Mhandisi Kakoko: Miradi ya JPM imetupaisha Bandari

10Jan 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Mhandisi Kakoko: Miradi ya JPM imetupaisha Bandari
  • Asema, kila alichokibuni kimekuwa ‘dili’ kwao TPA

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, ana simulizi ya mambo makubwa ambayo mamlaka hiyo inajivunia kufanyika ndani ya miaka minne ya awamu iliyopo ya serikali.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko. PICHA MTANDAO

Kakoko, anataja kwanza wanajivunia kukua kwa uwezo wa bandari zilizopo bahari kuu na maziwa makuu yote nchini na maboresho makubwa yaliyofanyika katika bandari zote nchini.

Pia anataja lingine ni maboresho makubwa ya mifumo ya utendaji kazi ambayo imechangia kuongeza idadi ya shehena zinazohudumiwa bandarini na ongezeko la mapato tofauti na miaka ya nyuma.

“Katika miaka minne ya kipindi cha serikali ya awamu ya tano mambo mengi yamefanyika TPA, ambayo tuna haki ya kujivunia, na katika kupima uwezo wa bandari ni pamoja na kuangalia tani za shehena ambazo tunazihudumia ukilinganisha na kipindi kilichopita.

“Kipindi cha nyuma, kuna hata baadhi ya watu walikuwa wanatudhihaki kwamba bandari haina mizigo, ni nyeupe na baadhi wakitamani hata kupiga picha, lakini kwa sasa wenyewe wanashuhudia mambo makubwa yanayofanyika bandarini, shehena zimeongezeka kwa kiwango kikubwa sana, hawana la kusema tena, kazi zinafanyika kwa uwazi na ubora.

"Mafanikio yaliyopo TPA kwa sasa ni sawa na mtu ambaye alilima shamba na kutarajia kuvuna, hayajaja kwa bahati mbaya, ni mipango madhubiti ambayo tumejiwekea ndiyo imesaidia kufanikisha yote haya."

Kakoko anasema, sasa, tayari imeimarisha pia ushirikiano na taasisi nyingine kufufua miundombinu yote ambayo kwa namna moja ama nyingine ina uhusiano wa kufanikisha shughuli za biashara za bandari ikiwamo kufufua meli kwa ajili ya kutumika kubebea shehena na mizigo.

“TPA imekuwa ikishirikiana na taasisi nyingine ili kufufua meli na miundombinu ya bandari nchini na kazi hii imekuwa ikifanyika kwa mafanikio makubwa. Kwetu sisi tukiona kuna meli nyingi tunapata usingizi, lakini meli zikikosekana hata usingizi hauji kabisa,” anasema Kakoko.

"Na ushirikiano huu umeanza kuzaa matunda, meli kwa sasa ni nyingi katika bandari zetu za Tanga, Mtwara nyinginezo na zina uwezo mkubwa, kwa hiyo tukiona mafanikio ya namna hiyo ndiyo na sisi tunapata usingizi, kadhalika zikipungua hata kulala na ukapata usingizi inakuwa shida.”

KULIVYOKUWA

Kakoko anasimulia wakati wanaanza kazi katika kipindi cha kwanza na bodi mpya mwaka 2016, meli zilikuwa chache sana na hali hiyo ilianza mwaka 2014/2015 na kwamba ndicho kipindi mzigo wa shehena ulipungua.

Kakoko anasema, ili kutoka katika hali hiyo, TPA ililazimika kujitoa na kuhakikisha inaweka mipango madhubuti ya kuondokana na changamoto hiyo.

Anasema mwanzoni walianza kwa kuhudumia tani milioni 14.7 kwa mwaka, lakini walipoanza kuimarisha zaidi huduma bandarini wakafanikiwa kufikia tani milioni 18.1 hali ambayo iliwapa nguvu ya kuendelea kujiimarisha katika mifumo ya utoaji huduma.

Anataja jitihada hizo zilianza kuzaa matunda na hivyo kufikia hatua ambayo waliiona kwamba ndiyo inafaa kwenda nayo.

Kakoko anasema walihakikisha wanaendeleza mapambano hayo mpaka sasa ambapo wanaona wana haki ya kujivunia na kile kinachofanyika japokuwa wanaendelea kujiimarisha.

Kakoko anasema mbali na kuongezeka kwa shehena ambazo zimetokana na jitihada hizo, pia kumekuwa na ongezeko la ukusanyaji wa mapato ambayo yamepanda ikilinganisha na huko nyuma na kwamba kwa upande wa shehena walikuwa na ongezeko la asilimia 6 hadi 7 kipindi cha kwanza na sasa wamefikia asilimia tisa hadi 11 kwa mwaka.

“Katika upande wa makusanyo ya fedha nako wakati tunaingia tulikuta wanakusanya Sh. bilioni 300 hadi 320, ikabidi tujiwekee malengo ambayo tulifanikiwa kukusanya Sh. bilioni 608 , na mpaka sasa tunavyozungumza tumepanda hadi kufikia Sh. bilioni 940 na mkakati wetu ni kufikia Sh. trilioni 1.40 kila mwaka.”

Pia anasema mafanikio hayo ni zao la mikakati mipya na imara waliojiwekea, ikiwamo kuongeza shehena na utoaji huduma kwa wateja wao.

Anaeleza mafanikio hayo yanatokana na mfumo wa upimaji wa utendaji kazi na ukusanyaji wa mapato kwa kila bandari na kwa kila mfanyakazi katika kila eneo.

Kwa mujibu wa Kakoko, TPA wanajivunia kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya tano ni kuwa na uwezo wa kutoa gawio kwa serikali.

“Kwa hiyo mapato ya fedha ambayo yanapatikana sasa TPA yanawiana kabisa na shehena tunayoihudumia, tunataka kujihakikishia kuendelea kuhudumia shehena nyingi zaidi siku hadi siku.

“Tunamshukuru sana Rais Magufuli kwa kufufua viwanda kwa sababu hivyo kwetu kama bandari ni faida,” anasema Kakoko na kuongeza:

“Miradi inayoendelea nchini kwetu inatuinua sana sisi kama TPA, kwa mfano mradi wa reli kuna vyuma ambavyo vinaingia nchini, pamoja na mitambo mingine ambavyo vinapoletwa kwa kupitia kwenye bandari zetu, tunapata fedha.

“Hata mradi wa umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere nako tutapata fedha kwa sababu malighafi za ujenzi zitapita kwenye bandari yetu.”

Pia anasema muda wa upakuaji na upakiaji wa shehena kwa sasa unatumika kwa usahihi na hivyo kuruhusu au kutoa mwanya wa kuhudumia mizigo mingi bandarini.

"Muda gani meli inakaa kwenye gati. Tangu unapofungua kamba ya kwanza hadi unapoifunga na kuanza kuondoka. Tunajitahidi kuhakikisha tunaanza kuhesabu muda tangu ilipofungwa kamba ya kwanza maana ile ni huduma, ukichelewa kufunga kamba ni kupoteza muda,” anasema Kakoko.

“Pia muda unaotumika kupakia na kushusha shehena nao unahesabiwa na inatakiwa muda uwe mdogo hata kama mzigo ni mkubwa kwa sababu hiyo nayo inasaidia kupima uwezo wako wa kutoa huduma, eneo ambalo tumefanikiwa kwa sasa,” anasema Kakoko.

Kwa mujibu wa Kakoko, wamefanikiwa katika kipindi ambacho kuna amani kwa nchi, pamoja na uhusiano mzuri kati yao na wadau wa bandari.

“Amani iliyopo nchini na uhusiano mwema kwa jamii kupitia biashara hurudisha wateja, kwa sababu hakuna mteja anayekubali kuleta vitu vyake mahali penye kelele au katika eneo ambalo muda wowote kuna uwezekano wa kutokea vita na mzigo ukapotea,” anasema Kakoko.

Habari Kubwa