Michelle Obama awafunda wanafunzi wasichana wa Tanzania

08Nov 2016
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Michelle Obama awafunda wanafunzi wasichana wa Tanzania

UNAPOSIKIA jina la Michelle Obama, unajielekeza moja kwa moja kwa mke wa rais wa Marekani, ukiajiminisha kuwa hajawahi kupitia changamoto za mtoto wa kike au mwanamke kama ilivyo kwa wasichana wengi hasa wa nchi zinazoendelea kama Tanzania.

Imani hiyo inajengeka kwa sababu amezaliwa na kukulia Marekani, taifa linalosifiwa kwa kuheshimu haki za binadamu na hususan jinsia ya kike.Hata hivyo mwenyewe anaelezea tofauti na mitazamo hiyo.
 
Michelle hivi karibuni alifanya majadiliano ya moja kwa moja na wanafunzi wa kike wa shule za nchi za Tanzania, Peru, Jordan, Uingereza na majimbo ya Washington na New York City ya Marekani, kupitia mtandao wa ‘Skype’, akiwa na mwigizaji na mwanaharakati, Yara Shahidi, ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani yaliyofanyika Oktoba 11 katika ubalozi wa Marekani nchini.

Fursa hiyo iliwezeshwa na serikali ya Marekani kwa kushirikiana na shirika la Plan International.

Michelle akizungumzia historia ya maisha yake
tangu akiwa mtoto mdogo, mwanafunzi wa chuo na baadaye kuwa mke wa rais wa Marekani, ikiwa ni njia mojawapo ya kuwahamasisha watoto wa kike wakabiliane na changamoto za kila siku ili kutimiza kufikia malengo maishani.
 
Michelle anasema baada ya mumewe kuwa rais wapo waliohoji endapo anaweza kuwa mke wa rais mzuri, anayeweza kusimama mbele ya jamii na kutoa hoja, lakini hakuyabeba maneno hayo kwa mtazamo hasi aliyageuza kuwa fursa ya kufanya vizuri zaidi.
 
“ Sikutaka kubishana nao kwa maneno, bali kwa vitendo kuonyesha kuwa fikra zao haziko sahihi. Na nimeonyesha kuwa, ninaweza kuwa mke na mama mzuri. Haya pia yalinikuta wakati nikiwa nasoma mtu akinidharau sikuhangaika naye, nilifanya bidii na kusonga mbele zaidi, mwisho waliishia kunipongeza,” anafafanua.
 
Kusoma na kufanyakazi kwa bidii anasema kuwa kuliondoa mawazo hasi dhidi yake “Daima usikubali mtu akurudishe nyuma katika malengo yako, paza sauti yako, eleza hisia zako, huko ndiko kujiamini, hauko mwenyewe ila jifunze kupuuza sauti zenye kukatisha tamaa kwa sababu zao binafsi,”
 
 
Wanafunzi 50 wa Tanzania kutoka shule mbalimbali walishiriki katika majadiliano hayo na kumweleza mke wa Obama kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo na kumuuliza maswali mbalimbali aliyoyajibu moja kwa moja huku akishuhudiwa na wanafunzi wa mataifa mengine..
 
“Naamini wasichana duniani kote wanaweza kuwa kama mimi, kwa kuwa nilipewa nafasi ya kwenda shuleni nikasoma kwa bidii, hivyo wazazi na walezi wanapaswa kutambua umuhimu wa kutoa nafasi kwa watoto,” anasema na kuongeza”
 
“ Wakati tunasoma wazazi wangu waliniamini zaidi kuliko kaka yangu. Hiyo ilitokana na bidii niliyokuwa nayo kuwa wanaponidharau mimi niligeuza kuwa changamoto na kuzitumia kusonga mbele kielimu.”
 
Michelle ambaye huongea kwa kujiamini anasema kuwa wazazi wake hawakuwa na elimu ya chuo, lakini walimsukuma kusoma kwa bidii na kumtia moyo ikiwamo kuzikataa sauti hasi dhidi yake na mawazo yenye lengo la kumkatisha tamaa.
 
Anasema vikwazo vya kielimu vinatofautiana kati ya mtoto mmoja hadi mwingine ndiyo maana akaja na kampeni ya ‘Let girl learn’
“Tunataka kuona viongozi kupitia sera na sheria wanawapa nafasi watoto wa kike na kubadili mtazamo dhidi ya mtoto wa kike,”
 
Michelle anasema, kampeni hiyo itaendelea hata baada ya mumewe kuachia madaraka Februari mwakani, kwa kuwa anatambua umuhimu wa kuwekeza kwa mtoto wa kike kupitia elimu na kwamba bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kubadili mtazamo wa jamii dhidi ya mtoto wa kike.
 
Mwanafunzi wa shule ya Kondo –Tegeta, Nasra Abdallah, alimuuliza mke wa kiongozi huyo nini kilimsukuma kuanzisha kampeni hiyo na kuona changamoto za watoto wa kike duniani, ikiwamo nchi za Afrika kama Nigeria ambako wasichana walitekwa na kutumikishwa kingono kwa muda mrefu, mimba za utotoni na kukatishwa masomo kwa sababu mbalimbali ikiwamo wazazi kutoona umuhimu wa elimu kwa watoto wao.
 
Michelle alisema kuwa changamoto za kielimu pia zipo Marekani kwa kuwa watoto wengi hupenda starehe na kuacha kuweka mkazo katika elimu, na kwamba jitihada za kuelimisha zinafanyika ndani na nje ya nchi hiyo.
 
Michelle anasema Lets girl learn inakusanya mabilioni ya fedha kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa kike duniani kupata elimu na imefanikiwa kuwafikia watoto hao kwa kiasi kikubwa.
 
“Siku zote usiogope kushindwa kwa kuwa ukijaribu na kushindwa ndiyo unafanya vizuri zaidi baada ya  kugeuza changamoto kuwa fursa. Pendaneni, saidianeni na kupeana moyo katika changamoto mbalimbali,” anasema.
 
Mwanaharakati Shahidi anasema wasichana wanapaswa kutambua kuwa wanapopata mtu wa kuwasaidia kielimu watumie nafasi hiyo vizuri ili kumpa moyo anayetoa msaada wa kuwakomboa kimaisha.
 
“Ukijithamini utathimini anayekuwezesha kupata elimu, utayapenda maisha na kuthamini elimu ambayo utaweka bidii, hivyo wasiiache nafasi hiyo ikapotea bure,” anasema.
 
Anasema changamoto za kudharaulika au kuonekana kwa sababu ni mwanamke ni kubwa na hazikwepeki kinachotakiwa ni kuhakikisha kuwa unafanya bidii katika masomo na kila jambo ili kuwaonyesha kuwa unaweza kufanya mambo makubwa tofauti kuliko fikra zao zilivyo.
 
Wakati Michelle na Shayiri wakitoa angalizo hilo, takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA), zinaonyesha kuwa, kwa kipindi cha miaka kumi ijayo wasichana zaidi ya milioni moja duniani watakuwa wameolewa katika umri wa chini ya miaka 18.
 
Kwa Afrika inaonyesha kuwa, asilimia 42 ya wasichana huolewa wakiwa katika umri wa chini ya miaka 18.
 
Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS), mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni na asimilia kwenye mabano ni Shinyanga (59); Tabora (58) na Mara (55).
 
Nyingine ni Dodoma (51), Lindi (48), Mbeya (45), Morogoro (42), Singida (42), Rukwa (40), Ruvuma (39), Mwanza (37), Kagera (36), Mtwara (35), Manyara (34), Pwani (33), Tanga (29), Arusha (27), Kilimanjaro (27), Kigoma (29), Dar es Salaam (19) na Iringa (8).

Habari Kubwa