si rahisi kuweza kutajwa katika hadhara kama ile kwa mazoea, bado ufadhili hasa unaelekea kwa mashirika ya misaada ya kibinadamu (hivi sasa wapo wanaoita ‘ya kiutu’) ya nchi za Magharibi.

Hadi sasa ni nadra kwa mfuko kama huo kutajwa nchini. Zipo angalau mfumo kama wa Hayati Reginald Mengi, kwamba alichokifuatilia kwa nguvu hayati Mengi kimefanyiwa kazi.

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, ina mazingira ya tiba bingwa katika maeneo kadhaa, ambayo miaka 10 iliyopita ilikuwa ni ndoto kupata huduma hizo nchini.

Tatizo la kuwapo taasisi huria zenye nguvu zinazoweza kuleta mabadiliko ya haraka katika jamii, yaani kuongezea nguvu katika kile idara za serikali zinachofanya, linagusa maeneo makuu mawili.

Moja ni kwamba, kuna vyanzo vya kiuchumi vinavyowezesha wanajamii kuungana au kuweka amana za misaada ya ‘kiutu’ kama sehemu mahsusi ya kile wanachokifanya, ambalo ni jambo la kawaida kwa mfano nchini Marekani.

Siyo rahisi kusema barani Ulaya kuna hulka ya matajiri kuingiza fedha zao katika mashirika kama hayo, kwani ni tofauti za utamaduni kati ya Ulaya na Marekani, zinazogusa maeneo mengine, kwa mfano uchangiaji wa wazi wa matajiri kwa vyama vya siasa, ambayo ni nadra kiasi fulani barani Ulaya.

Kuna eneo ambalo mabadiliko yanahitajika ili mwelekeo huo wa kijamii kwa kupunguza au kuondoa kodi (ya mapato) kwa shughuli zenye mwelekeo huo wa kijamii.

Ni linalotajwa pia kuhusiana na kukuza vipaji vya michezo au sanaa kwa watoto wa shule za msingi na sekondari.

Hivi sasa, hakuna asasi za wazi zinazojishughulisha utoaji misaada katika maeneo hayo. Mtu anapotangaza nia ya kusaidia eneo fulani anakuwa amejipeleka mwenyewe kuwa ana fedha nyingi, anapaswa kuanza kufuatiliwa ulipaji kodi wake, hata kuifanya jamii kujinasibu na ukwasi ulio nao.

Eneo jingine linatajwa kuwa uduni wa taasisi za wakfu katika jamii. Imezoeleka kwamba, mali za mtu binafsi na pale anapofariki wanagawana, na si dhihaka kusema kuwa kifo cha mtu mwenye fedha kinafuatiwa na ‘arobaini’ ya unywaji pombe miongoni mwa wanae.

Kulingana na ukwasi wa mtu huyo, fedha zikipungua ndiyo vijana hao wanaanza tena kuhangaika kama walivyozoea, baada ya kupoteza mamilioni ya fedha ambazo zingeingia katika mifuko ya kuongeza huduma za jamii kwa mfano katika afya, elimu na sanaa.

Ni kielelezo cha udhaifu wa mshikamano katika jamii na ni sababu isiyo ndogo ya wazee wasiojiweza kunyanyaswa wanapokwenda kufuatilia mafao, au kwenda hospitalini bila fedha ya kununua dawa.

Habari Kubwa