Miti kufunika vyanzo vya maji nchi nzima

13Jan 2019
Frank Monyo
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Miti kufunika vyanzo vya maji nchi nzima

MABADILIKO ya tabia nchi ni janga ambalo linaongeza maafa duniani ndicho chanzo cha tsunami, vimbunga vinavyoezua mabati mitaani, joto na jua kali, viuatilifu sugu lakini pia yanahusika na kasi ya ukame inayokausha vyanzo vya maji na kuathiri mfumo wa ikolojia ya misitu na upatikanaji wa mvua.

Chanzo cha maji kilichotunzwa kama hiki si rahisi kukauka. Ndiyo maana serikali imeanzisha kampeni za kupanda miti kufunika vyanzo vya maji nchi nzima.

Ndiyo maana katika harakati za kuokoa maji nchini, serikali inahimiza upandaji miti kuzunguka vyanzo vyote vya maji kila sehemu, kwani bila kufanya hivyo kitisho cha uhaba wa maji na mito, maziwa na visima kukauka ni kikubwa mno.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya MajiSafi na MajiTaka Dar es Salaam (Dawasa) Cyprian Luhemeja, mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na mji wa Bagamoyo inategemea vyanzo vikuu viwili vya maji ambavyo ni mito na visima kwa maana hiyo nguvu kubwa imewekwa na Dawasa kuhakikisha vyanzo vinatunzwa.

"Sisi Dawasa tusipo kuwa mstari wa mbele katika utunzaji wa vyanzo hivi vya maji miaka 10 ijayo Dar es Salaam huduma ya maji itakuwa na changamoto kubwa ikizingatiwa kuna kasi ya ongezeko la watu na mabadiliko ya tabia nchi kwahiyo lazima tuvilinde na kutunza vyanzo hivi", Anasema Luhemeja

Anaongeza kuwa kwa mwaka 2019 Dawasa imejiwekea malengo kuwa ifikapo Desemba usambazaji wa maji kufika asilimia 95 hivyo pamoja na mambo mengine utunzaji wa vyanzo vya maji ni muhimu katika kutimiza malengo hayo.

"Kazi inayoenda kufanyika ni kuongeza maunganisho ya maji kwa wateja wapya kazi ambayo ilianza mwaka jana na mwaka huu na itakwenda kwa kasi kubwa lakini juhudi hizi ni lazima tuwe na maji ya kutosha hivyo kampeni hii itakuwa ya umuhimu wa kipee kwetu ", Anasema Luhemeja.

KAMPENI

Kampeni za kulinda vyanzo vya maji hivi karibuni zilizinduliwa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa. Anayeeleza kuwa ni programu ya nchi nzima, inayolenga kukabili upungufu wa maji na kuvitunza vyanzo viwe endelevu.

Akiwa mkoa wa Pwani, Waziri Mbarawa anasema utunzaji wa vyanzo vya maji utakabiliana na changamoto ya kutishia upatikanaji wa maji ya uhakika kwa Watanzania.

Katika ziara hiyo mkoani Pwani miti zaidi ya 15,000 inakadiriwa kupandwa Ili kulinda mto Ruvu unaopeleka maji katika chanzo cha maji cha Ruvu Juu.

Waziri Mbarawa anasema mamlaka zote za maji nchini zinao wajibu wa kusimamia sheria ya utunzaji wa vyanzo vya maji na yeyote atakayekamatwa sheria ifuate mkondo wake.

Profesa Mbarawa anasema ni pamoja kulima kiholela pembezoni mwa mito, kutumia mbolea na viwandani zinaharibu vyanzo vya maji na pia kuathiri ubora wa maji na hivyo kufanya mamlaka kutumia fedha nyingi kuyasafisha .

"Ulimaji holela unaofanywa katika vyanzo hivi si sahihi, watu wanatifua udongo na hivyo kuathiri ubora wa maji ya mto sitakubali, lazima tuchukue hatua ili Watanzania wapate maji lakini watoto na wajukuu wetu wayakute ," Anasema Waziri Mbarawa na kutoa wito kwa mamlaka za maji kuhakikisha zinaweka utaratibu wa kupanda miti kwenye vyanzo hivyo ili kuvilinda muda wote.

MITI DAR ES SALAAM

Akizindua kampeni hiyo mwishoni mwa mwaka jana kwa kupanda miti kwenye chanzo cha maji Mto Kizinga, Mbagala jijini Dar es Salaam, Waziri Mbarawa anasema ili kuwe na vyanzo endelevu vya maji nchini ni lazima vitunzwe na sheria ya kukaa umbali wa mita 60 kutoka mtoni ni lazima kuzingatiwa na wale wanaokaidi wanachukuliwa hatua.

"Kuna watu wanaharibu vyanzo vya maji kwa kufanya shughuli za kilimo na kulisha mifugo haya yanachangia uharibifu hivi kwa sehemu kubwa na kusababisha ukosefu wa maji hasa wakati wa kiangazi", Anasema Mbarawa na kusisitiza:"Ili tuwe na maji endelevu lazima tupande miti, halafu kuondoa shughuli mbalimbali kama za kilimo ambazo kwa sehemu kubwa zinasababisha vyanzo kukauka,"

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva, anakizungumzia chanzo cha Mto Kizinga anasema kinahudumia Wilaya ya Temeke na kwamba kilianzishwa mwaka 1949 na wakoloni wa Kiingereza na kwamba ni lazima kitunzwe, wale wote wanaoendesha shughuli kando ya vyanzo vya maji, waache na kwamba atasimamia sheria.

BONDE LA WAMI/RUVU

Katika hatua ya kutunza vyanzo vya maji, mwishoni mwa mwaka 2018 Bodi ya Maji Bonde la Wami na Ruvu ilifyeka mazao mbalimbali yaliyolimwa pembezoni mwa Mto Ruvu na ndani ya mita 60 kutoka kwenye mto huo katika eneo la Ruvu Darajani mkoani Pwani.

Ofisa Maji wa Bonde la Wami/Ruvu, Simon Ngonyani, anasema kuwa zoezi hilo ni muendelezo wa operesheni ya kuwaondoa watu wanaofanya shughuli za kibinadamu ikiwamo kilimo na kujenga makazi ndani ya mita 60 kutoka mto huo ili kulinda chanzo hicho cha maji.

"Tukiwaachia hawa wakulima wafanye watakalo wanasababisha mitambo ya Ruvu Chini na Juu kuungua kwasababu watu wanalima hivyo michanga inaingia kwenye mto inapunguza kina cha maji na kusababisha mashine za kuchuja maji kuungua.," anasema Ngonyani.

Anasema kutokana na wakulima hao wanaolima kando ya mto kwa kutumia mbolea za chumvi chumvi kunapelekea usalama wa maji hayo kupotea kwa watumiaji hivyo watu wafuate sheria ili kuyalinda.

"Tumeamua kusimamia sheria hatutawabakisha, leo tunafyeka mazao yote yaliyopo ndani ya mita 60 lakini kinachofuatia ni nyumba ambazo zipo ndani ya mita 60 pia tutazifanyia kazi," anasema Ngonyani.

MITI MTWARA

Akiwa mkoani Mtwara, Waziri Mbarawa anatoa maagizo kwa bodi zote za mabonde tisa kuweka mkazo na mipango madhubuti ya kusimamia na kutunza rasilimali za maji ziweze kuwa endelevu.

Anasema kumekuwa na uharibifu mkubwa katika chanzo cha Mtawanya kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Mjini hali inayohatarisha kupungua maji kwa kiasi kikubwa.

"Naagiza bodi zote za mabonde nchini kutilia mkazo suala hili la utunzaji wa vyanzo vya maji kwani hali ni mbaya hata kusababisha ukosefu wa maji ya kutosha kwa ajili ya miradi inayoendelea kutekelezwa. Anasema Prof. Mbarawa

Anasisitiza kuwa vyanzo vyote vya maji nchini vitunzwe na kulindwa kwa kupandwa miti maalumu inayohifadhi maji na kwa wale wanaofanya shughuli za kibinadamu waache tabia hiyo na watakao kaidi wachukuliwe hatua.

‘‘Hatutaki kupata hasara kwenye miradi tunayowekeza fedha nyingi, halafu baadae iwe kama magofu kwa kukosa maji....Imefika hatua kuwa ni lazima tuchukue hatua za lazima kuinusuru taifa letu na uhaba wa maji....Niwatake wananchi watoe ushirikiano wa karibu na Serikali kuhakikisha vyanzo vyetu vyote vinakuwa endelevu kwa kuzalisha maji ya kutosha na kuwa na uwezo wa kutoa huduma ya uhakika kwa miaka ijayo’’, Anasema Prof. Mbarawa.

UONGOZI WA WILAYA

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Evod Mmanda, anawataka wananchi wazingatie sheria iliyopo ya utunzaji vyanzo vya maji kwa hiari pasipo serikali kutumia nguvu.

Anaongeza kuwa Wizara ya Maji imetoa Shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya malipo ya madai kwa wakandarasi mbalimbali wanaotekeleza miradi ya maji katika Mkoa wa Mtwara, ambapo uzalishaji wa maji kwa siku kwa mji wa Mtwara umefikia lita milioni 10, huku mahitaji kwa siku ni lita milioni 13.7.

Anasema fedha hizo zimetolewa kwa lengo la kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma, ambapo hadi sasa miradi 45 ikiwa imeshakamilika na mingine 33 ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.