Michezo, nyimbo za watoto enzi hizo

14May 2022
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Michezo, nyimbo za watoto enzi hizo
  • *Nyingi zimerudiwa na wanamuziki
  • *Za kurukia kamba nazo zimo

ULIKUWA ni wakati wa watoto kucheza pamoja. Ulikuwa ni wakati wa watoto ambao walikuwa wakifahamiana mtaa mzima.

Hata kama wazazi hawafahamiani, lakini watafahamiana na kuunda ujirani na urafiki kwa sababu ya watoto.

Ni wakati ambao mijini watu walikuwa hawajaanza kujenga nyumba na kuzungushia uzio wa ukuta na mageti. Ukiona uzio basi utakuwa ni wa nyasi, makuti, au miti ya michongoma. Inawezekana vijijini maisha kama haya bado yapo, ingawa aina hii ya maisha inaanza kufutika taratibu.

Mijini, imebaki kubwa historia. Nakumbuka miaka ya 1990 kurudi nyuma, kipindi watoto wamerudi mashuleni, hasa ikifika saa 12:00 jioni, watoto hukusanyika na kuanza michezo mbalimbali, ikiwemo kuimba.

Kulikuwa na michezo ambayo huwezi kuicheza bila kuimba nyimbo. Pia kulikuwa na nyimbo tu ambazo zilikuwa zikiimbwa wakati huo wakisubiri chakula makwao, baadaye kwenda kulala.

Mpaka leo haijajulikana zilikuwa zinatungwa na nani, lakini zilikuwa maarufu sana na zilijulikana na watoto wote Tanzania nzima. Ni nyimbo chache sana ndiyo zilikuwa zinaweza kuwa ni za mkoa fulani, kwingine huwezi kuzisikia.

Nyimbo hizo mwanzoni mwa miaka ya 2000, zilianza kurudiwa na bendi mbalimbali za muziki wa dansi za kizazi kipya kama African Stars 'Twanga Pepeta', Mchinga Sound, TOT Plus, African Revolution 'Tamtam' na hasa kwenye vibwagizo vyao.

Leo tutaziangalia baadhi ya nyimbo za watoto ambazo zilikuwa maarufu sana, zikiimbwa kwa sababu mbalimbali kama vile kwenye michezo na mambo mengine yanayofanana na hayo.

 

Nyimbo za michezo

 

Tukianza na nyimbo za michezo, kuna ile ya kurukia kamba. Kuna wimbo mmoja uliopigwa na Juwata Jazz Band uitwao 'Aziza'. Huu ulitumika sana kwenye mchezo huo na kuwa maarufu sana. Sidhani kama wale watoto na wasichana wa zamani ambao kwa sasa watakuwa kinamama watu wazima watashindwa kuufahamu wimbo huu.

"Aziza sasa naomba, turudiane, hayo yamekwisha, kipenzi changu, shetani katupitia, rudi mke wangu ee, mimi mwenzio mama ninapata tabu."

Kuna wimbo mwingine ambao unaitwa 'Shilingi ya Nyerere'. "Shilingi ya Nyerere katikati kuna mwenge, doli doli, doli samwela." Mara nyingi mchezo huu ni kwamba watoto au wasichana wawili wanashika kamba, upande mmoja na mwingine, huku anayeruka anakuwa kati. Zile nyimbo ambazo huwa zinaimbwa na wote, mrukaji, walioshika kamba na hata wanaoangalia, huwa ni burudani na kumhamasisha anayeruka ili asikosee. Akikosea anatoka anaingia mwingine.

"Kioo kioo, alikivunja nani, sijui sijui, waongo nyie wote, piteni piteni, wa mwisho akamatwe, atiwe gerezani."

Huu ni wimbo uliokuwa unatumika kwenye mchezo wa kioo. Hauna jinsia, kwani ulichezwa na wote, wavulana na wasichana.

Wawili wanashikana mikono wakiwa wameiinua juu, na watoto wengine wanapita kwa foleni katikati ya wawili walioshikana mikoni, lakini wakiwa chini ya ile mikono yao iliyoshikana kwa juu.

Mwisho wa wimbo, wanaishusha chini na kumbana yule ambaye wimbo umemalizika akiwa katikati yao na juu ya mikono.

"Namsaka mke wangu namsaka mke wangu, hapa hayupo hapa hayupo, kaenda wapi kaenda wapi, kaenda kusuka kaenda kusuka, kitana kampa nani, kitana kampa nani? Kampa msusi kampa msusi, kioo kampa nani kioo kampa nani? Kampa msusi kampa msusi." Huu ni moja wa wimbo maarufu wenye michezo ya kitoto ambao maneno yake yaliwekwa kwenye wimbo mmoja wa TOT Plus.

"Yai bovu yai bovu, linanuka linanuka, linanukaje linanukaje? Pwi pwi pwi. Nina ndoo yangu, ya kuchota maji, maji ya barafu, watoto masitizame nyuma, yai bovu linapita." Wimbo huu huimbwa kwenye mchezo huo ambao watoto wanakuwa wamekaa chini na kutengeneza mduara mkubwa. Anayeimbisha ndiye anayekuwa anazunguka na kitu au kitambaaa kilichofinyangwa kama mpira hivi. Hilo ndiyo yai bovu lenyewe. Halafu akishasema msitizame nyuma, ule mpira anauweka nyuma ya mtu yoyote aliyekaa ambaye yeye amemchagua. Atayewekewa atasimama na ule mpira na kumpiga nao aliyeimbisha. Kama ukimpata, basi aliyeimbisha atarudia tena kuimbisha, lakini kama ukimkosa, yule aliyewekewa lile tambara la yai bovu, basi ataanza kuimbisha yeye.

 

Nyimbo zilizorudiwa na bendi

 

Kuna nyimbo nyingi za watoto enzi zile ambazo miaka ya 2000 maneno yake yalirudiwa na baadhi ya bendi katika kunogesha vionjo, na kuwakumbusha watu mbali.

"Amina, Amina kadala, (snowea), Amina dumpepe dumpepe, Amina Magereza, Amoina dush dush. Dada kama wanipenda, kaninunulie zeze, nikilala kitandani, zeze lanibembeleza, dada Maida, kuchomachoma kubaya, utamchoma mkweo, aliyekuzalia mumeo." Baada ya hapo kuna mwingine unaimbwa

"Bilinge bayoyo bilinge bayoyo, bilinge bayoyo tunamuomba dada Asha uje hapa, kaa chini tukuone maringo yako, bingilibingili mpaka chini." Pia kuwa wimbo wa kinyulinyuli.

"Kinyulinyuli nyulika mwanangwa wa Jumbe, kavaa nguo mbili, ya tatu kajifunika."

Mbali na hizo kuna zingine kama 

"Moja chama chetu cha umoja, mbili macho kama pilipili, tatu, ratu mwizi wa mapera, Mwanne acha uhuni, tano, kwa mchuzi wa manjano, sita, baharini kuna vita, saba, sabasaba imefika, nane, zunguka tuonane, tisa, kwa Mzungu kunatisha, kumi, kwa mateke na mangumi."

Upo pia wa mkulima mwenye shamba.

"Mkulima mwenye shamba alipanda viazi, akachimbachimba akaona mali, lololo bahati ya mtu mwenye shamba, akatupa jembe upande akaenda mjini, kununua moto kali sasa ni tajiri, lololo bahati ya mtu mwenye shamba."

 

Tuma meseji 0716 350534

Habari Kubwa