Misitu inavyotikisa maabara zinazosaka tiba ya corona

02Jun 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Misitu inavyotikisa maabara zinazosaka tiba ya corona

MOJA ya vitu muhimu duniani sasa ni misitu na mimea mbalimbali ambayo ni hazina kuu kwa binadamu na ulinzi wa mazingira ardhini na angani.

Mmea ni chanzo cha dawa, huliwa na watu kabla ya kusindikwa viwandani na pia hutumiwa inapochunguzwa kimaabara na kutengenezwa dawa za kila aina.PICHA :MTANDAO.

Kwa mfano mapafu ya dunia au misitu kama Congo au Amazon, ndiyo inayoondoa gesiukaa angani na kuingiza gesi ya oksijeni ambayo inatumiwa na binadamu na viumbe wengine kwenye michakato muhimu ya maisha.

Ni kazi inayofanywa na mimea au misitu na ndivyo inavyotimiza jukumu la kusafisha hewa. Utafiti na machapisho mbalimbali yanafahamisha kuwa misitu na mimea ni chanzo muhimu cha dawa duniani.

Aidha, uzoefu na matumizi vinaonyesha kuwa mimea huota na kukua na katika mchakato huo huwa inadhurika na hata kupatwa na magonjwa kupitia vimelea na fangasi.

Katika hali hiyo ustawi wa misitu na mimea hudhoofika lakini hujitibu kwa namna moja au nyingine katika mazingira yake.
Ni jinsi gani hali hiyo hufanyika inabakia kitendawili ambacho Mungu ambaye ni tabibu mkuu alikiweka tangu uumbaji maana aliumba kwa ufanisi.

Kadhalika, mwili wa binadamu nao uliumbwa ukiwa na uwezo wa kupambana na magonjwa mbalimbali kupitia mfumo wake wa kujikinga. Jamii za vizazi vilivyotangulia ziliishi kwa afya kwa miaka mingi kwa kutegemea nguvu zao za miili.

Hali iliyoimarishwa kupitia mfumo wao wa kuishi kwa kufanyakazi wakitumia nguvu ya mwili na kula vyakula sahihi kuujenga mwili na iwapo itatokea kutojisikia vizuri walitumia dawa za mimea.

Mambo yalianza kubadilika maendeleo yalipoanza kuchukua nafasi yake na ugunduzi kuanza kupitia mapinduzi ya viwanda.

Mifumo ya kufanyakazi ilianza kuwa tofauti kadhalika, namna ya kuishi na vyakula vilivyotumika kwa kutozingatia umuhimu wa lishe bora kwa minajili ya kuimarisha nguvu za mwili.

Maendeleo ya viwanda yalihusisha pia utengenezaji dawa kupitia viwanda na katika mwelekeo huo umuhimu wa misitu na mimea kama vyanzo muhimu vya dawa ulizingatiwa.

Kwa kutambua hali hiyo wataalam walijikita katika kutafuta miti na mimea yenye vinasaba vya kutibu magonjwa mbalimbali.

Aina nyingi za miti na mimea zilikusanywa na kufanyiwa uchambuzi wa kina kisayansi na hatimaye kupata aina zinazofaa kwa dawa.

Kupitia viwanda utengenezaji wa dawa ukaimarika hasa kwa kutumia vinasaba vya kutibu na kutokomeza vimelea au kupunguza nguvu ya virusi na kuanza kutengenezwa kwa vingi na viwanda vya dawa kuimarika.

Inaaminika kuwa asilimia 75 ya dawa zinazotengenezwa duniani asili yake ni misitu, miti na mimea.

VIRUSI VYA CORONA

Sasa COVID-19 imevamia dunia na mabara zote zimezingirwa na virus vya corona ambavyo ndicho chanzo cha COVID-19 vinavyoelezwa kuwa ni ugonjwa uliozuka Desemba, 2019.

Hii ni kutokana na corona kuanzia China kwenye jimbo la Hubei ndani ya jijini la Wuhan na kusambaa dunia nzima.

Mpaka sasa ugonjwa huu ni hatari kwa uhai wa binadamu hakuna chanjo wala dawa ingawa tunasema baadhi ya mitishamba inasaidia kuimarisha nguvu za mwili hivyo kupambana na COVID-19 na hatimaye wagonjwa kupona.

Itakuwa faraja kubwa iwapo chanjo au dawa ikaweza kupatikana kutokana na rasilimali misitu na mimea.

MIMEA TIBA

Mimea na miti inachangia sana kwenye maendeleo ya viwanda dawa. Hivyo yawezekana COVID-19 ikapata udhibiti kutokana na nguvu za miti na mimea.

Naviangalia virusi vya corona kama kitu cha ajabu ambacho hata mwanzo wake haujulikani kiuhalisia. Hii inatokana na jinsi virusi hivyo vilivyosambaa kwa kasi kubwa na kwa dunia nzima na kusababisha maafa makubwa kiuchumi, kiafya na kijamii.

Ajabu kirusi hiki kimekuwa tishio kwa maisha katika mataifa yaliyoendelea zaidi yenye mifumo bora na kisasa katika sekta ya afya lakini pia kiuchumi.

Nchi za uchumi mdogo za Afrika Kusini ya Sahara, ikitokea hali kama ilivyoripotiwa Ulaya na Marekani wasingeshangaa maana inafahamika kuwa wanaishi ndani ya mifumo dhaifu ya kiafya na uwezo mdogo kiuchumi.

Hivyo kwa magonjwa kama malaria, kipindupindu au kuhara yamekuwa ya madhara lakini watu wanaishi.

Lakini 2020 imezuka COVID-19 ambayo haina matibabu ya kuaminika lakini Afrika imepambana nao kikamilifu kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu aliye muweza wa yote na tabibu namba moja aliyeumba viumbe ni kuvipa mfumo wa jeshi la kinga unaovizuia kupambana na magonjwa na kuyadhibiti, kwake hakuna lisilowezekana.

Ndiyo maana nguvu zetu zinaelekezwa kwanza kwa Mungu muumba wetu na pili, katika kupambana kuzuia maambukizo ya COVID-19 yasisambae sana mijini na vijijini.

TAHADHARI MUHIMU

Kila mmoja achukue tahadhari kikamilifu, kuvaa barakoa muda wote, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji yanayotiririka pamoja na sabuni.

Aidha, ni lazima kutumia vitakasa mikono (sanitizer), kuepuka misongamano isiyo ya lazima; kutoshikana mikono au kukumbatiana, kujifunika kwa kitambaa safi au sehemu ya mbele ya kiwiko cha mkono wakati wa kupiga chafya au kukohoa.

Kadhalika kutulia nyumbani iwapo hakuna shughuli muhimu ya kufanya nje ya nyumbani ya lazima na muhimu ya kukupeleka kwenye mikusanyiko.

Vilevile, hatua zitakazochukuliwa kama za kisera na udhibiti zilenge kuimarisha usalama wa chakula na lishe maana miili ikiendelea kuwa dhaifu ndipo COVID-19 itapata nguvu.

Pia suala la upatikanaji maji safi na salama ni jambo la msingi sana. Kadhalika, vita yetu kwa COVID-19 iimarishwe kwa kutumia matibabu asilia kupitia mitidawa kama kujifukiza lakini kwa njia sahihi na kwa wakati muafaka na isiwe kiholela.

Mwandishi ni Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki mstaafu.

Habari Kubwa