Miaka 10 ya Mkapa Foundation kuimarisha afya maeneo ya kazi

21Apr 2016
Dar es Salaam
Nipashe
Miaka 10 ya Mkapa Foundation kuimarisha afya maeneo ya kazi

Tanzania inakabiliwa na uhaba mkubwa wa watumishi wa afya kwa asilimia 56. Taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa, kutokana na mkakati wa kitaifa uliopangwa mwaka 2014, Tanzania ina asilimia 44 tu ya idadi ya wafanyakazi katika sekta ya afya, kwenye mikoa yote nchini.

Remmy Moshi, ambaye ni Mratibu wa Programu wa taasisi ya Mkapa (Benjamin Mkapa Foundation-BMF), Kanda ya Ziwa, anasema ili kupambana na upungufu huo, taasisi ya BMF imekuwa ikiweka jitihada za kuisaidia serikali, kuboresha huduma za afya na kuhusisha afya za wafanyakazi maeneo ya kazi.

Moshi anasisitiza kuwa, kutokana na jitihada hizo, taasisi ilianzisha mikakati ya kupambana na uhaba wa watumishi wa afya, kwa kuajiri watumishi, pamoja na kuwasomesha wanafunzi wapya kwenye vyuo mbalimbali nchini ili kusaidia kupunguza pengo la uhaba uliopo kwenye sekta hiyo.

Anasema kuwa, kwa zaidi ya miaka 10 sasa, Taasisi ya Mkapa imeanzisha miradi mingi ya ushirikiano na ushauri wa karibu na Serikali kupitia Wizara ya Afya, pamoja na taasisi zingine zinazohusiana na afya ya wafanyakazi.

Moshi anafafanua kuwa, miradi hiyo imekuwa ikilenga kuimarisha na kupambana na uhaba wa watumishi wa sekta ya afya, ambayo ni pamoja na ule wa dharura wa kukodisha watumishi wa afya (EHP) kuimarisha mifumo ya afya (HSS) na wa kuimarisha utendaji wa maabara.

Anasema kutokana na miradi iliyotajwa, jumla ya vituo vya afya 1,118, vilianzishwa na watumishi wengi walisomeshwa na kupelekwa kwenye vituo mbalimbali nchini, zikiwamo hospitali za mikoa na taasisi nyingine za afya,.

Moshi anasema kuna watumishi waliobahatika, kwa kupewa mikataba ya ajira ya kuanzia mwaka mmoja hadi miaka mitatu (wakitofautiana kutokana na mradi kwa mradi).

Anasema kuna kundi la watumishi 805 ama asilimia 72 miongoni mwao, walijumuishwa kwenye utumishi wa umma.

Kwa mujibu wa Moshi, watumishi wengine wa afya waliobakia, wakiwamo walimu walianza kulipwa mishahara na serikali kwenye mwaka wa Fedha wa 2015/16 na wengine wataanza kulipwa katika mwaka wa fedha wa 2016/17.

“Haya ni mafanikio makubwa yaliyofikiwa na BMF, kuhakikisha inaendelea kutekeleza majukumu yake,” anasema.

Aidha Moshi anasema, katika kuhakikisha kuwa huduma za afya sasa zinatolewa katika ubora wake na wataalamu wa afya wenye ujuzi, taasisi ya Mkapa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ziliboresha uzalishaji wa nguvukazi kwa sekta ya afya kutoka kwenye taasisi za mafunzo nchini.

“Na hili lilifanyika pamoja na mambo mengine katika kuhakikisha inaajiri watumishi wa afya kufanya kazi kwenye maeneo yenye uhitaji,” anasema.

Anasema hilo, lilifanyika kwa kukodisha wakufunzi 212 waliotumwa kufanya kazi kwenye taasisi 43 za mafunzo ya afya, likilenga kukabili upungufu wa wakufunzi, na hivyo kuboresha ubora wa mafunzo.

Moshi anasema, miongoni mwao, wakufunzi 100 waliingizwa kwenye mfumo wa ajira wa serikali na wengine 62 walitarajiwa kuingizwa mwaka wa fedha wa 2015/16.

“Kutokana na kuwapo kwa wakufunzi hawa, tumeweza kubaini ongezeko la idadi ya wanafunzi, kupungua kwa mzigo wa kazi, kuongezeka kwa kasi ya utoaji vibali NACTE na ubora wa mafunzo kwenye taasisi za mafunzo ya afya,” anasema.

Anafafanua kwamba, kutokea mwaka 2012 na kuendelea, taasisi ya Mkapa kwa ushirikiano wa karibu na Wizara ya Afya na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), ilisaidia kuchagua na kugharimia masomo ya wanafunzi 1,000 kwenye kozi mbalimbali za afya kama vile uuguzi, wasaidizi wa maabara na wasaidizi wafamasia.

Anasema, kati ya wanafunzi 72 waliofadhiliwa, 61 walimaliza masomo mwaka 2014 na kupelekwa kufanya kazi wilayani.

Moshi anasema kuwa, msukumo wa kuzalisha kada hizo za afya katika ngazi mbalimbali za kati, unalenga kuziba ombwe kubwa la watumishi wa afya kwenye ngazi za msingi za afya, ambako wahitimu wanaplekwa na kufanya kazi na mamlaka za serikali za mitaa.

Anasema, hadi kufikia Julai 2016, wanafunzi wote 807 waliobakia watakuwa wamehitimu na kupelekwa kufanya kazi kwenye vituo vya afya vya vijijini.

“Mpango wote wa nguvu kazi ya afya uliotajwa hapo juu ambao ulitekelezwa na taasisi ya Mkapa Foundation, umewezeshwa kifedha na wafadhili wengi wakiwamo Global Fund, inayopambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria; Irish Aid; Abbott Fund na kampuni nyingi za ndani zinazotoa fedha kwa taasisi, kama vie ACACIA, Bank M, NSSF, Quality Group, AngloGold Ashanti, taasisi ya MO Dewji, PPF na nynginezo nyingi,” anahitimisha Moshi.

Habari Kubwa