Mgosi Kwaheri, umeacha rekodi yako baba

14Aug 2016
Adam Fungamwango
Lete Raha
Mgosi Kwaheri, umeacha rekodi yako baba

MAISHA yanakwenda kasi sana. Mussa Hassan Mgosi, straika hatari kwenye kizazi hiki cha karne ya 21 amestaafu rasmi soka.

Amestaafu akiwa amefunga bao moja tu msimu uliomalizika wa 2015/16 kwenye mechi ya mwisho kabisa, Simba ikifungwa mabao 2-1 dhidi ya JKT Ruvu.

Hilo ndilo lilikuwa goli lake lake la mwisho kabisa kulifunga mkongwe huyo kwenye Ligi Kuu.

Pamoja na kwamba ametumikia klabu mbalimbali, lakini maisha yake marefu ya soka la ushindani ameyatumikia akiwa kwenye klabu yake ya Simba.

Na ametangaza kustaafu akiwa kwenye klabu hiyo, baada ya kuhangaika huku na huko kutafuta malisho.

Klabu ya Simba ina haki ya kumuaga mkongwe huyo kwa heshima zote kutokana na mchango mkubwa alioutoa kwa klabu hiyo kwa kipindi kisichozidi miaka 10.

Rekodi ya kuifunga Yanga

Mgosi anaweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyefunga magoli mengi kwenye mechi za watani za Ligi Kuu tangu kuingia karne ya 21 mpaka sasa kwenye klabu ya Simba.

Ikumbukwe kuwa karne ya 21 ilianzia mwaka 2000.

Amefunga magoli manne yanayomfanya mchezaji pekee wa klabu hiyo kuifunga Yanga magoli mengi, huku upande wa Yanga nao ukiwa na Jerry Tegete aliyefunga idadi kama hiyo ya magoli.

Kwa sasa hayupo na timu hiyo.

Magoli ya Mgosi yalianza mwaka 2009 alipofunga goli pekee kwenye dakika ya 26, Simba ikishinda bao 1-0, Oktoba 31.
Alifunga magoli mawili 2010, Simba ikiifunga Yanga mabao 4-3 mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa Aprili 18 Ligi Kuu msimu wa 2009/10.

Msimu wa 2010/11 alifunga tena goli kwenye mechi ya watani wa jadi iliyochezwa Machi 2, 2011 timu hizo zilipotoka sare ya bao 1-1.

Mzee wa bao la video Simba, Yanga

Katika historia ya mechi za Simba na Yanga tangu zilipoanzishwa, hakuna mchezaji aliyewahi kufunga bao la ajabu kama alilofunga straika huyo.

Ni bao la kiteknolojia.

Ilikuwa Machi 2, 2011, msimu wa Ligi Kuu 2010/11 alipofunga goli lililoamuliwa kwa maamuzi ya teknolojia.
Bao hilo alilifunga dakika ya 73 likiwa ni la kusawazisha lile la Stefano Mwasyika alilolifunga kwa mkwaju wa penalti dakika ya 59.

Ni bao lililoingia kwenye rekodi ya kukubaliwa kutokana na mwamuzi Orden Mbaga kuangalia marudio ya televisheni kubwa iliyokuwa uwanjani. Awali alikuwa amelikataa.

Kutwaa kiatu cha dhahabu

Ni mmoja wa wachezaji walioweka rekodi ya kutwaa kiatu cha dhahabu kwenye historia ya soka nchini.
Aliibuka kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2009/10 kwa kufunga mabao 18, akiisaidia Simba kutwaa ubingwa msimu huo bila kufungwa mechi yoyote ile.

Mchezaji pekee tangu 2005

Tangu mwaka 2005 alipojiunga na klabu hiyo kwa mara ya kwanza akitokea Mtibwa Sugar, ndiye mchezaji pekee aliyebakia kwa sasa.

Wengine walihama na kuendelea na soka, baadhi wameshataafu akiwemo Nico Nyagawa ambaye alijiunga naye wakitokea Mtibwa.

Nadhani hilo ndilo lililosababisha benchi la ufundi la timu hiyo kumpa unahodha kwa sababu ndiye anayepokea wachezaji wote wanaosajiliwa kwenye klabu hiyo, wakitokea klabu mbalimbali, ikiwemo klabu yake ya zamani Mtibwa.

Soka la kulipwa

Mwaka 2011, alikwenda kucheza soka la kulipwa nchini DR Congo kwenye klabu ya DC Motema Pembe.

Alirejea na kujiunga na JKT Ruvu msimu uliofuata, kabla ya kurejea kwenye klabu yake ya zamani Mtibwa.

Septemba 20, 2014 kwenye mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu kati ya Mtibwa dhidi ya Yanga, alifunga bao na kuibeba timu yake kushinda mabao 2-0 kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Novemba Mosi, 2014 kwenye uwanja huo huo aliiokoa Mtibwa isizame mbele ya Simba alipofunga bao dakika ya 59 na kuzifanya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.

Aprili 11 kwenye uwanja wa Manungu alipachika bao kwenye dakika ya 20 akiisaidia Mtibwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam FC.

Kurejea tena Msimbazi

Kwa mujibu wa viongozi wa Simba ni kwamba, alirejeshwa kutokana na timu yao kuwa na wachezaji wengi vijana ambao bado hajakomaa na wanahitaji uzoefu.

Hivyo alirejeshwa msimu uliopita ingawa hakufanya vizuri na kufunga bao moja tu.

Kuna taarifa kuwa huenda baada ya kutangaza kustaafu soka kwenye klabu hiyo kwa heshima zote, anaweza kutangazwa kuwa meneja mpya wa Wekundu hao wa Msimbazi.

Habari Kubwa