Mganga Mkuu Sasa kazi, tuone vitendo kila mmoja akiwajibikia wagonjwa

14Jan 2021
Yasmine Protace
Mkuranga
Nipashe
Mganga Mkuu Sasa kazi, tuone vitendo kila mmoja akiwajibikia wagonjwa
  • Hospitalini wamuige waziri kutoa simu
  • ‘Whatsap’ nyenzo rasmi ya kufuatiliana

UNAPOZUNGUMZIA sekta ya afya, maana kubwa inaangukia maisha ya watu. Hata tafsiri pana ya kinachofanywa na Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MAMM) nchini, unaotekelezwa kwa wastani wa miaka 12 sasa, unaangukia hapo.

Mtazamo wake ni walau kila kijiji wakazi wawe jirani na zahanati inayowahudumia na katika kata kunakuwapo eneo la rufani, kituo cha afya, wilaya inapata hospitali na mkoa hospitali ya rufani, hali kadhalika ngazi ya rufani za juu na juu yake Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Lengo kuu hapo ni kutatua au kupunguza kero kutoka mikononi mwa jamii, jambo ambalo Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Abel Makubi, anayesema ni jambo ambalo serikali ipo tayari kuzipokea.

Anafafanua kuwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ipo tayari kupokea kero na malalamiko ya wananchi, endapo wameshindwa ama kusikilizwa au kusaidiwa na viongozi wa ngazi za chini na vituo vya kutoa huduma za afya waliko.

Ni angalizo lililojaa ufafanuzi, ambalo Prof. Abel Makubi alilitoa baada ya kufanya kikao kwa njia ya mtandao na viongozi wakuu wa sekta ya afya, kilichowajumuisha waganga wakuu wa mikoa na wilaya.

Wengine walioshiriki kikao hicho ni Wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa Huduma za Afya za Mikoa (RHMT) na wilaya (CHMT) na wakurugenzi wa hospitali za kitaifa na jumla ya washiriki ni 220, ajenda kubwa ikiwa ni kupunguza kero.

Prof. Makubi anasema, wananchi wana matumaini na serikali yao, jambo ambalo ni haki yao kusikilizwa na kutatuliwa kero kupitia watendaji kwenye vituo vyote vya huduma za afya nchini.

WOTE KUBEBA MZIGO

Mganga Mkuu anaongeza kuwa kamati zote zinapaswa kufanya tathmini za kero zote kwa muda wa wiki nne, kuzitatua, kuwasilisha ripoti ziarani pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI).

“Tunaanzisha utaratibu ambao sisi viongozi wa sekta ya afya tunaenda kutafuta kero kutoka kwa wananchi na kuzitatua. Hili ni agizo na tumekubaliana wasambae kwenye ngazi zote,” anabainisha.

“Kuanzia zahanati vituo vya afya na kwenye hospitali, tunatakiwa kuhakikisha wananchi wapate huduma bora licha ya kuwa tumeboresha huduma kwenye vituo vyetu,” anafafanua.

Prof. Makubi anasema ni utaratibu unaorahisisha kutatua kero za wananchi na kuwaupunguzia kero ambazo hazipaswi kuifika ngazi za juu kiutendaji, kama vile ofisi ya waziri, hivyo watendaji husika wanapaswa kujitafakari namna ya kutatua shida za wananchi.

“Tumekubaliana kuimarisha suala la uongozi, uwajibikaji na usimamizi, kwani kila mmoja ameona kuna upungufu kwenye usimamizi wa huduma za afya nchini.

“Hivyo, tumekubaliana kila kiongozi kuanzia taifa hadi vijijini kusimamia sehemu zenye upungufu, kwani wananchi wanahitaji mazuri kutoka kwetu. Hatuwezi kuwaridhisha kwa kila kitu, lakini tupunguze matatizo yao," anasema.

Upande wa vitengo vya huduma kwa wateja, Mganga Mkuu huyo wa Serikali, anasema kunahitaji maboresho zaidi na umma unahitaji kuchakata kero zote na kuzifanyia kazi.

Ni utekelezaji anasema unafuatwa kilichofanyika kubandikwa kwenye mbao za matangazo ya vituo vyao na wanapaswa kuwa hai wakati wote, kwa kuwa mwananchi wanataka huduma za afya kwamba namna ya ufanisi wanaotarajia.

“Viongozi hao pia wanatakiwa kukagua ndani ya hospitali zao kwenye maeneo ya kutoa dawa na stoo, kuona kama dawa zipo na zinawatosheleza wananchi na kama kuna wizi tuweze kuchukua hatua.

“Waende kwenye wodi na ‘OPD’ (wagonjwa wa nje) kuwasalimu wagonjwa na kama wana kero waziseme, ili wazitatue, pia maabara kuweza kuona kama vipimo vinafanyika,” anasema.

Mganga Mkuu anataja ubunifu mwingine unajumuisha kutumia makundi ya mitandao ya simu na ‘Whatsap’ wataopokea na kushughulikia kero kwenye kila wilaya au mkoa husika, ili kila mwananchi aweze kutoa kero zake.

“Tumeagiza kuwe na namba ambazo zitatangazwa kwa wananchi. Pia, wawashirikie wananchi kupitia mikutano na kutaja namba zao, ili wananchi wajue wanawasilisha vipi malalamiko yao,” anasema.

Prof. Makubi ana ufafanuzi kwamba wananchi wanapaswa kujenga imani na kuwaamini watendaji wote wa sekta afya, hasa kwa kufuata nyayo za waziri mwenye dhamana aliyetangaza namba zake za kupokea malalamiko.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu, ndani ya wiki mbili, Waziri Dk. Dorothy Gwajima, aliyetangaza namba ya malalamiko mwishoni mwa mwaka jana, 0734124191 na ameshapokea jumla ya malalamiko 3,000 yanayohusiana na huduma za afya nchini, kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Ni katika kipindi hicho alichotoa namba, aliitisha kikao na viongozi wakuu katika wizara yake na eneo mojawapo alilowekea msisitizo ni matumizi sahihi ya bajeti ambazo wakuu wa vituo vya afya wamepewa kufanikisha majukumu yao ya kuhudumia umma.

Aidha, ni kipindi ambacho Mfamasia Mkuu wa Serikali, alihimiza Desemba 31 mwaka jana, wenye maduka ya dawa ambao hawajasajiliwa kuchukua hatua, ikiwa sehemu ya juhudi kusaka ufanisi wa huduma bora ya kazi ya kuhudumia mhitaji wa dawa, ambaye ni mgonjwa.

Habari Kubwa