MIAKA 41 YA KUTUMIKIA JWTZ

16Jul 2017
Flora Wingia
Nipashe Jumapili
MIAKA 41 YA KUTUMIKIA JWTZ
  • Luteni Jenerali Shimbo aukumbuka ‘ukomandoo’ kuiokoa Shelisheli
  • Asimulia miaka mitatu ya ubalozi China

KATIKA kipindi cha dakika 45 kilichorushwa Jumatatu iliyopita Julai 10 kupitia kituo cha ITV, mwongozaji wa kipindi, Sam Mahela alimkaribisha Luteni Jenerali mstaafu Abdulrahman Shimbo.

Luteni Jenerali mstaafu, Abdulrhaman Shimbo.

Baada ya kustaafu utumishi wa jeshi, aliapishwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, kuwa balozi China Juni 11, 2013, ambako alikaa hadi hadi Desemba mwaka jana.

Luteni Jenerali mstaafu Shimbo, kabla ya hapo alikuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Alitumikia jeshi kwa miaka 41, miezi tisa na siku 15.

Ni mazungumzo yaliyogusa mambo mbalimbali, ikiwamo namna alivyoshiriki katika operesheni za kuzima majaribio ya kijeshi, mfano nchini Shelisheli. Ifuatayo ni sehemu ya kwanza ya mfululizo wa makala zitokanazo na mazungumzo hayo, kupitia kipindi hicho cha dakika 45. Sasa endelea….

Swali: Wakati unalitumikia Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), uliwahi kufanya operesheni kule Shelisheli. Naomba uniambie nini unachokumbuka katika operesheni ile? Hali ya operesheni ilikuwaje?

Shimbo: Upo wakati nilikuwa Mkuu wa Kikundi baada ya aliyekuwapo kurejea nyumbani. Wakati ule, hali ilikuwa ni ngumu kidogo.

Kwanza, tulijaribu kuona hali halisi ya mapigano. Na tulipigana usiku mmoja na askari wa kukodiwa walipoona wamezidiwa,

waliteka ndege na wakachukua na watu waliokuwa uwanjani wakawateka na wakati tunakaribia, tulijipanga tuokoe maisha ya abiria waliokuwa kwenye ndege ile.

Kwa hiyo, hatukuwa na njia nyingine bali kuiokoa ile ndege. Wale askari tulikuwa tumewakata makundi mawili, waliowahi kuingia ndani ya ndege waliweza kuruka na ndege kwa kiasi fulani tuliiharibu na wale waliobaki asubuhi tuliwafuatilia, tukawakamata na baadaye walifikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Mahela: Operesheni kama hizi zinapofanyika, mara nyingi mnawasiliana na familia mnapokuwa mbali nao au sheria za jeshi unapojitosa mawasiliano yanakatika takribani kwa miezi kadhaa au hata mwaka na familia haijui wewe unaendeleaje, kwa sababu huenda ni operesheni hatarishi?

Shimbo: Operesheni zote ni hatarishi na sisi tumekula kiapo. Kwa hiyo, ni hali ambayo tumeizoea na tunategemea lolote linaweza kutokea.

Mawasiliano yetu makubwa ni kwa viongozi na tukiwa kule nchi za nje ni viongozi wa juu katika jeshi pamoja na tunawapelekea taarifa zote jinsi mapigano yanavyoendelea. Matatizo yetu yote yanapitia kwa Mkuu wa Majeshi. Ndiye anayetoa maelekezo, nasi tunatekeleza. Operesheni yetu tuliwakamata wale waliosalia na kazi yetu ikaishia pale.

Jaribio la pili kule Shelisheli halikufanikiwa, kwani tuliwahi kuwakata kabla ya kutekeleza jaribio lenyewe na zoezi lilifanikiwa.
Mahela: Wewe ni moja wa viongozi walioitumikia nchi ya Tanzania katika nafasi ya ubalozi nchini China. Lakini tofauti na China, nadhani pia kuna baadhi ya nchi ambazo ulipewa mamlaka ya kuziangalia. Pengine kwa faida ya Watanzania tujuze?

Shimbo: Ndio niliwahi kuwa Balozi China. Niliteuliwa mwezi wa tatu mwishoni mwa mwaka 2013. Nikiwa China, nilikuwa pia naiwakilisha nchi yangu Jamhuri ya Mongolia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Korea ya Kaskazini.

Hizi ndizo zilizokuwa nchi za uwakilishi. Nimekuwa mtumishi kule China hadi mwaka 2016 na nimerejea nchini mwezi Desemba.

Ubalozi wake China

Mahela: Na nafasi yako kama balozi, naona hapo ni nchi zaidi ya tatu au mbili, ulikuwa unawezaje kuangalia huku China, pia unahakikisha kuwa una mamlaka ya kuwakilisha Tanzania pia katika hizo nchi zingine?

Shimbo: Kazi kubwa ya balozi au kiti kile cha ubalozi ni kujenga uhusiano, kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa. Wizara yetu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imesaini ushirikiano ya Afrika Mashariki na ndio wanajenga uhusiano kati ya mataifa haya .

Uhusiano wa China na Tanzania ni mzuri katika kipindi chote tangu mwaka 1964. Na hata wakati narejea, niliacha unaendelea vizuri na nilimkabidhi mwenzangu aliyekwenda kule, jinsi uhusiano ulivyo na yeye pia nina imani kwamba ataiwakilisha vizuri nchi yetu.

Mahela: Natamani kujua ingawa umekuwa Balozi wa Tanzania nchini China, lakini hapo awali umetutajia Korea ya Kaskazini na Vietnam.

Changamoto ikoje?, kwa mfano , Rais anamteua balozi kuiwakilisha Tanzania katika nchi fulani na anakuwa anamuweka kwenye nchi mfano pale China tu. Lakini wewe ulikuwa unaenda hadi Korea Kaskazini. Ulikuwa huwezi kupata changamoto kusimamia nchi hizi zote au ni jambo rahisi kutokana na uzoefu wenu?

Shimbo: Uzuri wa sheria za kibalozi ni kwamba, mimi nikiwa pale Beijing, ni balozi wa nchi ile. Lakini pia China ina balozi hapa nchini Tanzania. Kwa hiyo, kule tuna shughuli tunazifanya na yeye ana shughuli anazifanya. Na kila mtu anafanya shughuli zake.

Na tunakuwa na muda wa kuzitembelea hizi nchi, tunakutana nao, tunaongea nao na kama kuna shughuli tunazotakiwa kuzifanya, kwa mfano, kama kuna miradi maalumu ambayo tukitafiti tunaona inaweza kuleta manufaa kwetu.

Mfano Vietnam, kilimo na viwanda vya kijeshi. Vietnam baada ya vita iliweza kujiendeleza haraka katika viwanda vidogo pamoja na kilimo.

Kilimo kwa mfano cha samaki na mpunga, wamekwenda mbio sana, pia viwanda vidogo vidogo vya kuchakata mazao ya kilimo. Kwa hiyo, hata ufugaji wa samaki ambao wanafuga katika mashamba yale yale ya mpunga.

Na ufugaji wa samaki ambao pia hapa nyumbani unakua sasa hivi, ni moja ya njia nzuri ya kukuza uchumi. Lakini vilevile, kuongeza ulaji kwa wananchi. Kwa hiyo, kuna muda maalum ambao tunapanga kutembelea kule.

Wakati mwingine tunapata ziara za viongozi mawaziri ambao wanakwenda kutembelea kule. Hujaribu kushauri maeneo yale yenye manufaa kwetu sisi. Hata Korea ya Kaskazini tunakwenda kuangalia fursa zilizopo.
*Itaendelea Alhamisi ijayo