Mhaidrolojia: Maji ya visima Moro machafu

07Dec 2017
Christina Haule
Nipashe
Mhaidrolojia: Maji ya visima Moro machafu
  • Hekaheka kipindupindu yaibua uozo
  • Mkoa mzima una visima halali 60 tu

INAELEWEKA rasmi kuwapo mahitaji makubwa ya maji kwa ajili ya matumizi ya kijamii na yasiyo ya kijamii.

Hivyo, huduma zitolewazo na mamlaka rasmi za kuitoa huduma za maji, hazikidhi kiwago cha mahitaji, huku kukiwapo maeneo mengine mengi yenye kasoro rasmi ya huduma hizo.

 

Kuwapo kwa hali hiyo kunawasukuma wakazi wa baadhi ya maeneo kutafuta mbinu mbadala za kupata huduma hiyo.

 

Hiyo ni moja ya sababu hivi sasa katika miji mingi, ikiwamo Dar es Salaam, kumejaa wafanyabiashara wakubwa na wadogo wanaouza huduma ya maji.

Ikirejewa uhalali wao, Sheria ya Mwongozo wa Watumiaji Maji Kifungu cha 11 na vifungu vinginevyo ya mwaka 2009, inaruhusu utumiaji maji majumbani, kwa masharti yachimbwa kwa kina cha walau mita 15.

Grace Chitanda, ni Mhaidrolojia kutoka Ofisi Kuu ya Maji Bonde la Wami Ruvu mkoani Morogoro, anayesema visima vingi huwa havichimbwi kufikia kina kilichotajwa cha mita 15, kuwapo uchafu, jambo linalovunja sheria rasmi iliyoundwa.

Anasema, kisheria mtu anayetaka kuchimba kisima ni lazima awasiliane na wataalamu wa visima kutoka ofisi kama yake zilizoko katika kila mkoa, ili kupata maelekezo na kibali cha kuchimba kisima kinachotoa huduma, huku kikilinda afya za watumiaji maji husika, lakini imegundulika wenye nia wengi hawafuati sheria.

Grace anasema matumizi ya maji kutoka visima visivyofuata sheria husika, mara nyingi yanasababisha magonjwa ya ngozi, ikiwemo vipele, muwasho na magonjwa ya tumbo ikiwemo kipindupindu na hata vifo.

Mlipuko Moro

Anasema mwaka 2016, mkoa Morogoro ulipata mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu na Ofisi ya Bonde la Ruvu mkoani lilichukua sampuli 200 za maji kutoka maeneo mbalimbali, ambako ugonjwa ulizuka na kugundua kasoro nyingi za tahadhari ya kiafya.

Mhaidrolojia huyo, anatoa mfano wa wilaya za Kilosa na Morogoro, sampuli zake zilibainisha kwamba visima vingi vilichimbwa jirani na vyoo, hivyo walichukua hatua ya kuwashauri wakazi kuchemsha maji kabla ya kunywa.

Anasema, pia hatua ilichukuliwa ya kuvifunga visima vitano vilivyokuwepo katika Kata ya Mwembesongo, Manispaa ya Morogoro, sambamba na kuwa makini na visima vipya kufuata masharti yaliyowekwa kisheria.

Grace anasema mkoani Morogoro mpaka sasa, hawazidi watu 60 wenye visima viliovyofuata taratibu na kwamba Ofisi ya Maji Bonde la Wami Ruvu tayari umeshatembelea wananchi kwa mara ya kwanza, ili kuwakagua.

 

Anaongeza kuhusu kuwapo mpango wa kutembelea tena katika utaratibu wa ‘nyumba hadi nyumba’ ili kukagua ufuataji wa sheria zilizopo katika visima vyao.

 “Tutatembelea tena kuona, kwasababu huwezi kukuta kisima kimechimbwa nyumba hii na inayofuata na inayofuata. Licha ya sheria kutoruhusu, ni wazi kuwa wengine watakosa maji,” anasema Grace.

Ofisi ya Afya

Ofisa Afya Manispaa ya Morogoro, George Mkimbo, anawataka watumiaji wa maji ya visima, kufuata kanuni na sheria zilizopo, ili kulinda afya zao na kuepusha magonjwa kwa watoto.

 Mkimbo anasema matumizi ya maji yasiyokuwa safi na salama, kitaalamu husababisha magonjwa ya milipuko na vifo, huku wengine wakilazwa, jambo ambalo si salama kwa afya ya umma na kitaifa kwa jumla.

 

Sheria, kanuni na adhabu za watumiaji maji ya visima bila ya kufuata taratibu au kwa wanaotengeneza za taarifa ya uongo ili kupata kibali cha kuchimba kisima adhabu yake inafikia kifungo cha kati ya mwaka mmoja na miwili, au faini isiyozidi Sh.milioni tano.

Ni taratibu ambazo usimamizi na ufuatiliaji wake huko chini ya

Ofisi ya Taasisi ya Uhakika wa Maji, kupitia Mradi wa Shahidi wa Maji, uliofadhiliwa na asasi ya DFID

Sheria inaelekeza kwamba watumiaji wa maji ya visima zaidi ya mahitaji ya nyumbani, ikiwemo umwagiliaji bustani za mboga za biashara, miti ya matunda na shughuli nyingine nyingi, watatozwa faini isiyozidi Shilingi 300,000 hadi Sh. 500, 000,000 ya kutumikia kifungo jela cha kati ya miezi 2 na 6.

 

Waliosaidiwa watabasamu   

Yalikuwa mazingira ya kicheko na tabasamu yaliyoyotawala kwa wakazi wa Kata ya Mwembesongo, Manispaa ya Morogoro walipoeleza namna wanavyotumiaji maji ya visima,

Wanatoa pongezi kwa Ofisi ya Maji Bonde la Wami Ruvu, kwa kuwapatia dawa za kuua vijidudu katika maji hayo na kuwafanya waendelea kuyatumia katika hali ya Usafi na salama.

Mzee Machika Makweta, anayemiliki kisima cha maji, anakiri Ofisi ya Maji Bonde la Wami Ruvu, imefanya operesheni iliyofunga baadhi ya visima vilichimbwa kiholela mitaani na ambavyo vilikiuka sheria, huku badajhi havikuwa na hata mifuniko ya kuiweka salama.

 

Anasema ufuatiliaji huo unawapa moyo wamiliki wa visima kuvihifadhi na kutoa huduma hiyo kwa wengine, mbali na kwake binafsi yanavyomsaidia.

 “Yaani hapa ukifika asubuhi, watu wengi wanapanga foleni kabisa ya ndoo zao, kwa ajili ya kuchota maji, nami napata pesa japo kidogo” anaeleza mzee huyo.

Meya Morogoro

Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascar Kihanga, neno lake kuu ni kuwataka wachimba visima kuzingatia sheria na kanuni walizowekewa kwa ajili ya usalama wao.

Kihanga kwa upande wa pili wa shilingi, anawatetea na kuwapongeza wachimba visima, akisema ‘sio dhambi’ kutokana na uhaba wa maji uliopo, kwani bwawa tegemezi la Mindu sasa linashindwa kukidhi mahitaji ya waka wake.

Pamoja na kuwapongeza, naye anaungana na sharti la kuzingatia sheria, akisisitiza kwamba itakapovunjwa, msimamo uliopo ni kwamba sheria zilizopo za Manispaa ziotachukua mkondo wake.

Meya Kihanga anaainisha bila ya kutaja takwimu, akisema Bwawa la Mindu linalohudumia maji Morogoro, lilijengwa katika miaka ya 1980 kulingana na takwimu ya wakazi wa wakati huo.

Anasema, sasa ikiwa ni wastani wa zaidi ya miongo mitatu, kuna ziada ya wakazi 8500, kwa mujibu wa Sensa ya Watu ya na Makazi ya Mwaka 2012, ikimaanisha maji yaliyopo hayakidhi mahitaji ya wakazi waliopo.

 

Habari Kubwa