Mhadhiri awafungua macho namna kutojua soko kunawaachia ‘majanga’

31Jul 2020
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Mhadhiri awafungua macho namna kutojua soko kunawaachia ‘majanga’
  • • Wakiri ‘zadoda’ ugenini na nchini
  • • Waonyeshwa njia tatu za kufanikiwa

KATIKA shughuli za biashara kuna mbinu mbalimbali wafanyabiashara wanazitumia kufikia malengo yao.

Mkufunzi Mariam Tambwe (kushoto), akiendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake wanaofanya biashara nje ya mipaka ya nchi. PICHA: SABATO KASIKA

Lakini, baadhi ya wanaojishughulisha na biashara kuvuka wanafanya shughuli hizo kwa mazoea, hali inayochangia kukwama.

Ni mambo yanayojiri kutoka kwa jumla ya wanawake 40 wa mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Mara na Kigoma, waliofundishwa mbinu muhimu za kuwawezesha kufanikiwa katika biashara zao.

Mafunzo hayo ya siku tano kwa wanawake wanaofanya biashara nje ya mipaka ya Tanzania, yaliandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), chini ya Mkufunzi Mariam Tambwe,

Mkufunzi huyo, ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), anaainisha biashara kuwa na mbinu nyingi, lakini hizo tatu ndizo muhimu kwa ajili kufikia malengo stahiki.

Anataja muhimu kwa mfanyabiashara ni kuwa na chapa; kufanya utafiti wa soko kabla ya kuanza biashara; na umuhimu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kwa kuwa dunia sasa imekuwa kijiji.

WAFANYABIASHARA

Upendo Nkwira, kutoka Manyovu Kigoma, ni mama anayefanya biashara ya kuingia nchini Burundi kwa miaka miwili sasa, ananunua na kuuza matunda katika nchi jirani ya Burundi.

Pia, anaeleza ‘majanga yake’ ya anaponunua na kuuza katika nchi hiyo, lakini bado mambo hayajamuendea vizuri, akifafanua:"Biashara zangu zimekuwa zikiniozea na kupata hasara kwa kukosa wateja. Kwa mfano, ninaweza kununua machungwa ya shilingi laki mbili na kupata nusu ya pesa niliyonunua, kwa sababu wateja ni wachache kule."

Upendo anasema alianza kukata tamaa, lakini sasa anaendelea kujipanga upya, baada ya kupigwa msasa wa siku tano wa jinsi ya kufanya biashara ya kupata faida badala ya hasara.

Mwemzake Mariam Makoko, kutoka Tanga, anasema biashara ndani ya mipaka ya Tanzania ina matatizo yanayochangia kukwamisha hatua za maendeleo ya wanajamii.

UTAFITI

Kama ilivyo kwa hoja ya Rais mjenzi wa taifa kubwa kibiashara duniani China, Mao Tse Tung, pasipo utafiti ‘hakuna haki ya kunena jambo’naye mhadhiri huyo ana hoja kama hiyo kutoka katika nadharia ya masoko.

Anasema, ni muhimu kwa mtu anapotaka kufanya biashara, la kwanza kwake liangukie utafiti wa masoko, ili kubaini aina ya biashara anapaswa kuifanya na idadi ya wateja walioko kama wanakidhi matakwa yake, kabla hajajitosa tu.

"Watu wengi wanafanya biashara kienyeji. Anaamka na kuanza kukaanga vitumbua bila ya kujua labda wateja wanataka mihogo, matokeo yake vitumbua vinakosa soko," anasema Mariam.

Pia, anafafanua kuna wakati mtu anaweza kujibebesha dhana ya uchawi kwenye biashara, kumbe inaangukia mtazamo wa kisayansi na ukweli wa mambo, ikianzia mwenyewe hakufanya utafiti wa soko, kabla ya kuamua kufanya aina ya biashara isiyo na wateja.

"Kwenu mnaofanya biashara nje ya mipaka ya Tanzania, mnatakiwa kuwa makini sana, kwani unaweza kubeba mzigo mkubwa kwenda Kenya na kujikuta hunakosa soko, huku umetumia gharama kubwa," anasema.

Mariam anahimiza suala la utafiti ni muhimu zaidi kwa kwa kila mfanyabiashara, ili kujua ni bidhaa au vitu gani vinavyohitajika sokoni.

CHAPA BIASHARA

Mariam anaeleza kwa mfano, iwapo mtu anauza viatu, ni lazima awe na chapa yake itakayomtambulisha na umarufu wake, ili aweze kupata wateja wengi zaidi.

"Hata ukiwa na biashara ya kawaida tu, chapa yako inaweza kukufanya ukawa maarufu kwa watu na siyo vibaya ukajiita mama viatu ili ujulikane kwa jina hilo na hiyo inakuwa ni chapa yako ya biashara," anasema.

Anarejea mfano wake wa kuwapo watu wengi wanaouza viatu, nguo na vingine, na ili kujitofautisha nao sokoni, ni muhimu ubunifu utumike kumpa muizaji wateja wengi katika biashara.

KWANINI TEHEMA?

Anasema, ukuaji wa tekonolojia habari na mawasiliano umewezesha mengi, ikiwamo urahisishaji wa ununuzi kupitia mtandao mbalimbali kama ya simu za mkononi.

"Unaweza kuona bidhaa kabla ya kuinunua, hivyo tumieni Tehama kutangaza biashara zenu na siyo kuuza sura kama ambavyo baadhi ya wanawake wamekuwa wakifanya," anasema.

Aidha anasema, kupitia teknolojia ya mawasiliano wanaweza kupata elimu ya biashara kwa kujifunza mengi yahusuyo biashara kupitia tovuti, blogi na mitandao ya kijamii kama ‘facebook.’

"Katika teknolojia ya mawasiliano, kuna utoaji wa huduma bora kwa wateja, kuwapo kwa uhusiano wa karibu kati ya mzalishaji na mfanyabiashara, msambazaji na mteja," anasema.

OFISA TGNP

Ofisa Programu Msaidizi wa TGNP, Jackson Malangalila, anasema katika karne iliyoko, Tehama haikwepeki, hivyo kinachotakiwa ni kila mwanamke kwenda na wakati.

"Kwa majibu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini, asilimia 25 ya Watanzania, wanatumia mitandao ya kijamii kama jukwaa la kuwaunganisha katika shughuli zao mbalimbali, " anasema Malangalila.

Anafafanua kuwa mitandao ya kijamii pia inatumiwa na wafanyabiashara kubadilishana mawazo, uzoefu na mengine muhimu kwa ajili ya maendeleo ya shughuli zao za kila siku.

"Sisi TGNP, tupo tayari kuwafundisha wafanyabiashara jinsi ya kufungua barua pepe na namna ya kutumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya biashara, ili waweze kuwasiliana na wengine wa ndani na nje ya nchi," anasema.

Habari Kubwa