Miundombinu ikiboreshwa vijijini madaktari wote watakwenda huko

11Jun 2019
Raphael Kibiriti
Dar es Salaam
Nipashe
Miundombinu ikiboreshwa vijijini madaktari wote watakwenda huko

WIKI iliyopita tuliwaletea sehemu ya kwanza ya mazungumzo aliyoyafanya Rais mpya wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Costantine Alex Ntanguligwa na Nipashe juu ya masuala mbalimbali katika sekta ya afya.

Wahitimu wa astashahada, stashahada, shahada za awali na shahada za uzamili katika upande wa afya wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), wakila kiapo cha uaminifu wakati wa mahafali ya 12 yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. PICHA: MTANDAO

Katika sehemu hii ya pili na ya mwisho, Rais huyu anazungumzia masuala mbalimbali yakiwemo ya nini kifanyike ili madaktari wasikwepe kwenda maeneo ya vijijini kuliko na asilimia 70 ya Watanzania wote takribani milioni 55.

Endelea na mahojiano hayo ambapo Ntanguligwa anaanza kufafanua changamoto za rasilimali watu, vifaa tiba na siasa kuingia kwenye kada ya afya.

SWALI: Unaweza kuzifafanua zaidi changamoto hizi?

JIBU: Tukianza na changamoto ya wataalamu, pengine tatizo hili linaanzia kwenye ajira. Kwamba watu hawaajiriwi wa kutosha kwani kwa sasa hali yetu siyo nzuri sana kama taifa.

Bado madaktari wetu wanaona watu wengi sana na hali hii inaifanya sekta yetu ya afya kuwa ni ya watu kama wakujitolea.

Hata hivyo uzuri ni kwamba tunapokuwa trained(kwenye mafunzo), tunafundishwa kukutana na hali kama hizo.

Kwa hiyo utaona watu wengi hawapendi kwenda vijijini, watu wote wanataka kukaa mjini. Na kimsingi, huduma zetu za afya vijijini bado ziko duni sana. Zinahitaji kuendelezwa kwa kiasi kikubwa.

Sasa kwa minajili ya raslimali watu, nchi yetu inapata watumishi wengi sana wa afya wanaomaliza kila mwaka tofauti na miaka ya zamani.

SWALI: Sasa shida hapo iko wapi?

JIBU: Shida inakuja serikali ina uwezo wa kuajiri kwa kiasi gani ili kuendana na matakwa ya wananchi pengine katika viwango ambavyo Shirika la Afya Duniani (WHO) linavihitaji? WHO inashauri daktari mmoja aone walau wagonjwa 300, lakini kwa Tanzania daktari mmoja anahudumia wagonjwa 20,000.

Hata hivyo, wanaohitimu kwa miaka ya sasa nchini ni wengi tofauti na miaka ya nyuma. Vilevile tukiangalia vifaa tiba, utaona mwisho wa siku ni matatizo ya kimfumo na serikali nafikiri ina wajibu sasa wa kuhakikisha dawa, vifaa vinatosha.

Kwa kweli ukienda vijijini utakuta hali si nzuri na vifaa vya msingi kabisa unaweza ukakuta vinakosekana.

Kwa hiyo niisihi serikali pengine kama inasikia itafute namna ya kuhakikisha madaktari wanapatiwa vifaa vya kufanyia kazi.

SWALI: Ulitaja mambo matatu, la tatu nalo unalielezeaje?

JIBU: Jambo la tatu ambalo nimeliongelea ni kuhusu matumizi ya siasa katika taaluma ya afya. Niseme kuwa siasa ni sehemu ya maisha.

Wote tunazaliwa kwenye siasa, tunakulia kwenye siasa, siasa inatuathiri kila siku, lakini lazima tuwe na utaratibu wa siasa kwenye sekta ya afya, kuanzia kwa policy makers (watunga sera) wanaotengeneza hizi sera zetu za kiafya.

Hivyo tatizo linaanzia kwenye wizara, kwamba matatizo yanaanzia huko kunakowekwa vipaumbele. Nashukuru kwa mwaka huu bajeti ya afya imeongezeka na itafanya mambo makubwa.

SWALI: Kwa hiyo mambo yatakuwa mazuri?

JIBU: Inategemea kwenye resource mobilization, resource allocation (upatikanaji na ugawaji wa rasilimali), kote huko kuna haja ya kufanya kitu.

Lakini kama nilivyosema wanasiasa hawapaswi kuiingilia taaluma kupitia, matamko yao mfano yale yaliyotolewa Iringa na Arusha, yanakuwa yanatuathiri na kutukatisha tamaa kwa namna moja au nyingine.

SWALI: Hivyo ushauri wako ni upi kwa upande huo?

JIBU: Kwa hiyo ninawasihi wataalamu wa afya kujiingiza zaidi kwenye siasa kwa sababu tunachokiona ni matokeo ya sisi kuwa nyuma. Kwamba ukiwa na mwanasiasa anayeelewa taaluma vizuri, anakuwa na uwezo wa kudhibiti na kuratibu vitu vizuri zaidi kuliko kukaa nyuma kama watalamu wa afya na kuwaachia wanasiasa wafanye wao, matokeo yake wanatulazimisha tufanye kazi kisiasa kuliko taaluma yetu.

SWALI: Hebu tueleze wewe ni mwanafunzi wa udaktari unasomea nini sasa, uko mwaka wa ngapi na kwa nini uliamua kusomea udaktari?

JIBU: Eee ahsante.. Swali la kwa nini niliamua kusomea udaktari huwa kuna msemo mmoja kwamba kila mmoja hapa unayemuona kuna sababu iliyofanya asomee udaktari.

Eee wanasema, kila mtu ana stori yake, kwangu mimi naamini udaktari ni zaidi ya kazi ila ni wito kama ilivyo miito mingine.

Kwamba kuwa daktari unaitwa na pengine inaanzia na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo baraka hizi na wito huu unaweza kukupitia kwa namna tofauti. Mimi nilizaliwa nikakulia katika familia ambayo mama ni mwalimu na baba ni mhandisi, lakini unaweza ukashangaa mwisho wa siku nimetamani kuwa daktari.

Kwa kweli nikiwa shule ya msingi, nilipenda kuwa Mhandisi kama baba yangu na nilikuwa najiita Mhandisi Ntanguligwa mpaka nilipofika kidato cha tatu ndipo nilipobadilisha mawazo.

Ni vyema tufahamu pia dunia yetu ni ya utandawazi sasa, hivyo unaweza ukakutana na mtu akaku-inspire (hamasisha) kwa namna tofauti.

SWALI: Kwa hiyo kuna mtu wewe aliyekuhamasisha?

JIBU: Ni kweli, mmoja wa watu aliye nihamasisha kuwa daktari ni mjomba wangu aitwaye Dk. Floridus Ndokoye.

Nimekuwa nikimuona na amekuwa akinihamasisha kuwa daktari. Lakini vilevile kunakuwa na ile sauti ya ndani ikiniambia juu ya wagonjwa, watu wanapata shida za kiafya na walau unaona ufanye kitu. Hivyo niliamua kuchukua mchepuo wa sayansi, yaani Fizikia, Kemia na Bailojia (PCB).

Hata hivyo safari hiyo haikuwa nyepesi kwa sababu ilifika kipindi nikatamani kuhamia PCM (Fizikia, Kemia na Hisabati). Nashukuru Mungu nilipata walezi wazuri darasani shuleni, walimu wakanitia nguvu.

Nashukuru mpaka leo niko hapa mwaka wa nne, nasomea udaktari na Mungu akipenda kama inavyoonekana hapa, tunatarajia tuje kuwa watunga sera katika sekta yetu ya afya.

SWALI: Sehemu kubwa ya wananchi wa Tanzania, takribani asilimia 70 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 wanaishi vijijini. Hata hivyo madaktari wengi hawapendi kufanyia kazi vijijini, unalizungumziaje suala hili?

JIBU: Eeee hapa swali la kwanza inabidi tujiulize ni kwa nini hawa madakatari hawapendi kwenda vijijini? Kwa sababu ukishajua ni kwa nini hawapendi kwenda huko unaweza ukatoa solution (suluhisho).

Kama nilivyosema awali bado katika vijiji vyetu kuna hali duni sana ya kimaisha. Hivyo hatua ya kwanza inayotakiwa kufanyika ni kuhakikisha tunapeleka miundombinu ya kutosha katika vijiji vyetu.

SWALI: Kwa nini unasema hivyo?

JIBU: Kwa sababu huyu daktari mbali na kuwa kazi hii ni ya wito, bado na yeye anatamani kuwa na maisha mazuri, anatamani kukaa sehemu yenye barabara nzuri, sehemu yenye vifaa ili anapotaka kusaidia watu aweze kufanya hivyo. Anatamani kukaa sehemu yenye umeme, maji na kadhalika.

Kwa hiyo hatua ya kwanza kabisa ukitaka kushawishi watu kwenda vijijini, ni ya kuhakikisha kama serikali kuna mpango wa kuendeleza vijiji kuwa katika hali nzuri ya kimaisha ya miundombinu yenye mahitaji yote yanayotakiwa.

Hivyo, ninaamini hiyo ndiyo muhimu na tukiwa na hivi vyote sidhani kama kuna mtu atakwepa kwenda vijijini.

Binafsi napenda sana kuishi vijijini kwa sababu maisha ya kule siyo ya gharama kama ilivyo mjini na ukianzisha programu zako huko ni rahisi kufanikiwa kama mtu aliye mjini.

SWALI: Sasa shida hapo ni nini?

JIBU: Ukiangalia hapo shida ni kwamba huyu anakaa mjini na anacholipwa ni kilekile sawa na huyu anayekaa kijijini.

Hivyo mtu anajiuliza kwa nini aende kijijini kwenye maisha magumu wakati mshahara ni uleule na stahiki ni zilezile? Ninaamini tukiendeleza vituo vya afya vijijini, vikawa katika hali nzuri na kumtengenezea mazingira mazuri daktari, mimi ninaamini huko kunaweza kukashawishi wataalamu wetu wa afya kukaa huko, kuliko tukibaki kulalamika kwa nini hawaendi vijijini. Ninaamini kama kuna maji, kama kuna miundombinu mizuri, barabara, umeme, idadi ya wale wasiopenda vijijini itapungua kwa kiasi kikubwa.

SWALI: Tuongelee urais wako… mipango yako ni nini, ajenda yako ni nini na unataka utakapokabidhi madaraka baada ya urais wako, MUHAS ikukumbuke kwa lipi?

JIBU: Eee unapoongelea nitaifanyia nini MUHAS, ni suala ambalo limegawanyika katika mambo mawili. Jambo la kwanza ni majukumu ya lazima ambapo kama serikali lazima iyatimize mfano kusimamia taaluma ya wanafunzi na changamoto ya mikopo. Watu wanakosa mikopo na changamoto nyingine za maisha kama makazi ambayo ni changamoto kubwa sana. Ninawasihi wadau kama wananisikiliza, kuna changamoto kubwa ya makazi hapa. Kwa hiyo kama kuna namna yoyote ambayo wadau tunaweza kushirikiana tufanye hivyo. Kwa mfano wenye nyumba maeneo ya karibu ambao tunaweza tukazifanya zikawa sehemu ya kuishi wanafunzi wetu, tutafurahi sana kuwapata.

SWALI: Changamoto nyingine?

JIBU: Vilevile tuna changamoto kubwa ya wanafunzi wanaokosa mikopo ambayo kama serikali mwaka huu tumeahidi tutafanya kila namna kusaidia.

Lakini pia kama kuna wadau wananisikiliza wanaweza wakafadhili wanafunzi wetu. Lingine ni la majukumu ya msingi kabisa ambayo hata katiba yetu inatuelekeza tufanye nini.

Kwamba lazima tusimamia wanafunzi na kuhakikisha mahitaji na haki zao hazidhulumiwi na kwamba kuhakikisha taaluma inaenda kama inavyokusudiwa.

SWALI: Kuna lingine katika hili?

JIBU: Ndiyo kwa maana kuwa ninapenda kuhakikisha kwamba tunatengeneza viongozi wa baadaye na hiyo ni goal (lengo) yangu kubwa.

Tunatengeneza kwa namna gani, cha kwanza nataka kutengeneza uongozi wa mfano ambao utakuwa wa maadili.

Uongozi ambao utakuwa unagusa maisha ya watu, wa haki na kila mtu afurahie na mwisho wa siku tuhakikishe kwamba hawa wanafunzi wetu tukiachana na majukumu yetu ya msingi, tuwatafutie fursa nje na pia tukitangaze chuo chetu kwa kutumia vipaji mbalimbali ambavyo wanafunzi wetu wanavyo.

Kuna watu ambao wanafanya innovations (ubunifu), wana idea (mawazo) nzuri tu.

Kwa mfano tulifanya symposium ya artificial intelligence in health care (Mkutano wa ubunifu kwenye huduma za afya) ulipokelewa vizuri sana na wadau.

Kwa hiyo lengo pia ni kuhakikisha tunawatafutia fursa wanafunzi wetu, kwamba ukiachana na taaluma, Universities ni universal (a-kiulimwengu) hivyo lazima wawe na kitu cha ziada.

Kwa hiyo kuwajengea uwezo wanafunzi wetu wa kupata vitu extra (vya ziada), waonyeshe vipaji vyao, uwezo wao katika kutatua matatizo mbalimbali katika nchi yetu. Kwa hiyo tunataka wanafunzi wetu wawe sehemu ya kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya afya nchini.

SWALI: Watu wangependa kumfahamu huyu Rais wa serikali mpya ya MUHAS, ni nani, ametokea wapi hadi hapa alipo, unaweza kutupa historia yako?

JIBU: Ahsante sana, kwa majina naitwa Constatine Alex Ntanguligwa.Nimezaliwa Dar es salaam, Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo na nimelelewa na wazazi wangu ambao mpaka sasa bado wako hai, mama ni Mwalimu, baba ni Mhandisi.

Elimu yangu ya msingi nimeipata hapa hapa Dar es Salaam, Shule ya Msingi Mwenge, baadaye nikasoma Shule ya Msingi Canossa kidogo na mwisho St. Marys-Mbezi.

Nilibahatika kwenda seminari kipindi ambacho nilikuwa natamani kuwa Padre. Nilianza kidato cha kwanza pale Visiga.

Safari yangu ya uongozi kwa kweli ilianzia toka nikiwa shule ya msingi, madarasa yote ambayo nimesoma nilikuwa kiranja wa darasa, hata nilipofika sekondari, kidato cha kwanza nilikuwa kiranja wa darasa.

Kidato cha pili nikawa kiongozi wa maktaba na nilipofika kidato cha tatu nikawa kaka mkuu msaidizi.

Nilienda kidato cha tano na sita shule ya sekondari Msolwa, nilikaa Ilboru kidogo, lakini nilirudi tena Msolwa na kule nilikuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi.

Hatimaye ndoto yangu ya muda mrefu ya kuwa daktari niliianza mwaka 2015, nilipojiunga na MUHAS. Kama kawaida ndoto ile ya uongozi ilianza kuchipua tangu mapema sana.

SWALI: Kivipi?

JIBU: Nilipofika hapa nilikuwa mwakilishi wa darasa mwaka wa kwanza na mwaka wa pili niliingia kwenye Bunge nikiwakilisha wanafunzi.

Aidha, nikateuliwa kuwa naibu waziri mwaka huo na nikafanya kazi yangu kwa kadri Mungu alivyonijalia. Mwaka huo huo niliamua kugombea umakamu wa rais ingawa kura hazikutosha lakini haikunikatisha tamaa.

Kuingia mwaka wa tatu nilipumzika siasa kidogo, lakini wanaMUHAS wakaniamini nikawaomba kuwa mwenyekiti wa kitivo cha udaktari ambacho kina wanafunzi wa udaktari, maabara na mionzitiba na nikawa mwenyekiti wa wanafunzi wote hao.

Mwaka huu wa nne wa udaktari nimeamua kugombea urais na ninashukuru wanaMUHAS wamenidhamini kwa kishindo kabisa, kwani kihistoria haijaweza kutokea kwa rais kushinda kwa asilimia 76.

Nashukuru Mungu kwa sehemu zote ambazo nimekuwa kiongozi watu wamekuwa wakipenda uongozi wangu, kwani nimekuwa nikigusa maisha ya watu. Lakini niseme tu kama umezaliwa kuwa kiongozi utaona ile mbegu inamea.

SWALI: Kwa nini unasema hivyo?

JIBU: Nasema hivyo kwamba pamoja na changamoto zote nilizopitia katika safari ya uongozi leo hii tuko hapa.

Natamani baadaye nimalize udaktari wangu, nijiendeleze katika taaluma kwa sababu ninaamini uongozi ni kama kipaji, ni sawa na mchezaji mpira, unaweza kuwa daktari na ukawa mchezaji mpira mzuri.

Kwa hiyo vilevile nina mpango wa kujiendeleza katika taaluma yangu ya udaktari na hata kuwa daktari bingwa na kwa upande wa pili kujiendeleza katika fani ya uongozi kwa kufanya kozi mbalimbali za uongozi na pengine Mungu akipenda kuingia katika siasa za nchi.

SWALI: Tanzania imejielekeza katika uchumi wa viwanda, ikilenga kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025, unazungumziaje hili katika jicho la afya?

JIBU: Tunapoongelea Tanzania ya viwanda katika sekta ya afya, tunaongelea mambo mengi.

Jambo la kwanza kutoka kwenye neno lenyewe la Tanzania ya viwanda, ifike wakati sasa kwamba upungufu wa vifaa na baadhi ya vitu katika hospitali zetu, unaotokana na sisi kutegemea sana wenzetu kuliko sisi wenyewe ukome. Tuna viwanda hapa vinatengeneza dawa, vingeendelezwa na pengine kuletwa vingine.

Kwa mfano issue kama drip na water injection, sidhani kama kuna haja sana ya sisi kuagiza kutoka nje, kwani tuna maji ya kutosha. Tunaweza kutengeneza vifaa hivi, vitu basic kabisa ambavyo vinahitajika katika hospitali zetu.

SWALI: Una maana gani?

JIBU: Ninaamini kabisa kama nchi tukijipanga tukawa tunatengeneza wenyewe kama nchi na kupunguza gharama ya kutengeneza hivi vifaa kwa sababu kama vinatengenezwa hapa itakuwa ni vyema zaidi kwa sababu vitapatikana kwa wingi kwa kutengenezwa hapa.

Lakini kwenye sekta ya afya, tuna vitu artificial intelligence, yaani uendelezaji wa kiteknolojia. Kuna vijana wengi wenye idea nzuri na kubwa za kutatua matatizo katika sekta ya afya kwa kutumia teknolojia.

Naamini tunapoongelea Tanzania ya viwanda, tunaongelea vijana wa namna hiyo kwani wapo vijana hapa wana idea nzuri za kuleta solution katika sekta yetu ya afya.

Kwa mfano kuna kampuni zimeanzishwa na wanafunzi hapa, moja inarahisisha kugawa dawa mbalimbali.

Lakini kuna idea za wanafunzi wetu kama daktari mkononi, ambayo inatoa huduma ya afya kwa wananchi kwa kupitia mitandao ya simu, mitandao ya kijamii na vitu kama hivyo.

Kama nchi tunaweza kuwekeza katika eneo hilo pia na kwamba sasa tunaelekea katika teknolojia ya viwanda, tukawekeza katika eneo kama hili ili kutatua changamoto mbalimbali za wananchi wetu.

Naamini kwamba tunapoelekea kuwa nchi ya kipato cha kati 2025, tutaweza kuboresha walau miundombinu katika hospitali zetu, kuweka vituo vya afya na mazingira mazuri ya kufanya kazi kwa madaktari wetu na wataalamu wetu wa afya.

Ninaamini kama nia ya dhati ya Rais wetu John Magufuli ikitimia, tutakuwa tumepiga hatua kubwa sana katika kuendeleza sekta ya afya kwenye Tanzania ya viwanda.

Habari Kubwa