Miaka mitatu ya EWURA katika vita dhidi ya adui wachakachuaji mafuta

29Jul 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Miaka mitatu ya EWURA katika vita dhidi ya adui wachakachuaji mafuta
  • Ushindi? Umepungua kutoka 80% hadi 4%

KWA muda mrefu kumekuwapo kilio cha uchakachuaji mafuta ya petroli, hivyo kuhatarisha vyombo vya moto, hususani magari.

Kituo cha kujaza mafuta ya petrol. PICHA MTANDAO

Baada ya tatizo hilo kuwa sugu, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), jicho la kiserikali katika eneo hilo iliamua kuingilia kati kwa kuchukulia hatua jambo hilo litowekwe kabisa.

Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo, anasema suala hilo limetatuliwa kwa kiasi kikubwa, baada ya EWURA kuja na programu ya kuweka vinasaba kwenye mafuta hayo, iliyowezesha kupunguza athari hizi kwa kiasi kikubwa.

Kaguo anasema, ni hatua iliyofanikisha kupunguza uchakachuaji mafuta kutoka asilimia 80 za mwaka 2017 hadi asilimia nne za mwaka jana.

Akizungumza na wadau wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAWAVITA), Kauo anasema EWURA ilianzisha programu hiyo, mnamo Septemba mwaka 2010, ikiweka vinasaba kwenye mafuta yanayotumika nchini.

Katika mjumuiko huo akimwakilisha Mhandisi Godfrey Chibulunje, Kaimu Mkurugenzi wa EWURA, Kaguo, anasema lengo kuu la kuchukuliwa hatua hiyo ni baada ya kuona kuwa uchakachuaji na ukwepaji unafanywa na wajanja wachache, hali yenye athari kufikia mazingira ya ushindani na haki.

“Uchakachuaji wa mafuta ni changamoto kubwa hapa nchini,  EWURA kwa kuliona hilo, imepambana na kufanikiwa kupunguza  uchakachuaji kutoka asilimia 80 hadi kufikia asilimia nne mwaka 2020,“anasema.

Kagua anafafanua kuwa mbinu zilizotumika ni pamoja na mwaka 2010, Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), kilifanya utafiti kuhusu matumizi ya vinasaba na kubaini kati ya mwaka 2010 hadi 2013 kulikuwapo ongezeko la mapato ya serikali kupitia kodi, ziada ya Sh. bilioni 468.50, manufaa yanayoendelea kupatikana.

UCHAKACHUAJI MPYA

Kaguo anaeleza kuwa pamoja na jitihada hizo za EWURA, bado ilibaini uchakachuaji mpya wa mafuta, ambao katika namna hiyo mpya unachangia kuipotezea mapato serikali.

Anasema, katika kupambana na uchakachuaji mafuta, wamebaini baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wanachanganya mafuta yaliyolipiwa kodi na yasiyolipiwa kodi.

“Moja ya jukumu la EWURA ni kudhibiti ubora na usalama na tija ya watoa huduma na uchakachuaji wa mafuta, ni changamoto kubwa nchini katika sekta ndogo ya mafuta,” anafafanua.

“Kazi kubwa imefanyika ya kudhibiti uchakachuaji wa kuchanganya petroli au dizeli na mafuta ya taa, lakini sasa kumeibuka uchakachuaji wa kuchanganya mafuta yaliyolipiwa kodi na yasiyolipiwa,” anabainisha Kaguo.

Mwana- mawasiliano huyo wa EWURA, anasema ni takribani nusu ya mafuta yanayoingizwa nchini ni mafuta yanayoenda nchi jirani, vilevile kuna mafuta yenye msamaha wa kodi na uwezekano wa mafuta ya magendo kuingia nchini.

“Vitendo vya kuingiza mafuta kwenye soko ambayo hayajalipiwa kodi pia vilikithiri. Mafuta hayo ni yale ya kwenda nchi jirani yaliyosamehewa kodi na ya magendo kutoka nchi jirani, hasa kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kaskazini,”anasema.

Kaguo anasema, ni hali iliyosababisha kuwapo ushindani usio sawa kwa wauzaji mafuta nchini, hata kuikosesha serikali mapato.

HATUA ZILIZOCHUKULIWA

Anasema mwaka 2007 EWURA ilianza kuchukua sampuli za mafuta kutoka maghala ya mafuta na vituo vyake kupima ubora uliopo, kwa ajili ya kukagua hali ya uchakachuaji na imeshachukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika waliokosa.

Hata hivyo, Kaguo anakiri kwamba pamoja na hatua zilizochukuliwa, hazijaweza kumaliza tatizo la uchakachuaji, kwani wapo wafanyabiashara wasio waaminifu wanaitrumia mbinu za ziada na kisha wakakidhi viwango vya Shirika la Viwango Tazanznia (TBS).

“EWURA iliona suluhisho ilikuwa ni kutafuta teknolojia ambayo inaweza kung’amua uchakachuaji na uingizwaji wa mafuta ambayo hayajalipiwa kodi hata ukifanyika kwa kiwango kidogo, ndipo ikaonekana kuwa teknolojia sahihi ilikuwa kuweka vinasaba kwenye mafuta inayotumika na nchi mbalimbali duniani,”anaeleza.

Hata hivyo, msemaji huyu wa wadhibiti na wasimamizi wa mafuta hayo, anasema teknolojia ya kuweka vinasaba imesaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti uingizaji mafuta hayo yasiyolipiwa kodi.

HALI YA USHINDANI

Pia, anasema matumizi ya teknolojia hiyo yamechangia kuleta ushindani sawa katika soko na mapato ya serikali yakaongezeka, kwani sasa kuna kiasi kikubwa cha mafuta kinacholipiwa kodi.

Kaguo anatoa mfano wa kiasi cha mafuta ya dizeli kinachotumika nchini na kulipiwa kodi, sasa kimeongezeka kutoka wastani wa lita milioni 80 kwa mwezi mwaka 2010 hadi kufikia ita milioni 184 kwa sasa.

Vilevile, kiasi cha mafuta ya petroli kinachotumika nchini na kulipiwa kodi kimeongezeka kutoka wa lita milioni 40 za mafuta kwa mwezi mwaka 2010 hadi lita milioni 136 kwa sasa.

TEKNOLOJIA VINASABA

Kaguo anaieleza teknolojia ya vinasaba, kwamba inahusisha kuweka kemikali maalumu kwenye mafuta, inayoweza kutofautisha nishati husika na mafuta, ambayo hayajawekewa kemikali husika.

Pia, anasema teknolojia hiyo inatakiwa kuwa na vifaa maalumu vya kupima na kung’amua kwa usahihi mkubwa mafuta yenye kiwango stahiki cha vinasaba, pia yale yamekosa au yana kiwango pungufu.

UAGIZAJI MAFUTA

Kuhusu namna EWURA ilivyookoa fedha kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini, ni kwamba aliandaa Mfumo wa Uagizaji wa Pamoja (BPS) wa Mafuta nchini.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na UDSM Aprili 2014, ulibaini BPS imesaidia kupunguza gharama Sh. bilioni 121.57 kwa mwaka. Anafafanua ni kupungua gharama za usafirishaji kwa kiasi cha mabilioni kila mwaka.

Kaguo anaendelea: “Kupungua kwa gharama za demurrage kwa Sh. Bilioni 25.7, kupungua kwa gharama za uagizaji mafuta kutokana na maboresho ya mikataba kwa Sh.bilioni 13.95 kwa mwaka.”

Anaweka bayana faida iliyopatikana kwa kutumia mfumo wa pamoja wa BPS kuwa ni kupatikana kwa taarifa sahihi za kiwango cha mafuta kinachoingizwa nchini na hivyo kuongeza mapato ya kodi ya serikali kwa kiwango cha asilimia 24 kwa mwaka 2012.

“Kuongeza ufanisi katika udhibiti wa bei za mafuta kwa kuwa na gharama halisi za mafuta yanayoingia nchini. Kurahisisha udhibiti wa ubora wa mafuta yanayoingizwa nchini chini ya mfumo huu,”anasema Kaguo.

Anasema EWURA itaendelea kusimamia taasisi na mfumo kwa ujumla, kutokana na kuwa EWURA ina utaalamu mpana zaidi na taarifa za mwenendo wa soko la mafuta ndani na nje ya nchi.

“Kutokana na ubora wa mfumo huu, taasisi nyingi za hapa nchini zimeitembelea EWURA kujifunza namna ya kuanzisha na kutekeleza mfumo wa uagizaji wa bidhaa kwa pamoja (mfano mbolea na Dawa, Bodi ya Sukari na ununuaji wa dawa za maji MSD).”anasema.