Mila zinavyokwamisha wanawake mkoani Shinyanga kwenye chaguzi

23Oct 2019
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Mila zinavyokwamisha wanawake mkoani Shinyanga kwenye chaguzi

UTAMADUNI ni mfumo wa maisha ambao makabila mbalimbali nchini yamejiwekea ili yaweze kuishi kwa kufuata utaratibu.

Mbunge wa Ilemela ambaye ni Naibu Waziri wa Ardhi, Angelina Mabula, ni mmoja wa wanasiasa kutoka Kanda ya Ziwa, ambako mila kandamizi zinafifisha ndoto za wanawake kugombea nafasi za kisiasa. PICHA: MTANDAO

Hata hivyo, kuna mila zingine ambazo ni kikwazo kwa jinsia ya kike kwani zinawanyima sauti wanawake, hivyo kubaki kama wajakazi kwa waume zao.

Baadhi ya makabila yamekuwa yakimnyima fursa mwanamke kuwa sehemu yoyote ya maamuzi wala kutoa mchango kwenye vikao vya familia, ukoo, hata katika mikutano ya vijiji, na hivyo kubaki kuwa mtu wa kutekeleza maagizo anayopewa.

Hali hiyo ndiyo chanzo cha tatizo la mfumo dume inayosababisha wanawake walio wengi washindwe kugombea nafasi zozote za uongozi kwa kuhofia kuvunja miiko ya mila na desturi za makabila yao.

Ndiyo iliyoathiri mfumo mzima wa maisha ya mwanamke, kwamba pamoja na kupewa elimu ya ujasiri na kudai haki ya usawa wa kinjisia kwa asilimia 50 kwa 50 hata kwenye ngazi ya nafasi za uongozi, bado walio wengi wamekuwa ni waoga.

Waoga wa kuthubutu kugombea nafasi za uongozi kwenye chaguzi mbalimbali nchini.

Novemba 24, mwaka huu kuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ajili ya kuchagua wenyeviti wa vitongoji, mitaa, vijiji na wajumbe wao.

Aidha, kuna uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais mwakani huku wanawake wakihamasishwa kujitokeza kuwania nafasi hizo.

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), ni miongoni mwa makundi ya wanaharakati wanaohamasisha wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uongozi kwenye chaguzi hizo zijazo.

Na ndiyo maana umezindua Ilani ya Uchaguzi ya Mwanamke ili kuwahamasisha washiriki kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Pamoja na hamasa hizo, bado wanawake wengi katika baadhi ya maeneo wanaogopa kufanya hivyo kwa sababu ya mila na desturi kandamizi za makabila yao.

WAZEE

Sonda Kabeshi ni mzee wa kimila mkoani Shinyanga.

Anaeleza namna mila na desturi za kwao zilivyojenga mtazamo hasi kwamba mwanamke akiwa kiongozi, mume wake atadharaulika kwa kuonekana kwamba anatawaliwa na mkewe.

Anasema mila na desturi zinamtambua mwanamke kama mtu wa kutoa malalamiko, si maamuzi, hivyo akiwa kiongozi ataonekana amedharau wanaume wote ndani ya jamii.

“Mila na desturi zetu Wasukuma, hazimpatii nafasi mwanamke kuwa na sauti ndani ya jamii, kwani ni mtu wa kuolewa, kwenda kufanya kazi za familia anakoolewa na si kuwa mtu wa kutoa maamuzi…yeye ni wa kupokea maagizo na kuyatekeleza,” anasema na kuongeza:

“Hivyo mwanamke kuwa kiongozi, kwanza ni kuvunja miiko ya mila na desturi zetu pamoja na kuonekana hana heshima kwa wanaume, dharau kwa mumewe kwani mila haziruhusu awe juu ya mwanaume na kutoa maagizo.”

Aidha, anasema kama mwanamke akiwa kiongozi, hataweza kutoa huduma stahiki kwa wananchi sababu ya majukumu mengi ya kifamilia na hivyo kukosa muda wa kufanya kazi.

DIWANI

Mariamu Nyangaka ni Diwani wa Viti Maalumu Kata ya Kitangili, Shinyanga Mjini, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Anasema changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uongozi, zinatokana na mila kandamizi zinazoendekeza mfumo dume, kutojiamini, pamoja na ukosefu wa fedha.

Anasema amekuwa akiwania nafasi ya viti maalumu badala ya udiwani wa kata, sababu ya hofu ya mfumo dume, kwamba akijitosa huenda akakosa nafasi zote.

Anabainisha kwamba kuna baadhi ya wazee ambao wameshamfuata wakimtaka agombee nafasi ya udiwani wa kata kwenye uchaguzi mkuu mwakani kutokana na uchapa kazi wake, lakini amekataa na kwamba ataendelea kugombea viti maalumu.

“Tunaiomba jamii iachane na mila kandamizi zinazoendekeza mfumo dume ili tupate fursa ya kushika nafasi kubwa za uongozi kama wanawake na si kuishia kwenye viti maalumu…tuna uwezo mkubwa wa kuongoza na kutatua matatizo ndani ya jamii,” anasema na kuongeza:

“Kwanza ni viongozi kuanzia ndani ya familia, hivyo tunapopata nafasi za kuongoza huwa ni viongozi wazuri sana…Chukulia mfano wa Mama Samia Suluhu Hassan, Ummy Mwalimu, Prof. Joyce Ndalichako na wengineo wanafanya vizuri kwenye uongozi wao.”

MBUNGE

Azza Hilali ni Mbunge wa Viti Maalum mkoani Shinyanga, anawasisitiza wanawake kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la mpiga kura na kuchukua fomu za kugombea uongozi kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Anasema wakati umefika wanawake kuonyesha uwezo wao wa kuchapa kazi, kwa kugombea nafasi za uongozi ili waonyeshe jinsi walivyo watendaji wazuri katika suala la kushughulikia matatizo ya wananchi.

MTIA NIA

Habiba Jumanne ni mwanamke aliyejitokeza kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya uenyekiti wa Mtaa wa Kitangili, Manispaa ya Shinyanga.

Anasema amewiwa kuchukua fomu hiyo baada ya kujiona anaweza kuongoza wananchi kushughulikia matatizo yao.

“Wanawake tusipojiamini kamwe hatutaweza kufikia 50 kwa 50 kwenye nafasi za uongozi, tunapaswa tusimame imara na ndio maana nimechukua fomu ya kugombea uenyekiti wa serikali ya mtaa na nina imani nitashinda,” anasema.

UWT

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake CCM, Wilaya ya Shinyanga Mjini (UWT), Shambuo Katambi, anasema wao kama CCM, wameshaweka mkakati wa kuhamasisha wanawake kujitokeza kujiandikisha pamoja na kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu, na uchaguzi mkuu mwakani.

Anasema katika mkakati huo wamekuwa wakitembelea wanawake maeneo mbalimbali na kufanya nao mikutano ya hadhara na ya ndani, lengo likiwa ni kutoa hamasa ili wajitokeze kujiandikisha na kugombea nafasi za uongozi kwenye chaguzi zijazo.

“Sisi kama UWT, tunatambua kuwapo kwa changamoto nyingi zinazomnyima fursa mwanamke kushika nafasi kubwa za uongozi, likiwamo suala la mila na desturi kandamizi zinazotokana na mfumo dume, rushwa ya ngono na ndio maana ya kupeana elimu,” anasema na kuongeza:

“Wito wangu kwa wanawake wenzangu wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa Novemba 24 na uchaguzi mkuu mwakani… wasiogopeshwe na changamoto zitokanazo na mila.”

Aidha, Katambi anawataka wanawake wapendane wenyewe kwa wenyewe, na kuacha tabia ya kusemana vibaya pale mwenzao anapojitokeza kuwania nafasi za uongozi, bali washirikiane naye kikamilifu pamoja na kumpigia kura nyingi za ndio ili ashinde na hatimaye awainue kidedea wanawake wenzake.

“Kuna tatizo kubwa vilevile la wanawake kusemana vibaya, kumtafutia visa mwanamke mwenzao, hasa pale anapojitokeza kuwania nafasi za uongozi, kumkalia vikao visivyo na maana ili ashindwe... nawaomba waache tabia hiyo, washikamane,” anafafanua.

CCM

Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Agnes Gregory, anataja takwimu za wanaCCM waliojitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi ya uenyekiti wa vitongoji kuwa ni 172, huku mwitikio wa wanawake ukiwa ni mdogo.

Anasema Wilaya ya Shinyanga Mjini, ina tarafa sita ambazo ni Kolandoto, Kizumbi, Mwamalili, Old Shinyanga, Ibadakuli, na Mwawaza.

Hata hivyo Agnes anabainisha kwamba watu waliojitokeza kuchukua fomu za kugombea uenyekiti wa vitongoji ni 172, wanaume wakiwa 151, na wanawake 21 uwiano ambao si sawa kijinsia.

“Tarafa ya Kolandoto waliojitokeza kuchukua fomu za kugombea uenyekiti wa kitongoji ni 23, wanaume 21, wanawake wawili. Tarafa ya Kizumbi waliochukua fomu ni 43, wanaume 37, wanawake sita na Tarafa ya Mwamalili waliochukua fomu ni 19, wanaume 19, hakuna mwanamke," anasema na kuongeza:

"Kwa upande wa Tarafa ya OldShinyanga waliochukua fomu ni 34, wanaume 29, wanawake watano, Tarafa ya Ibadakuli waliojitokeza ni 37, wanaume 30 wanawake saba na Tarafa ya Mwawaza waliochukua fomu ni 16, wanaume 15, na mwanamke mmoja.”

Idadi hiyo ndogo ya wanawake waliojitokeza inamfanya Agnes atoe wito kwa wanawake kujitokeza kugombea nafasi zilizobaki na waachane na tabia ya kuogopa kushindana na wanaume.

Habari Kubwa