Mfumo wa udhibiti mwendo wa mabasi na sarakasi zake

13Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mfumo wa udhibiti mwendo wa mabasi na sarakasi zake
  • Baadhi waupinga wakidai unalenga kukusanya mapato zaidi
  • Wanaoukubali wasema unasaidia kufuatilia mienendo ya madereva wao
  • Nchi jirani ‘zatia timu’ nchini kujifunza

UNAWEZA kusema ni patashika nguo kuchanika kwa jinsi suala la mfumo wa kudhibiti mwendokasi wa mabasi nchini  kwa minajili ya kuhakikisha usalama wa abiria lilivyo na mvutano mkali baina ya wamiliki wa mabasi, madereva na taasisi za serikali.

Mnamo mwaka 2017 Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (LATRA), zamani SUMATRA ilianza kuufanyia majaribio mfumo wa kielektroniki wa kufuatilia mwenendo wa kasi ya magari, hususani mabasi ya abiria ujulikanao kama Vehicle Tracking System (VTS).

Hiyo ni katika kukazia sheria ya usalama barabarani (1973) ili kulinda usalama wa wadau wote wanaotumia barabara.

Hata hivyo, baadhi ya madereva na wamiliki wa mabasi wanapinga namna unavyoendeshwa, wakidai mfumo huo ni mradi unaolenga zaidi kukusanya mapato, badala ya kudhibiti mwendokasi ili kuepusha vifo na majeruhi vinavyotokana na ajali za barabarani.

Hoja hii inakanushwa vikali na mamlaka za serikali.

Mfumo huu unaohusisha kampuni binafsi zilizopewa kazi na LATRA kufunga vifaa maalum kwenye mabasi ili kuweza kusoma kuanzia namba za basi husika, mahali lilipo, linapopita pamoja na mwendo wake, umefanyiwa majaribio tangu mwaka 2017, na sasa unatumika rasmi kwenye mabasi zaidi ya 3,323 yanayofanya safari zake mikoa mbalimbali nchini.

MKURUGENZI

Mkulugenzi Mkuu wa LATRA, Gilliard Ngewe anasema tangu kuanza kutumika kwa mfumo huu, madereva wengi wameachana na tabia ya mwendo hatarishi kwasababu wanajua wanatazamwa muda wote na VTS.

Hatahivyo anasema wapo wachache wasiotii sheria ambao wanaadhibiwa kwa kuzingatia sheria, kanuni za LATRA pamoja na sheria nyinginezo za usalama barabarani.

“Ni mfumo wa kisasa kwani tuna uwezo si tu wa kuona dereva alipo na mwendo anaoenda nao, bali kujua hata sehemu ambazo dereva alifunga breki za ghafla,” anasema na kuongeza:

“Maofisa wa LATRA wanakuwa kazini muda wote wakipokea taarifa za mienendo ya mabasi yote… wanapoona yanayozidisha mwendo ulioelekezwa kisheria, wanatuma taarifa kwa polisi walio katika maeneo ya uelekeo wa basi au maofisa wa LATRA ili wachukue hatua kwa madereva husika.”

UWAMATA

Katibu wa Umoja wa Madereva wa Mabasi (UWAMATA), Abdallah Lubala hakubaliani na ufanisi wa teknolojia hii.

Anasema kama LATRA ina lengo la kudhibiti mwendokasi wa mabasi, inatakiwa kutumia mfumo wa kianalogia kwa kufunga vidhibiti mwendo (Speed governor) na si vifuatilia mwendo (VTS).

“VTS haizuii dereva kuzidisha mwendo, inapiga kengele tu mwendo unapozidi kilometa 85 kwa saa, wakati kidhibiti mwendo kinaweza kuzuia gari lisiongeze mwendo zaidi ya ule uliokubalika kisheria,” anasema na kuongeza:

“Mpaka sasa bado sheria zinatambua kidhibiti mwendo, hii VTS ni ya kibiashara zaidi…haiwezekani dereva apelekewe faini ya mwendokasi inayofikia milioni 11, akiuliza imekuwaje, anajibiwa kuwa alizidisha mwendo miezi minne iliyopita.”

Lubala anasema madereva wanalazimishwa kulipa mamilioni ya fedha, huku akitoa mifano ya madereva wawili anaodai walipelekewa ankara ya milioni 3 na milioni 11, na baadhi ya faini wakitakiwa kulipa Sh. laki mbili kwa kila kosa kwa mujibu wa kanuni za LATRA na si Sheria ya Usalama Barabarani inayotaja faini ya elfu thelathini kwa kila kosa.

MBUNGE ‘MSUKUMA’

Hoja zake zinaungwa mkono na Joseph Kasheku 'Msukuma', Mbunge wa Geita Vijijini na mfanyabaishara wa mabasi ya abiria mkoani Mwanza, Geita na Dar es Salaam.

Anabainisha  kuwa                          tayari        wafanyabaishara wameshatoa malalamiko kuhusu VTS na uendeshaji wake, kikiwemo kikao cha wamiliki wa mabasi na waziri mkuu kilichofanyika Juni 30, 2019 jijini Dodoma.

“Lengo la serikali ni kudhibiti mwendokasi na si kuwatumia madereva kama chanzo cha mapato… Wafanyabiashara tunasema tunahitaji kidhibiti mwendo na si kifuatilia mwendo…hili tulishamwambia hata waziri mkuu,” anasisitiza.

Msukuma anabainisha kuna ulazima wa serikali kutengeneza mfumo wa kuwa na mtoza faini mmoja na si madereva kutozwa faini na maofisa wa LATRA, na siku zingine polisi huku faini hizo zikiwa na tofauti kubwa.

“Mfumo wenyewe wa VTS, ‘seva’ zake zinashikiliwa na kuendeshwa na watu walio mtaani (kampuni binafsi), kwahiyo ni rahisi kuchezewa na wamiliki mfumo,” anasema na kuongeza:

“Kwanini LATRA wanashindwa kuuendesha wenyewe badala yake wanakuwa waangalizi tu?... Dereva wa Dar - Mwanza anaambiwa amezidisha mwendo mara 100, alipe faini milioni 3 wakati mshahara wake ni laki mbili kwa mwezi, haiwezekani.”

TRAFIKI

Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mratibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Deus Sokoni anafafanua hatua ambazo polisi huchukua unapojitokeza utata katika udhibiti wa mwendokasi.

"Sheria mama ya usalama barabarani ni Sheria ya Usalama Barabarani, imeruhusu uwepo wa kipima mwendo (speed radar), ambapo polisi tunaita tochi, na LATRA kupitia kanuni zao ndiyo wanatumia VTS,” anasema na kuongeza:

“Kisheria ushahidi wa mwendokasi unaorekodiwa na tochi ya polisi, ambayo askari anaishika na kulipiga picha gari linalokimbia huwa haubishaniwi hata mahakamani, ni ushahidi wa mwisho na unaojitosheleza.”

ASP Sokoni anasema VTS ni mfumo mzuri kubaini tabia za dereva na kumwajibisha ila si mzuri sana kiusalama barabarani kwasababu inachukua muda kurekodi mwendo, kutafuta taarifa za basi na kisha kuzituma na hivyo dereva anaweza kuwa ameshatenda makosa mengi yanayohatarisha usalama wa abiria.

“Tochi ya polisi ikimnasa dereva aliye kwenye mwendokasi, anasimamishwa na kupigwa faini pamoja na onyo… VTS inahitaji muda mrefu na inapotokea utata baina ya mwendo uliorekodiwa na VTS au tochi ya trafiki basi inazingatiwa zaidi tochi,” anasema na kuongeza:

“Hiyo ni kwasababu ipo kutokana na sheria mama na VTS ipo kutokana na kanuni za sheria nyingine… vivyo hivyo kwenye kutoza faini, faini ya polisi inazingatiwa zaidi.”

Katikati ya mwezi Julai, 2019 zilisambaa tetesi kupitia mitandao ya kijamii kuwa mfumo wa VTS umesitishwa kutumiwa na LATRA.

Hata hivyo, Julai 20, mamlaka hiyo ilitoa ufafanuzi ikisema makosa ya mwendokasi yaliongezeka kwa zaidi ya asilimia 230, ndani ya kipindi cha wiki mbili tu baada ya kuenea kwa taarifa hizo.

Aidha, ilifanya kikao na wamiliki wa mabasi na kusisitiza kutositisha na kwamba inaendelea kuchukua hatua kali kwa madereva.

TABOA

Katibu wa wamiliki wa mabasi (TABOA), Ernea Mrutu anasema mfumo wa VTS hauna shida kwani unawasaidia hata wamiliki wa mabasi kufuatilia mienendo ya madereva wao na kuokoa mafuta yanayopotea zaidi kutokana na mwendokasi.

Hata hivyo, Mrutu anaomba pamoja na uwepo wa VTS, pia kiongezwe kidhibiti mwendo ili kumzuia dereva asizidishe mwendo.

 

“Hatupingi VTS, mfumo huu unaunganisha LATRA na mmiliki wa gari na wote wanakuwa na uwezo wa kuona mwenendo wa dereva mwanzo mpaka mwisho wa safari. Madereva waendeshe mwendo unaokubalika kisheria,” anasema na kuongeza:

“Tumewaomba LATRA kwasababu wao ni wachache kuweza kukagua mwendo wa magari yote, basi watuunganishe TABOA tuwe na uwezo wa kuyafuatilia mabasi yote ili kuyabaini yanayouchezea mfumo na kuyaripoti…si kumuunganisha mmiliki mmojammoja tu na basi lake kama ilivyo sasa.”

UFAHAMU

Ingawa king’amuzi cha VTS kinachofungwa katika mabasi hupiga kengele kwa nguvu kila dereva anapozidisha mwendo wa Kilometa 85 kwa saa, lakini abiria wengi hawafahamu kengele hiyo huashiria nini.

Hiyo inasababisha wasichukue hatua zozote za kumuonya dereva ili apunguze mwendo, jambo linalohatarisha usalama wao.

Abiria wanne kati ya watano ambao mwandishi aliwauliza iwapo wanafahamu namna ya kutambua kama dereva wa basi alilopanda amezidisha mwendo, walisema hutumia njia za asili za kuangalia kasi ya kupishana na miti au kuyapita magari mengine.

Ni mmoja tu ndiye aliyesema husubiri kusikia mlio wa king'amuzi cha VTS kujua kama dereva wa basi anazidisha mwendo.

Eveline Joseph, ambaye hufanya safari kati ya majiji ya Dar es Salaam na Mwanza mara kwa mara anasema:

“Nimewahi kusikia mlio katika baadhi ya safari zangu, hususani ambazo nilipata viti vya mbele... sikuelewa kama ni VTS, kwasababu inalia kidogo na kunyamaza… hivyo askari ambao huingia ndani ya mabasi kutuuliza juu ya uendeshaji wa dereva, pia hutuelimisha abiria kuhusu vifaa hivyo.”

RAMADHANI HAKEEM

Ramadhani Hakeem ni abiria aliyekuwa akielekea Musoma kutokea Dar es Salaam wakati wa mahojiano na mwandishi wa makala haya. Anakiri kuifahamu VTS kupitia vyombo vya habari.

Anasema alimuona Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isaac Kamwele akitangaza uzinduzi wa mfumo wa VTS na namna unavyofanya kazi ndipo akaujua na kuanza kuufuatilia zaidi baada ya kusikia kuwa hata mtu binafsi anaweza kufunga kwenye gari lake.

“Baadaye nilijifunza zaidi kuhusu VTS kwa kusoma mtandaoni, na nikawa makini nikipanda basi nafuatilia kuona kama kengele ya VTS italia, ingawa mara kadhaa ambazo nilisikia ikilia sikuwahi kumwambia dereva apunguze mwendo kwasababu ya kuhofia abiria wenzangu kuniona msumbufu,” anasema.

TAKWIMU

Kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi nchini, jumla ya watu 61 wamefariki kati ya Januari mpaka Juni mwaka 2019, kutokana na ajali za mabasi, ukiwa ni wastani wa vifo vya watu 10 kila mwezi, huku asilimia kubwa ya ajali hizo zikisababishwa na mwendokasi.

Ripoti ya Usalama Barabarani ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), iliyotolewa mwaka 2018 inasema asilimia 30 za ajali barabarani katika nchi zilizoendelea hutokana na mwendokasi huku nusu ya ajali katika nchi za dunia ya tatu, Tanzania ikiwemo husababishwa na mwendokasi.

Tafiti za WHO zinabainisha zaidi kuwa kadri dereva anavyoongeza mwendo, ndivyo uwezekano wa ajali kutokea huongezeka.

“Gari linalokimbia kilometa 50 kwa saa litahitaji kusogea mita 13 zaidi mbele ili liweze kusimama na gari linalokimbia kilometa 40 kwa saa litasogea kwa mita 8.5 mbele ndipo liweze kusimama…kila inapoongezeka kilometa moja kwa saa na uwezekano wa kutokea kwa ajali uonaongezeka kwa asilimia tatu,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Katika mazingira haya, udhibiti wa mwendokasi ni suala muhimu kwa usalama wa abiria, ingawa jitihada za udhibiti wa mwendokasi wa mabasi nchini zinaonekana kuibua mvutano.

MWANASHERIA

Mwanasheria wa madereva wa mabasi nchini Frank Kisanga anasema madereva wamemuelekeza kufungua kesi kuhoji uhalali wa matumizi ya VTS katika mabasi pamoja na kutozwa faini kwa kutumia kanuni za LATRA, badala ya sheria ya usalama barabarani.

Ngewe anajibu madai hayo, akisema:

“Kama madereva hawataki kutozwa faini na mamlaka yetu waache udereva wa mabasi, wakaendesha magari binafsi ambayo hatuyapi leseni ya kufanya kazi,” anasema na kuongeza:

“Haiwezekani mamlaka ya usimamizi iwe haina mamlaka ya kuadhibu iliyowapa leseni za kufanya kazi husika… udhibiti mwendokasi unafanyika kuokoa maisha ya abiria na hata hao madereva walalamikaji.”

Ngewe anasema kuanzia mwaka 1996 walipokuwa wakifunga kidhibiti mwendo kinachozuia gari isiweze kuzidisha mwendo kwa kuzuia mafuta yasitumike, madereva walikuwa waking'oa au kuvichezea vifaa bila wao kujua.

“Mfumo wa sasa wa VTS unaweza kuona kama basi limezuia kifaa kilichofungwa kisifanye kazi… tunaona kwenye kompyuta zetu na kuchukua hatua… hatuwezi kurudi nyuma, mambo yanabadilika na teknolojia inakua,” anasema.

JIRANI WAJIFUNZA

Aidha, imebainishwa kwamba mataifa jirani yameshaanza kutuma maofisa wake wa masuala ya usalama barabarani nchini, kujifunza mfumo wa VTS, ili wakaanzishe katika mataifa yao.

Maofisa wawili wa Mamlaka ya Usimamizi wa Usalama Barabarani nchini Rwanda (ARUA), walifika nchini na kutumia siku mbili kujifunza mfumo huo miezi sita iliyopita.

Aidha, maofisa watano wa NTSA ya Kenya walifika Julai mwaka huu kujifunza mfumo huo kwa wiki moja.

Mkurugenzi Mkuu wa NTSA ya Kenya Francis Meja alipoulizwa na mwandishi kuhusu alivyouona mfumo wa VTS ameupa 'heko', na kusema wamebaini mabasi yanayosafiri kati ya Tanzania na Kenya yalikuwa hayazidishi kilometa 85 kwa saa yanapokuwa Tanzania.

“Lakini yakivuka mpaka wa Namanga na kuingia Kenya, yanakimbia mpaka kilometa 140 kwa saa kwani VTS haiwezi kutumika kuadhibu makosa yanayotendeka nje ya Tanzania,” anasema na kuongeza:

"Tumependa mfumo, tumejifunza na sasa tupo nyumbani Kenya tukianza kuandaa mazingira tuanze kuutumia na kuachana na kidhibiti mwendo…sisi hatutafunga VTS kwenye mabasi tu, tutafunga hata kwenye malori, na magari mengine ya kibiashara kama teksi.”

KITUONI

Mwandishi alipotembelea kituo maalum kinachopokea taarifa za VTS zinazohusu mabasi yote 3,323 yaliyofungwa vifaa hivyo, aliona uwepo wa maofisa wasiozidi 10 wa LATRA wanaohusika katika ufuatiliaji wa mienendo ya mabasi na kuripoti maeneo mabasi yanayokoelekea.

Katika mazingira haya si rahisi mabasi yanayozidisha mwendo kinyume cha sheria ya barabarani kubainika na kuripotiwa papohapo kwani inabidi maofisa hao watafute taarifa za basi mojamoja.

Kwamba inapobainika lililozidisha mwendokasi, taarifa zinatumwa linapoelekea ili hatua zichukuliwe.

Ufinyu wa rasilimali watu wa kufuatilia mabasi haya ndiyo unasababisha malimbikizo ya makosa na faini mpaka kufikia mamilioni kwa dereva mmoja.

Habari Kubwa