Mikakati yainyanyua Singida kutoka mkiani 2017 kuwa ya 14 mwaka jana

25Jun 2019
Elisante John
SINGIDA
Nipashe
Mikakati yainyanyua Singida kutoka mkiani 2017 kuwa ya 14 mwaka jana
  • Ni matokeo ya darasa la saba
  • Ni ushirikiano wa uongozi mkoa na wadau
  • Ufuatiliaji, usimamizi, vitendo na kuacha kukaa ofisini siri iliyojificha

BAADA ya Mkoa wa Singida kushika nafasi ya mwisho kwenye matokeo ya darasa la saba kitaifa mwaka 2017, hatimaye umeondokana na aibu hiyo, baada ya kujinasua hadi nafasi ya 14, kati ya mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

Wasichana wa Sekondari ya Kinambeu katika Wilaya ya Iramba wakipokea sehemu ya msaada wa ndoo kutoka kwa Mbunge Aysharose Mattembe, kwa ajili ya usafi, ili kuchochea morali ya ufaulu wa jinsia hiyo.

Mafanikio hayo yametokana na juhudi kubwa zilizochukuliwa na serikali, wadau wa elimu, viongozi, walimu, wazazi na jamii kwa ujumla, zilizowezesha kuukwamua mkoa huo kutoka nafasi hiyo ya ‘mkiani’.

 

Mkoa una jumla ya shule za msingi 525, 21 miongoni mwao zikiwa ni za watu binafsi.

Haikuwa rahisi kuyafikia mafanikio haya bila ya juhudi za wadau wengi kujitoa kwa dhati, kufanya ufuatiliaji, kuchukua maamuzi magumu na hata kukumbushana majukumu ili kuikimbia dhihaka ya kuitwa ‘Mkoa ulioshika mkia mwaka 2017’.

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Singida, Mwalimu Nelesi Mulungu, anasema matokeo ya mwaka jana yanauweka mkoa kwenye nafasi nzuri zaidi siku za usoni.

Hiyo ni baada ya wanafunzi 20,617 kati ya 27,653 waliofanya mtihani Septemba mwaka jana, kufaulu na hivyo kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza.

Mwalimu Mulungu anabainisha kuwa kati ya wanafunzi hao waliofanya mtihani, wasichana 14,741 na wavulana 12,668, wasichana waliofaulu ni 11,091 na wavulana 9,526, hivyo kuwezesha ufaulu kuwa sawa na asilimia 75.21 mwaka jana.

“Ufaulu kwa mwaka jana ulipanda hadi kufikia asilimia 75.21, ikilinganishwa na asilimia 62 za mwaka 2017…huu umepanda kwa asilimia 13.21, na hili ni jambo la kujivunia, ingawa bado tuna safari ndefu kuyafikia mafaniko bora zaidi,” anafafanua.

HALMASHAURI ZILIZOONGOZA

Ofisa elimu huyo anazitaja halmashauri tatu za wilaya zilizoongoza kwa ufaulu kimkoa, huku nafasi zao kitaifa zikiwa kwenye mabano kuwa ni Itigi iliyokuwa ya kwanza (50), Manispaa ya Singida ya pili (75) na Singida Vijijini ya tatu (82).

Anasema Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ambayo mwaka 2017 ilishika nafasi ya mwisho kimkoa na kitaifa pia, mwaka jana imeendelea kuwa ya mwisho kimkoa, lakini ikajinasua kitaifa kutoka mkiani baada ya kuwa ya 181, miongoni mwa halmashauri za Tanzania Bara (kitaifa).

Hata hivyo, Mwalimu Mulungu anaipongeza halmashauri hiyo baada ya Shule ya Msingi St Marie Eugenie iliyopo wilayani humo, kushika nafasi ya kwanza kimkoa, wakati ambapo halmashauri hiyo inaburuza mkia, kimkoa.

Anasema licha ya Wilaya ya Mkalama kuwa ya mwisho kimkoa, lakini uongozi wa mkoa unajivunia halmashauri hiyo kuongeza hali ya ufaulu hadi kufikia asilimia 57, ikilinganishwa na asilimia 37.08 za ufaulu, mwaka 2017.

Anasisitiza, kama ambavyo mkakati uliwekwa kuukwamua mkoa kutoka nafasi ya mwisho, juhudi hizo ndizo zitakazounganishwa pia kuiwezesha wilaya hiyo mwaka huu iweze kufanya vizuri zaidi, baada ya changamoto zake nyingi kutatuliwa.

Anazitaja baadhi ya changamoto zilizopo katika wilaya hiyo iliyogawanywa kutoka Iramba kuwa ni uwepo wa jamii ya wafugaji inayohamahama, uhaba wa walimu, mwamko duni wa elimu kwa baadhi ya familia, umaskini na miundombinu duni.

Anaomba wadau wa elimu kuisadia wilaya hiyo kuzikabili changamoto zake, zikichangizwa pia na uwepo wa jamii ya Wahadzabe inayoishi katika wilaya hiyo, huku ikitegemea asali, matunda pori, nyama pori na mizizi, kama chakula chao kikuu.

KATIBU TAWALA

Akizungumzia mafanikio ya elimu kimkoa, Katibu Tawala Mkoa, Dk. Angelina Lutambi, anasema mshikamano kati ya serikali, idara ya elimu, wataalamu wabobezi, wanafunzi, walimu na wadau wa elimu, ndio uliowezesha mkoa kujinasua katika nafasi hiyo.

Dk. Angelina anasema, baada ya matokeo ya mwaka 2017 kuonyesha Singida ni mkoa wa mwisho, Sekretarieti chini ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi, ilikutana mara moja kubaini tatizo na dosari zilizokuwa ndani ya uwezo wao ili kuzitatua.

Walifikia maazimio na kuandaa mikakati kwa ajili ya ufuatiliaji na usimamizi wenye nia ya kuhakikisha hakuna kosa litakalojirudia tena, ili kurejesha hadhi ya mkoa katika suala zima la sekta ya elimu ya msingi, katika ngazi zote.

Dk. Angelina anasema, ndipo wataalamu na wadau walielekeza nguvu kwa vitendo, badala ya kufanya kazi kwa mazoea ofisini, hatimaye wakafanikiwa kumaliza kero nyingi kabla hata ya kufika ofisini, kwa kushirikiana na jamii husika, pia jitihada za wanafunzi.

Anasema kati ya wadau hao ni, Mpango wa Kuboresha Elimu nchini (EQUIP-T), uliowezesha msaada wa pikipiki kwa waratibu elimu ngazi ya kata, zikiwamo pikipiki 21 zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 63 kwa Halmashauri ya Wilaya Singida Vijijini.

Pikipiki hizo pia zilisambazwa kwa halmashauri nyingine sita za mkoa ikiwamo, Manispaa ya Singida, Ikungi, Mkalama, Itigi, Manyoni na Iramba, ambapo waratibu walifanya kazi zao kwa ufanisi kusimamia sekta ya elimu na maendeleo kwa ujumla.

Wakati wa makabidhiano ya pikipiki hizo kwa halmashauri zote za wilaya, Mkuu wa Mkoa Dk. Nchimbi, aliwaagiza waratibu elimu kuzitunza na kufuata maelekezo ya serikali, badala ya kuzigeuza kuwa bodaboda.

“Licha ya kuzitumia pikipiki hizi kwa kazi zenu za kila siku, hakikisheni taaluma inasonga mbele…huko mnakopita muwe mnakagua na miundombinu mbalimbali na mtoe taarifa kwa viongozi wa maeneo yenu na kwangu pia, ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa,” anasisitiza.

Anawataka waratibu hao kuwajibika zaidi kwa kuwasaidia walimu waliokata tamaa ya maisha, na kuwarejesha katika hali ya upendo, badala ya kuwakaripia ili waweze kujirudi na kuipenda kazi yao, kadri walivyofundishwa vyuoni.

CCM

Wadau wengine walioshiriki juhudi za kuunasua mkoa kutoka nafasi ya mwisho ni, Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Jumuiya ya Umoja wa Wazazi, kutokana na kongamano kubwa la wadau wa elimu lililoitishwa katika ukumbi wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Singida.

Kongamano hilo lilipewa jina la ‘Maadili na Elimu ni Mapacha wasioachana, Tutimize Wajibu wetu kwa Maendeleo ya Taifa.’

Katika kongamano hilo Jumuiya hiyo, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Manispaa na wadau, walizibainisha dosari nyingi zinazosababisha Mkoa wa Singida kuanguka vibaya katika elimu.

WADAU WENGINE WALIOALIKWA

Waalikwa wengine walikuwa ni mashirika ya madhehebu ya dini, wajasiriamali, wataalamu, wadau, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) pamoja na mashirika ya umma na yale ya binafsi.

Baadhi ya maazimio yaliyopitishwa ni pamoja na msisitizo wa suala la nidhamu kwa wanafunzi, maadili kwa walimu, wajibu wa wazazi, pia suala la lishe (chakula cha mchana), kwa ajili ya wanafunzi wakiwa shuleni.

CECE & DANIEL ENTERPRISE

Shirika la Cece & Daniel Enterprise la jijini Dar es Salaam nalo limetoa mchango wake kupitia shindano lililojulikana kama ‘The 2018 Spelling BEE’, likiwa mahsusi kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Meneja mwezeshaji wa Cece & Daniel Enterprise, Upendo Mushi, anasema, lengo la shindano hilo ni kusaidia wanafunzi kutamka kwa ufasaha maneno, likianzia na shule 14 za msingi na nyingine 14 za sekondari, huku nyingine nne zikiwa za wenye mahitaji maalumu.

Anasema wanafunzi wote watashiriki, lakini watachujwa wapatikane 10 bora kwa kila shule, tayari kushiriki kwenye shindano kubwa litakalojumuisha wanafainali 320, na wengine 10 wenye mahitaji maalumu, (walemavu wa kusikia), ili kumpata mshindi.

TUME YA UTUMISHI

Nayo Tume ya Utumishi wa Walimu nchini (TSC), ni miongoni mwa wadau waliosaidia mkoa wa Singida kuimarisha matokeo ya darasa la saba.

Hiyo ni baada ya makatibu wasaidizi wa tume hiyo ngazi za wilaya kukutana, ili kubaini changamoto zinazochangia kuporomoka kwa elimu.

TSC Taifa ilijielekeza zaidi katika taratibu za kazi, yaani kufuata sheria, kanuni na taratibu za kazi, kutoa ushauri murua kwa waajiri wao ili kupunguza malalamiko na mashauri ya kinidhamu kwa walimu katika vituo vya kazi.

Masuala ya sheria, utawala na ajira kwenye maeneo ya kazi, ni kati ya mada zilizofundishwa kwa makatibu hao wasaidizi, lengo likiwa lilelile la kuboresha sekta ya elimu hapa nchini.

Kiongozi wa timu ya mkoa wa Singida Phoibe Okeyo, kutoka asasi ya Equip-Tanzania inayosaidia kuboresha elimu nchini na mkoa wa Singida kwa ujumla, aliahidi asasi hiyo kuendeleza ushirikiano na serikali, ili kuinua sekta ya elimu katika mkoa wa Singida.

COMMUNITY EMPOWERMENT

Shirika la Community Empowerment Project-4CCP linalomilikiwa na Hospitali ya Haydom mkoani Manyara, nalo limejitosa kuhakikisha linatoa mchango wake kwa jamii ya Wahadzabe, katika kijiji cha Munguli, Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.

Kwa ufadhili wa Shirika la Norwegian Church Aid (NCA) la nchini Norway, shirika hilo limejenga vyumba viwili vya madarasa, kuajiri walimu na kulipa mishahara yao katika Shule ya Msingi Munguli, na kuchimba kisima cha maji ambacho kimegharimu Sh. milioni 145, kwenye kijiji hicho.

Vyumba vya madarasa na ofisi ya walimu katika shule hiyo, kwa pamoja vimegharimu Sh. 65,000,000, huku shirika hilo likiahidi kuisaidia zaidi halmashauri hiyo, ili kuwezesha jamii ya Kihadzabe kuelimika na hivyo kuachana na maisha ya zama za kale.

Hatua hiyo imeleta mageuzi ya ufaulu wa darasa la saba na la nne, ambapo umepanda kutoka wanafunzi watano (2016) hadi 16 mwaka 2017 kwa darasa la saba, huku kwa darasa la nne wanafunzi wote wakifaulu katika wastani wa daraja A na B, ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

MIKAKATI KUINUA ELIMU 2019

Ofisa Elimu Mkoa, Mwalimu Mulungu, anasema idara yake itaendelea kufuatilia na kuhakikisha walimu wanafanya maandalizi ya kutosha katika majukumu yao, ili kuzing’arisha zaidi shule zao na mkoa wa Singida kwa ujumla.

Anasema, kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya na manispaa, idara yake itaendelea kuielimisha jamii kupitia kamati za shule na kamati za maendeleo za kata, juu ya umuhimu wa mahudhurio ya wanafunzi kuwa ni ya lazima, tangu anapoandikishwa hadi anapomaliza.

Hata hivyo, Mulungu anafafanua kuwa, hivi sasa mkoa unaendelea na juhudi za kuzihimiza halmashauri za wilaya na manispaa, zihamasishe jamii kuchangia gharama za miundombinu iliyopungua katika kila shule zake.

Mwalimu Mulungu anasisitiza kuwa, kupitia mpango wa uboreshaji wa elimu (EQUIP-T), jamii imehamasishwa kuhakikisha kila shule na kwa kila darasa kunakuwapo mwakilishi ambaye atakuwa anafuatilia maendeleo ya shule.

Anasema, idara yake itaendelea na vikao vya mara kwa mara na maofisa elimu ngazi ya wilaya, kata na walimu wakuu, kuhimiza uwajibikaji, kuandaa mitihani miwili ya utimilifu kwa darasa la saba na la nne kila mwezi, na kuwapo uwasilishaji wa upimaji kutoka kila halmashauri na kwa kila shule.

Habari Kubwa