Mfungaji yupi wa kigeni atatikisa zaidi VPL?

14Aug 2016
Lasteck Alfred
Lete Raha
Mfungaji yupi wa kigeni atatikisa zaidi VPL?

LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) inatarajia kuanza wikiendi ijayo huku wachezaji wa kigeni wakipewa nafasi kubwa kwenye kinyanganyiro cha kutwaa taji la mfungaji bora wa msimu ujao.

Laudit Mavugo.

Licha ya kuwepo kwa mastraika wengi, wachezaji wa kigeni wa idara ya ushambuliaji wanapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri msimu ujao. Vyombo vya habari mbalimbali, wachambuzi wamekuwa wakiwataja washambuliaji kadhaa wa kigeni na kuwapa zaidi nafasi ya kufunga mabao mengi msimu ujao.

Hata hivyo hawakuwapuuza wale wazawa ingawa wamewapa nafasi kubwa wageni kufanya vizuri kutokana na kile walichodai kuwa wamesajiliwa wakiwa na viwango bora na wamekuwa wakionesha kuwa na uwezo mkubwa. Wanaotabiriwa kufanya makubwa ni;

Laudit Mavugo (Simba)

Ni mchezaji mpya tishio wa Simba, ameonyesha uwezo mkubwa kwenye mechi moja aliyoichezea timu hiyo. Mrundi Laudit Mavugo ametua Simba kutoka Vital’O ya Burundi ambapo kwa msimu uliopita alifunga magoli 30 kwenye Ligi Kuu.

Uwezo wa Mavugo huenda ukamfanya moja kati ya straika tishio zaidi msimu ujao. Kwa uwezo wake aliouonesha akiwa klabu hiyo ya Burundi ni wazi ni moja kati ya straika watakaopeleka Simba kwenye mafanikio makubwa msimu ujao.

Kocha mkuu wa Simba, Joseph Omog alisema, “ Nimekuwa naye kwenye mazoezi mara moja, anaonesha kuwa ni mchezaji mwenye nia, anajua anachotakiwa kukifanya. Ana nguvu na uwezo mzuri.”

Donald Ngoma (Yanga)

Kweli utendaji wa kazi kwa juhudi, unalipa. Alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa kigeni msimu uliomalizika miezi mitatu iliyopita

Mshambuliaji nambari moja wa Yanga, na raia wa Zimbabwe Donald Ngoma alionesha umahiri mkubwa wa kufunga mabao lakini pia kutoa pasi za mwisho kwenye mechi za Ligi Kuu. Straika huyo pia alionesha uhhodari mkubwa kwenye ukokotaji wa mpira lakini umakini kwenye upigaji wa pasi.

Straika huyu hatari amekuwa chachu ya mafanikio ya Yanga msimu uliomalizika na kuiwezesha klabu yake kutwaa ubingwa mbele ya klabu za Simba na Azam FC.

Kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm aliwahi kusema, “Ngoma amekuwa akipambana kwa nguvu kubwa kwaajili ya timu. Ni mchezaji mwenye uwezo wa kucheza kwa kipidi kirefu bila ya kuchoka.”

Frederick Blagnon (Simba)

Muivory Coast, Frederick Blagnon, anatajwa kuwa jiwe kuu la kati kwa klabu ya Simba msimu ujao, ametajwa kuwa ni mfungaji mzuri wa mabao mwenye uzoefu wa kufunga kwenye ligi na michuano ya kimataifa.

Straika huyo ameshuhudiwa kwenye baadhi ya mechi za kirafiki za Simba kule Morogoro na jijini Dar es Salaam na tathmini fupi ambayo imekuwa ikitolewa ni kuwa straika huyo ni mtaalamu wa kufunga mashuti makali na mwenye uwezo mkubwa wa kulenga goli.

Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema, “Ni mchezaji wa kimataifa, ana nidhamu nzuri na anajua ni nini kinachohitajika anapokuwa na mpira.”

Abasalim Chidiebere (Stand United)

Straika Mnigeria, Abasalim Chidiebere ni straika mwenye akili ya mpira, nguvu na maamuzi ya haraka anapokuwa karibu na goli.

Straika huyo alifanya vizuri msimu wa 2014/15 akiwa na Stand United akifunga mabao zaidi ya 12 lakini aliposajiliwa msimu uliopita kwenye klabu ya Coastal hali haikuwa nzuri kwani hakuweza kufunga mabao hata matano. Amerejea Stand na tayari ametabiriwa kufanya vizuri msimu ujao.

Kocha wa Stand, Mfaransa Patrick Liewig alisema, “Chidiebere ni mchezaji mzuri, ana nguvu na ana nidhamu nzuri hivyo sina wasiwasi kwa kuwa nina kikosi cha maana na nitakuwa nikimtegemea yeye kwenye ufunaji wa mabao.”

Amissi Tambwe (Yanga)

Licha ya kuwa kwa misimu mitatu amekuwa mfungaji bora wa ligi kwa mara mbili, straika wa Yanga anapewa nafasi kubwa ya kuendeleza rekodi ya ufungaji ambayo ameiweka tangu alipotua Tanzania.

Akiwa Simba alikuwa mfungaji bora kwa kufunga mabao 19 msimu wa 2013/14, msimu wa 2014/16 alihamia Yanga ambapo alimaliza akiwa kwenye nafasi ya pili akiwa na mabao 14 na msimu uliopita alikuwa mfungaji bora akifunga mabao 17.

Kocha Pluijm alisema, “Tambwe ni mfungaji bora, ni mshindi na anapenda timu yake ishinde kila inapokuwa inacheza.”
Mastraika wazawa;

Mastraika wazawa ambao watakuwa wakiwania vikali kiatu cha mfungaji bora ni; John Bocco (Azam), Dani Mrwanda (Kagera Sugar), Paul Nonga (Mwadui), Rashid Mandawa (Mtibwa Sugar), Jeremiah Juma (Prisons), Atupele Green (JKT Ruvu), Fully Maganga (Ruvu shooting), Waziri junior (Toto African) na Mohamed Mkopi (Mbey City).