Miaka 20 Kumbukizi ya Mwal Nyerere; Nakubali tusijikweze, tunyenyekee

23Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Kahama
Nipashe
Miaka 20 Kumbukizi ya Mwal Nyerere; Nakubali tusijikweze, tunyenyekee

AWALI ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai. Tunaishi na imekuwa hivyo kwa rehema na mapenzi yake.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. PICHA: MTANDAO

Sasa miaka 20 tangu kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Kimsingi alikuwa mtu wa pekee siyo tu kwa taifa letu hata kwa Bara la Afrika.

Mchango wake katika harakati za kuleta usawa unafahamika na kuheshimiwa na wengi waliopata fursa ya kuwa karibu naye.

Hakuwa mbinafsi wala wa kunyenyekea kirahisi kwa mantiki ya kunyenyekea tu, bali alisimama kwenye ukweli na akapigania uhuru wa Mwafrika ipasavyo.

Sasa ni miaka 20 tangu Mwalimu atutoke, yapo mengi aliyoyafanya kwa Tanzania na Bara la Afrika.

Hata hivyo, kupitia fursa mbalimbali ikiwamo makongamano, mikutano ya hadhara, mitandao ya kijamii na kwenye vyombo vya habari; tumekuwa tukikumbushwa Mwalimu alifanya nini kwa Tanzania.

Kikubwa kinachosisitizwa ni amani. Mwalimu alikazania sana utu wetu na amani kwa faida ya watu wote.

Hakuishia hapo pia aliamini kuwa baada ya kupata uhuru Desemba 9, 1961, hatutakuwa na amani kamili iwapo majirani zetu wataendelea kutawaliwa na kukandamizwa na wakoloni.

Hivyo, nguvu nyingi zikaelekezwa kuikomboa Afrika na suala la kunyenyekea halikuwapo.

Tulikuwa tunadai uhuru wa Afrika na alisema tutafanya hivyo kwa nguvu na uwezo wetu wote.

Mungu mwema, haikuchukua muda mrefu Afrika yote ikawa huru na kukomesha ubaguzi wa rangi.

Wakati akipigania uhuru wa Afrika, pia aliendelea kujenga Taifa lenye umoja, nguvu na mshikamano na Aprili 26, 1964 ikaunganishwa “Tanganyika” na Zanzibar ikazaliwa Tanzania.

Yeye akawa kiongozi Mkuu (Rais) wa kwanza wa Tanzania akisaidiana na Rais wa Zanzibar.

Muungano wetu ulilenga zaidi kuimarisha uhuru na ujirani wetu na kuhakikisha uwepo wa amani ya kutosha kwa kuzingatia taifa imara lenye nguvu kijeshi kuimarisha ulinzi na usalama.

Wakati huohuo kukawa na itikadi ya chama kimoja na sera ya kujenga “Ujamaa na Kujitegemea.”

Tukajua kuwa “Ujamaa ni utu na Upebari ni unyama” na siyo hivyo tu hatua zaidi za makusudi zikachukuliwa tukataifisha baadhi ya mali (kama nyumba) ambazo zilipatikana kinyemela.

Katika kufanikisha hivyo, kulikuwa hakuna cha kunyenyekea na kama ilikuwa kujikweza sijui mradi nia ilikuwa kujenga taifa lenye haki na usawa kwa kupunguza nguvu za “wenyenavyo na wasionavyo”.

Yawezekana serikali ya awamu ya tano kwa namna moja au nyingine inajaribu kumuenzi Mwalimu kwa kulifanyia kazi jambo hilo.

Vilevile, jitihada za makusudi zilifanyika tukaanzisha “Vijiji vya Ujamaa” sehemu mbalimbali nchini na 1967 Azimio la Arusha likawekwa kama muhimili wa kuiongoza Tanzania wakati wa utawala wa chama kimoja.

Zoezi la kuanzisha vijiji vya ujamaa (ambavyo sasa vinafahamika kuwa ni vijiji tu baada ya kuweka Sera na Sheria ya Ardhi ya Vijiji 1999); lilifanyika kwa lengo la kuweka Watanzania pamoja ili serikali iweze kuwapatia huduma za kijamii (elimu, afya, maji, kujenga miundombinu na masuala ya ugani) kirahisi kuliko ilivyokuwa watu wametawanyika, kila mtu na lwake kiasi cha kufanya kazi hiyo iwe ngumu sana.

Kwa mtazamo huo nia ya Mwalimu Nyerere ilikuwa nzuri kwa faida ya wote.

Hata hivyo katika kuanzisha vijiji vya ujamaa, hakukuwapo mkazo kwa unyenyekevu wala kujikweza (unajikweza au kunyenyekea kwa nani na kwa jambo lipi).

Tulihitaji watu wawe pamoja kwa faida ya wote. Sasa vijiji vipo na huduma za kijamii zinafanyika ipasavyo kwa sababu vilianzishwa bila malumbano.

Hatukuishia hapo kukateuliwa “Mameneja wa Vijiji” ili kusimamia maendeleo vijijini.

Katika kufanikisha suala hili, kulikuwa hakuna kuulizana maswali. Mtaalamu alipewa barua nenda kijiji fulani wewe sasa ni meneja wa kijiji na ikawa hivyo.

Hakuna hata aliyethubutu kuuliza sasa naenda kufanya kitu gani huko wakati mimi sina utaalamu wowote kuhusu umeneja wa kijiji. Sasa siyo mameneja ni watendaji wa vijiji.

Yapo kadhaa mengine yaliyofanyika lakini kwa nia njema ya kutafuta njia bora ya kuiendeleza Tanzania.

Mfano, kufuta mfumo wa halmashauri kama tulivyokuwa tumerithi kwa wakoloni na kuanzisha mifumo ya “Madaraka Mikoani” pia tukafuta “Vyama vya Ushirika” na kuweka Mamlaka za Mazao (crop authorities).

Nia ilikuwa nzuri lakini wakati wa kutekeleza yote haya, je, kulikuwa na kunyenyekea au tulijikweza?
Hakukuwa na fursa ya kufanya mashauriano na wakulima kuona kama wanaafiki kufuta ushirika na kuingiza mamlaka nyingine.

Ilionekana ni suala jema tutekeleze na ikawa hivyo kama tulijikweza hapo sijui.

Ndiyo miaka 20 bila Mwalimu imepita lakini ni kipindi cha mabadiliko makubwa kwa nchi yetu kiitikadi, kisera na kisheria.

Azimio la Arusha liko wapi? Tunu au miiko ya taifa iko wapi? Tumekumbwa na masuala tofauti na enzi ya Mwalimu: “Utandawazi”; siasa za vyama vingi; ubinafsishaji; teknohama na mitandao ya kijamii vimetukolea; mifumo ya elimu imebadilika sana; maadili ya kitanzania ndiyo hivyo.

Matokeo yake yamekuwa ni kushamiri rushwa na ufisadi, wizi wa mali za umma na kadhalika.

Ubinafsi ukaotesha mizizi na hivyo ujamaa na utu kubakia kwenye makaratasi na nadharia tu.

Harakati zikawa za kila mtu kujijua na heshima ya utu wetu ikawa chini na upendo ukazorota. Unapendwa au kuheshimiwa kwa sababu ya kile ulichonacho siyo kwa utu au binadamu aliyeuumbwa kwa mfano na sura ya Mungu.

Isitoshe tunu/maadili kwa taifa tumevipiga teke sisi wenyewe. Likaanzishwa “Azimio la Zanzibar” sijui lililenga kufanikisha kitu gani kwa taifa na watu wake?

Tunaposema tusijikweze na tunyenyekee, nakubali kwa asilimia zote lakini najiuliza tunajikweza na kunyenyekea kwa nani na kivipi?

Tuangalie tulipo, wakati tunamuenzi Baba wa Taifa kwa mambo mazuri aliyotuachia.

Hata hivyo, tunafanya hivyo tukiwa kwenye hali gani kisiasa, kijamii na kimazingira?

Bahati nzuri Mwalimu alijitathmini, akajitambua mapema, akasema hapana siendelei “nang’atuka”.
Baadhi yetu tulibisha kidogo lakini akasema kwa hili sinyenyekei kwa yeyote yule mimi nimeamua, naachia madaraka: Tukakubali ikawa hivyo.

Tuheshimu mawazo na kukubali hoja za wengine kama hatukubaliani tupingane kihoja: Ni sawa iwe hivyo.

Lakini tuangalie pia tulipotoka mfano, kulitokea kutofautiana kimawazo na kwa mtazamo wa kitaifa kukazuka hoja ya “Tanganyika” na baadhi ya wabunge wakaunda kikundi (G55), je, kulikuwa na kunyenyekeana au kujikweza?

Mara nyingi viongozi wetu huwa wanatuasa kuwa: Suala la Muungano halina mjadala tutaulinda muungano kwa nguvu zote.
Je, kufanya hivyo ni kujikweza au kunyenyekea kunawekwa wapi?

Lazima tukubali kuwa kuna masuala muhimu ya kitaifa (kama hili la Muungano) ambayo ukiachia hisia na matakwa ya kila mtu yatawale, taifa litayumba.

Hata Baba wa Taifa wakati akiwa Rais, pamoja na kuheshimu mawazo ya wengine, alikuwa na msimamo thabiti kwa masuala yaliyohusu maslahi ya wengi, hakuruhusu watu wachache wajikakamue.

Wakati wa Azimio la Arusha walioona halina maslahi kwao walikuwa na uhuru wa kwenda walikotaka: Kulikuwa hakuna cha kunyenyekea bali kusonga mbele kwa faida ya wengi.

Mbali na hilo wakati fulani kulitokea tofauti ya mawazo na mtazamo kuhusu masuala ya wagombea urais.

Nakumbuka Baba wa Taifa aliona yataelekea kuleta mpasuko na mgawanyiko mkubwa kwa taifa letu, hivyo kupelekea kuhatarisha uhuru na amani kwa nchi yetu.

Mwalimu Nyerere alisimama kidete na wala hakuwa na subira bali alikemea kwa nguvu zote bila kunyenyekea.

Wakati fulani alitishia kurudisha kadi yake ya uanachama iwapo hatua stahiki hazichukuliwi.

Nani aliweza kusema rudisha, si tulikubali yaishe hata kama baadhi ya viongozi walikuwa hawakubaliani naye. Kuna wakati wa kunyenyekea na kujikweza, lakini siyo kwa kila jambo, lazima tuangalie mazingira yaliyopo na inakuwa hivyo kwa nia gani au kwa faida ya nani.

Tusipotoshe kwa faida binafsi bali maslahi ya wengi yatawale maamuzi, tunapokuwa viongozi.

Viongozi wanaandaliwa, hawaokotwi sawa, lakini wanaandaliwa kivipi na mazingira yapi?

Enzi za Mwalimu ilikuwa rahisi kuendesha mafunzo ya uongozi, sasa tunatofautiana kisiasa na kiitikadi ndiyo maana chuo husika kinafanya kazi tofauti na lengo lake.

Yawezekana tukarejesha hilo kwa nia ya kuwaandaa viongozi wa kesho ila iwe ni kitaaluma na siyo kisiasa.

Walengwa wakasome kulingana na mitaala itakayokubalika kwa misingi ya utawala bora. Vijana wahitimu na wawe na sifa ya kuongoza na iwapo mtu anateuliwa kuwa kiongozi mfano, Mkuu wa Mkoa au Wilaya iwe ni moja ya sifa zinazotakiwa kuwa nazo.

Serikali ya Awamu ya Tano inajitahidi sana kuwaletea Watanzania maendeleo kupitia uchumi wa viwanda na kupambana na umaskini wa miaka mingi.

Viongozi wake siyo malaika, watakuwapo wachache wa kujikweza au kukosa unyenyekevu; tuangalie hali halisi pia tukosoane kwa lengo la kuboresha isiwe ni kubeza na hali ya kuvumiliana iwepo.

Miaka mitano siyo muda mrefu wa kutekeleza ahadi ambazo wanasiasa huwa wanazitoa ili wapewe ridhaa ya kuongoza nchi.

Sasa mazingira ya kuongoza siyo yale ya enzi za marehemu. Ubinadamu umeyeyuka na hofu ya Mungu ni kitendawili. Zaidi tunajali fedha kuliko utu wala kumtii Mungu.

Njiani tunapishana kama sisi siyo binadamu na baadhi wanaona jinsia moja kufunga ndoa ni jambo jema eti kwa “Misingi ya Haki za Binadamu.”

Hapo kunyenyekea mbele za Mungu kupo au ndiyo kujikweza? Hali ya utii kwa sasa ni tofauti na ilivyokuwa enzi za Baba wa Taifa.

Tunataka watoto wetu shuleni walelewe na kufundishwa wanavyotaka wenyewe au kama baadhi ya wazazi wanavyopenda.

Mtoto siyo tena thamani ya jamii isitoshe hata wazazi hawana imani na baadhi ya ndugu zao wa karibu kwa kuogopa watoto kufanyiwa ukatili wa makusudi kwa maslahi binafsi.

Watoto wa kike kuwa wajawazito wakiwa shuleni ni sahihi? Mwanafunzi kuwa na simu shuleni inaonekana ni bora kuliko kunyenyekea kwa walimu wao.
Maeneo kama Dar es Salaam utasikia eti wazee hawatakiwi kuwa mijini, tunaambiwa makazi yao ni Chalinze au Msata.

Je, kunyenyekea kuko wapi au ni kujikweza? Baba wa Taifa alikuwa akikemea sana udini na ukabila kwa nguvu zote, je, kiongozi akichachamaa na kukemea udini na ukabila atakuwa anajikweza?

Ndiyo maana inafika mahali viongozi wetu wanakabiliana na hali ngumu ya kukosa utii, kutowajibika na fikra za kupata fedha kirahisi bila kufanya kazi kwa bidii.

Mazingira kama hayo yanapelekea kutokuwapo kunyenyekea maana kiongozi atafanya linalowezekana ili maendeleo kwa wengi yapatikane.

Wakoloni walibeba nguvukazi na rasilimali nyingi toka Afrika. Walifanya hivyo ili wasonge mbele ipasavyo leo “tukakopi” na “kupesti” kutoka kwao bila kujiuliza walifanyaje hadi kufikia hapo walipo?

Historia inaonyesha mataifa yaliyoendelea miaka 150 mpaka 200 iliyopita watu wake waliumia na wengine kupoteza maisha katika harakati za kujiletea maendeleo waliyonayo sasa.

Waliojikweza walifanya hivyo bila kunyenyekea lakini baada ya kupata maendeleo unyenyekevu, demokrasia na utandawazi vikafuata.

Hali kama hiyo hata sisi hatutaikwepa iwapo tunahitaji maendeleo ya kweli, maana baadhi yetu tutaumia lakini tujipe moyo wajukuu na vitukuu wetu watafaidi matunda ya jasho letu.

Tumwombe Mwenyezi Mungu atuzidishie hekima na busara ikiwezekana tunu na miiko ya taifa virejeshwe kwa faida ya wote na amani yetu idumu.

Huu ni wakati wa kushikamana kikamilifu na kusonga mbele mpaka kieleweke kuwa Tanzania ni namba moja Afrika.

Mwandishi anapatikana kupitia, P.O. Box 79011, Dar-es-Salaam, Tanzania.
[email protected]; +255756007400; +255714250050;

Habari Kubwa