Mitihani inavyowasubiri walioomba kuteuliwa CCM

05Aug 2020
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Mitihani inavyowasubiri walioomba kuteuliwa CCM

MCHAKATO wa kura za maoni kwa makada wa CCM wanaoomba kuteuliwa kuwania ubunge, uwakilishi na udiwani, unaendelea kupamba moto, safari hii walioibuka washindi nao wakisubiri hatima zao.

Kazi hiyo ya ‘kukatwa’ au ‘kung’ara’ ilianza tangu Julai 20 mwaka huu, imewaachia vicheko na vilio baadhi ya makada wa chama hicho baada ya wengine kuibuka washindi, wengine kuambulia kura chache na wapo waliiondoka na ziro, kwani ndiyo yaliyokuwa maamuzi ya wajumbe.

Baada ya mchakato huo ambao kila mgombea alipewa nafasi ya kujinadi kisha zamu ya wajumbe 'kuwachinja', ikafuata walioachiwa vicheko na vilio wamepatikana na sasa vikao zaidi vya CCM vinakuja.

Inawezekana wale walioambulia kura chache, watakuwa wamekosa matumaini wakidhani kwamba, malengo ya kutaka kuwatumikia wananchi kupitia ubunge, uwakilishi au udiwani yamezimwa.

Hata hivyo, uongozi wa juu wa CCM unasema, wale walioibuka na ushindi wasichekelee, kwa vile mchakato wa kupata makada wa kuwakilisha chama katika uchaguzi mkuu bado unaendelea.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, anabainisha hilo, wakati akihojiwa na vyombo vya habari, hali ambayo inaonyesha kuwa walioongoza katika kura hizo hawapaswi kujiamini kwamba wamefanikiwa.

Katibu Mkuu Bashiru anasema, katika kuwapata makada wa kupeperusha bendera ya chama miongoni mwa wale walioshinda katika kura za maoni, kuna vigezo vya msingi ambavyo chama kitavingatia.

Kauli hiyo ya Dk. Bashiru inaonyesha kwamba, mazoea ya zamani ya kupata ushindi mkubwa katika kura za maoni na kujihakikishia kupitisha na vikao vya juu hayapo tena bali kuna darubini kali itakayomulika.

Hivyo, kwa maana nyingine ni kwamba, walioongoza katika kura za maoni wasishangilie wala wasijipe matumaini, bali wawe kimya wakisubiri hatua nyingine za maamuzi, ambazo ni mchujo.

Kwa maelezo ya Katibu Mkuu ni wazi kada anaweza kuwa ameshika nafasi ya kwanza kwenye kura za maoni, lakini akajikuta ameachwa na kuchukuliwa mwingine ambaye uongozi utaona anatosha.

Kiongozi huyo anasema, ushindi kwenye kura za maoni ni hatua muhimu, lakini siyo kigezo pekee cha uteuzi, hatua ya uteuzi inafanywa kwenye vikao vilivyoainishwa kikatiba kwa madiwani wa aina zote.

"Kikao cha mwisho cha uteuzi ni Halmashauri Kuu ya Mkoa, kwa wabunge na wawakilishi wa ngazi zote hatua ya mwisho ya uteuzi ni kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa," anasema Dk. Bashiru.

Anasema, baada ya kura za maoni, majina yote yanajadiliwa moja baada ya jingine yanapewa alama kutegemea na vigezo vya sifa za uanachama, uongozi, mwenendo wa mgombea na uzoefu wake.

"Vilevile ujasiri wake mchango wake katika jamii, kukubalika kwake na wakati mwingine dosari zake na uhusika wake katika utii wa taratibu na kanuni wakati wote wa mchakato," anasema.

Anaeleza kuwa wapo ambao wakishinda kura za maoni, ukioanishwa na sifa hizo wanaweza kuteuliwa pia wapo ambao wakishinda kura za maoni, ukioanishwa na vigezo vingine wanaweza wasiteuliwe.

"Lakini matarajio yetu ni kwamba kutakuwa na uwiano wa aina fulani kati ya matokeo ya kura za maoni na uteuzi wa mwisho wa waliojitokeza kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hizo," anasema.

Aidha, wenyeviti wa chama hicho wa wilaya na mkoa, ambao walijitosa kuwania mojawapo ya nafasi hizo, hawaruhusiwi kushiriki katika vikao vya maamuzi, kwa maelezo kuwa wana maslahi.

MCHAKATO WA KWANZA

Baada ya mchakato wa kwanza uliofanywa na wajumbe, sasa unaingia wa pili wenye lengo la kuwapata makada sahihi, ambao CCM itawapa kazi ya kupeperusha bendera ya chama kwenye uchaguzi mkuu.

Hii inatokana na ukweli kwamba, CCM huwa ina utaratibu unaotumika kuwapata makada hao kwa kupitia mchakato huo unaoanzia katika ngazi ya wilaya na kufuatiwa na ya mkoa.

Inaelezwa kuwa mkoa una jukumu la kuitisha vikao ili kujadili na kuweka alama kwa walioomba kuteuliwa na kisha kutoa mapendekezo, katika zoezi lote la kuwapata wagombea sahihi.

Hao ni wagombea waliopatikana kwa kupigiwa kura na wajumbe wa chama hicho, huku wengine kama nilivyoeleza awali, wakiambulia kura chache wakiwamo hata wanasiasa wakongwe.

Zaidi ya wabunge 40 wameanguka katika kura za maoni kutoka vyama mbalimbali vya siasa, huku wale wa CCM wakiwa ni wengi, hali ambayo inaonyesha kuwa wajumbe wamewapa ujumbe wa kuwataka kupumzika.

Hatua ya kuwatosa hata wanasiasa maarufu imewafanya wajumbe wajipatie umaarufu mkubwa miongoni mwa Watanzania na sasa kila kona jina lao limekuwa likitajwa mara kwa mara katika mambo ya utani.

Baadhi ya wabunge wakongwe wa chama hicho walianguka kwenye kura za maoni zilizofanyika hivi karibuni, hali inayoonyesha kwamba, huenda wajumbe wamewachoka na sasa wanataka sura mpya.

Miongoni mwao ni Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela), Profesa Jumanne Maghembe (Mwanga), Dk. Mary Nagu (Hanang), William Ngaleja (Sengerema), Dk. Shukuru Kawamba (Bagamoyo), Dk. Deodorus Kamala Nkenge na Charles Kitwanga (Misungwi).

Panga hilo halikuwakumba CCM tu bali hata wabunge wa upinzani nao ambao idadi yao pamoja na wale wa CCM ni zaidi ya 40, waliotoswa na wajumbe wa vyama vyao katika kura za maoni.

Lakini kwa upande wa CCM, imeshaweka wazi kwamba kushinda katika kura siyo sababu ya kushangilia, bali kuna mchakato unaendelea wa kuwapata watakaopeperusha bendera ya chama, lakini kwa kuzingatia vigezo.

Habari Kubwa