Mila potofu zisiwe kikwazo kwa maziwa ya kwanza

26Aug 2021
Maulid Mmbaga
Dar es Salaam
Nipashe
Mila potofu zisiwe kikwazo kwa maziwa ya kwanza
  • * Yasitupwe ni chanjo, tiba kwa watoto

MAZIWA ya mama kwa mtoto mchanga mara tu anapozaliwa yana umuhimu wa kipekee kwa sababu ya virutubisho vilivyo ndani yake ambavyo humpa mtoto kinga ya magonjwa na kuimarisha ufahamu au utimilifu wa akili.

Maziwa ya mwanzo yenye rangi ya njano ni tiba, chanjo na kinga ya kudumu. Mama amnyonyeshe mtoto asiyatupe. PICHA:MTANDAO.

Lakini licha ya umuhimu huo imani potofu kuwa maziwa ya kwanza yenye rangi ya njano si salama   kwa mtoto, inaendelea kukwamisha juhudi za unyonyeshaji, pengine si Tanzania pekee bali Afrika na Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Maziwa hayo ya kwanza au ‘colostrums’, ndiyo ya muhimu zaidi kuliko mengine yoyote atakayopewa, ni  kama chanjo ya kwanza kwa binadamu na yana virutubisho vingi na pia kinga ambazo zinamuepusha mtoto na maradhi mbalimbali, anasema Dk.Peter Daudi, kutoka Hospitali na Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Kuambukiza cha Kibong’oto.

Mtaalamu huyo wa watoto, anasema utafiti unaonyesha kuwa asilimia kubwa ya kinamama maziwa yao yanatosha kabisa katika kumnyonyesha mtoto kwa miezi sita.

Wakati anayasema hayo, baadhi ya jamii huwahimiza wazazi kukamulia chini maziwa hayo kwa maelezo kuwa hayafai kwa mtoto huku wengine wakiamini kuwa yanamuumiza tumbo.  

Mathalani, jamii za kanda ya ziwa zinaelekeza mama anapojifungua kabla ya kumnyonyesha mtoto, kukamulia maziwa hayo ukutani hadi yanapokuwa meupe, bila kujua kuwa wanaharibu kitu muhimu kwa maisha ya binadamu.

Essong Jerry, mwanahabari kutoka Cameroon, anayeishi Tanzania anaeleza kuwa hata katika taifa lake, kuna mila potofu zinazowataka wanawake kuyakamulia chini na kuufanya mwiko kumnyonyesha mtoto maziwa ya njano.

Dokta Daudi, anasema kuhamasisha unyonyeshaji kutamaliza tatizo hilo baada ya kinamama kuelimishwa umuhimu wa maziwa hayo kazi inayotakiwa kufanyika kliniki na hata vijijini.

Anaendelea kusema kuwa, tatizo lililopo ni kuwa kinamama wengi hufikiria hawana maziwa ya kutosha kwasababu utengenezaji wa maziwa pia unahusisha saikolojia ya mama mwenyewe, kama ana mawazo mengi, msongo na kuchoka vyote huchangia kuyapunguza.

MTOTO ASIPEWE MAJI

Dokta Daudi, anafafanua kuwa maziwa ya kwanza ni muhimu na yana virutubisho vyote muhimu kina mama wasiyatupe. Yana maji hivyo mtoto anayenyonya ndani ya miezi sita hahisi kiu na hahitaji maji.

Akifafanua sababu za mtoto kulia na kuibua hofu kwa mzazi, anasema kunatokana na sababu mbalimbali, lakini kunyonyesha kunaweza kumbembeleza na kama mama atafuata maelekezo yote maziwa yatatosha na atashiba vizuri, lakini pia ni vizuri kujua mambo mengine yanayosababisha mtoto kulia.

Anawashauri kinamama wanaohofu kuwa wakianza kazi baada ya miezi mitatu watoto hawatashiba na kuanza kuwapa watoto maziwa ya kopo, ya ng’ombe au uji mwepesi kuwa wanakosea.

“Kabla ya kwenda kazini unaweza kukamua na kuyatunza kwenye jokofu na kuyagandisha, yanaweza kukaa kwa siku nyingi bila kuharibika na kufanya mtoto wako aendelee kupata maziwa yako, hiyo inamsaidia mtoto asipate vyakula vingine kabla ya miezi sita.” Anasema Daudi.

Anakumbusha kuwa mtoto anapaswa kunyonya ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa kwa kufuata masharti ya kiafya yanayohusu unyonyeshaji, na anaweza kunyonya mpaka angalau miaka miwili, akilishwa vyakula vingine baada ya kunyonya maziwa ya mama pekee kwa miezi sita.

“Maziwa ya mama ni muhimu sana kwa mtoto kwasababu yanajenga kinga imara ya mtoto, yanamfanya awe na makuzi bora ya ubongo, hivyo mtoto anapoyakosa lazima atapata shida kimakuzi pia atakuwa katika hatari ya kupata magonjwa mara kwa mara.”

KINACHOKWAMISHA MAZIWA

Anataja baadhi ya sababu zinazomfanya mama asitoe maziwa ya kutosha kuwa ni pamoja na matatizo ya vichocheo au ‘hormones’, mama anapojifungua kama atakuwa na matatizo mfano kisukari yanaweza kukwamisha maziwa.
Daktari anataja matumizi ya dawa za kupanga uzazi zenye vichocheo’

akisema, kama mama aliyejifungua ataanza kuzitumia kabla mtoto kufikisha miezi minne, inaweza kusababisha maziwa kupungua.

Wakati mwingine upungufu wa maziwa unatokana na matumizi ya baadhi ya dawa za kusaidia kuharakisha kujifungua kama epidural anaesthetic’ zinaweza kupunguza maziwa, anasema Dk. Daudi.

“Kumuongezea mtoto maziwa ya kopo pale baadhi ya kinamama wanapojifungua siku ya kwanza kwa vile maziwa hayatoki,  iwapo  ataanza kupewa  maziwa  kwenye hatua za mwanzo kabisa itasababisha matiti yasitengeneze maziwa kwa kiwango cha kutosha,” anaonya na kukumbusha kuwa maziwa yatatoka kwa wingi kama mzazi atamnyonyesha mtoto mara kwa mara kwani kufanya hivyo kunachochea utengenezaji wa maziwa.

Anataja kutomyonyesha mtoto usiku kuwa ni sababu nyingine ya kupungua maziwa.

“Ni kawaida kwa mama anayenyonyesha kutopenda kumyonyesha mtoto usiku ili  alale,   tabia hii ikiendelea  inapunguza kiwango cha maziwa kinachotengenezwa kwasababu usiku vichocheo vinavyosisimua utengenezwaji wa maziwa vinafanyakazi zaidi, hivyo kuongeza uzalishaji na  kama hanyonyeshi usiku,  mwili utahisi hayahitajiki na kiwango kitashuka, ” anabainisha.

Dokta Daudi anataja sababu ya mtoto kutonyonya ipasavyo inaweza kuyapunguza kwani anatakiwa kuvuta maziwa kikamilifu kwenye chuchu na akishindwa inaweza kupunguza utokaji.

Kukosa lishe bora na virutubisho mama anapokuwa mjamzito na anapojifungua, kuimarisha afya yake na ya mtoto pamoja na kutengeneza maziwa ya kutosha na kuepuka mtoto kuwa na utapia mlo ni sababu nyingine.

Msongo wa mawazo pia unahusika kwa vile mama anayenyonyesha anapokuwa na hali hiyo kutokana na sababu mbalimbali inaweza kuchangia kukausha maziwa.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), mama anayenyonyesha anatakiwa kuwa na lishe bora yenye aina zote za virutubisho kutokana na mahitaji makubwa  kwa ajili ya afya yake na kutengeneza maziwa ya mtoto na kushauriwa  kula milo kamili zaidi ya mitatu kwa siku na vyakula vingine kati ya mlo na mlo.

TFNC inaeleza umuhimu wa ulaji unaofaa kwa mama anayenyonyesha kwa sababu humpatia afya bora na virutubisho vya kutosha kukidhi ongezeko la mahitaji yake na ya mtoto anayenyonya na kuuwezesha mwili kutengeneza na kutoa maziwa ya kutosha wakati wote.

Lishe bora ni kinga na tiba ya kuzuia upungufu wa damu kwa mama na mtoto, aidha huongeza akiba ya madini chuma ambayo hutumika kwa mama na kwa mtoto kuzalisha damu.

MAMBO YA KUZINGATIA

TFNC inamshauri mama kula milo kamili zaidi ya mitatu kwa siku yenye mchanganyiko angalau chakula kimoja kutoka katika kila kundi la chakula na kula chakula kingi na cha kutosha katika kila mlo, kupata asusa (vyakula vingine) kati ya mlo mmoja na mwingine, kumeza vidonge vya kuongeza damu (FEFO) kwa kipindi cha miezi mitatu baada ya kujifungua, kutumia vyakula vilivyoongezwa virutubisho.

Hivyo ni pamoja na unga wa ngano, wa mahindi, mafuta ya kupikia na kutumia chumvi yenye madini joto, pia kuongeza ulaji wa nyama, kuku, samaki. Kutumia mayai, maziwa na vyakula vyenye madini chuma kuongeza damu mwilini.

Matunda ya aina mbalimbali na mbogamboga kwa wingi, kunywa maji ya kutosha kila siku angalau lita 1.5 kwa siku ni muhimu pia.