Mjadala mkali usio na marekebisho yaliyotarajiwa

22Jun 2016
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Mjadala mkali usio na marekebisho yaliyotarajiwa

KATIKA kile ambacho hakikutarajiwa kwa wabunge wa Chama cha Mapinduzi ni kukubali kwa kura ya ndiyo na makofi mengi kupitisha bajeti ya mwaka 2016/17 bila marekebisho waliyotaka,

Ambayo wakati wa mjalada walikuwa wakali kiasi cha kutishia kushika Shilingi kwenye mshahara wa Waziri wa Fedha na Mipango.

Maeneo yote yaliyopigiwa kelele kwa kiasi kikubwa kwa takribani siku saba hayakuketa mabadiliko yoyote zaidi serikali imerudi na bajeti ile ile iliyowasilishwa huku ikifafanua namna ambavyo itakwenda kuitekeleza.

Wabunge 251 waliokuwepo bungeni juzi walipiga kura ya ndiyo, licha ya baadhi yao kutishia kutoa shilingi iwapo serikali haijafanya marekebisho, lakini bado msimamo wao ulibadilika na kuunga mkono bila marekebisho waliyotaka.

Akijumuisha bajeti hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mipango, anasema ni lazima kila Mtanzania akubali kuvuja jasho kwa kulipa kodi ili kupiga hatua ya kimaendeleo huku akieleza rais amekubali kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo chake kwa kuwa anatambua wajibu wa kila Mtanzania kulipa kodi.

Maeneo ambayo yalitawala mjadala wa bajeti mwaka huu ni kukata kodi ya asilimia tano kwenye kiinua mgongo cha wabunge, ambacho kilipingwa vikali na wabunge wote isipokuwa Mbunge wa Mtera, Livingston Lisinde, ambaye alitaka kuwapo kwa mazungumzo baina ya wabunge wa CCM na serikali.

Wabunge wengine walienda mbalimbali na kumkaribisha jimboni Waziri huyo ili aone utamu wa jimbo kwa kuwa wamegeuzwa kama mashine za kutolea fedha (ATM), na kwa siku wanapokea simu zaidi ya 30 za kuomba fedha kwa ajili ya huduma za kijamii za wananchi wao.

Baadhi wanasema serikali imegusa pabaya kwa kuwa tayati wanakatwa kodi ya Sh milioni 1.3 kila mwezi kwenye mishahara yao na baada ya miaka mitano wanakuwa wamelipa Sh. milioni 50.

Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, anasema serikali imegusa pabaya huku akiomba kuachana na mpango huo kwa kuwa fedha wanayolipwa wabunge baada ya miaka mitano ni sawa na posho na huwaandalia mazingira mazuri ya kurudi jimboni.

"Unataka kuondoa msamaha, nataka nikuhakikishie kuanzia utawala wa Benjamini Mkapa, wabunge na watumishi wengine waliomba mafao yao yasikatwe kodi kwa sababu wamefanyakazi miaka 30 au 40 wanakatwa fedha wengine wanakufa kesho yake," alisema na kuongeza:

"...matokeo yake unatuletea kufuta za wabjunge, nyie wenyewe ni mashahidi wakati wa Spika Anne Makinda, alisema amechoka kupokea wabunge wastaafu wenye matatizo wanamuomba hela wamekuwa ombaomba, maslaji yetu yanakatwa kodi alafu mafao yetu wanayakatwa tena, hatukubali,"alisisitiza.

Anasema "Mnataka turudi nyumbani halafu muanze kutucheka, lazima wabunge tulinde maslahi yetu, hatutakubali fedha ambazo kila mwezi zinakatwa kodi ya mashahara halafu baada ya kutoka hapa unakatwa tena, Wabunge tusikubali hili," anasema huku akishangiliwa na wabunge.

Lugola anasema mshahara wa wabunge ni mdogo kuliko wa Waziri, lakini amekimbilia kukata kodi kwenye mshahara wao na kamba kwenye majimbo yao wamegeuzwa serikali na ATM kwa kuwa wanatumia fedha zao kutekeleza shughuli maendeleo na kijamii.

"Mheshimiwa Mpango unataka kucheza na maslahi ya Mbunge, wewe (Waziri), ulipo jimbo lako ni mheshimiwa rais, sisi hapa ni mifuko yetu. Tumekuwa tukiomba fedha halmashauri kutekeleza miradi wanasema kazi ya Mbunge, alafu leo hata hicho kidogo mnataka kukikata," alisisitiza.

Lugola alisema "Fedha zetu ni kidogo sana halafu unazikwangua, sijui ikifika mwakani utakuja na agenda gani, hili halitakubalika,” anasema.

Mbunge wa Sikonge (CCM), Joseph Kakunda, anasema hakukua na ulazima wa kuleta suala la kodi kwenye kiinua mgongo cha wabunge kwa kuwa halitatoa fedha za kutekeleza maendeleo kwenye bajeti hii.

Anasema mhimuli wa Bunge unajitegemea na haipaswi kuingiliwa katika suala hilo na kwamba maslahi ya wabunge ni madogo hivyo hayapaswi kukatwa kodi.

Mbunge wa Ulanga Mashariki, Goodluck Mlinga anasema "Waziri wa Mipango naona umeamua utupange wabunge kwa kukata fedha zetu, ukiendelea hivi mwakani utakuja na mapendekezo tuondoe magari ya serikali tutumie pikipiki na baiskeli, na mwaka unaofuata utakuja na pendekezo la tupangishe Ikulu halafu rais akaishi Mbagala.”

Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby, anasema suala la kukata kodi kiinua mgongo cha wabunge halikubaliki ni vyema serikali ikaangalia vyanzo vingine.

Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia: "Kwenye serikali hii inaelekea watu wanafanyakazi kwa woga sana kwa kila anayetaka kufanya maamuzi anamsingizi rais, kila mmoja afanye kazi zake aache woga...unapogusa fedha zetu ambazi zinatujengea msingi wa kugombea na kutekeleza mahitaji ya wananchi wengine," alibainisha.

CAG

Wakitetea hoja ya CAG wabunge wamesema bila kumuongezea Bajeti CAG, jitihada za Rais Dk. John Magufuli, kutumbua majipu zitakwisha baada ya mwaka huu kwa kuwa majipu yote aliyotumbua yalitokana na kazi iliyofanywa na CAG.

"Juhudi za rais kutumbua majipu hatazifikisha mwakani endapo atabaki peke yake mtumbua majipu wakati mtambua na mbaini majipu ambaye ni CAG ataendelea kuwa na Sh. bilioni 32,” anasema na kuongeza:

"CAG ndiye anayekagua miradi halafu anapewa fedha kidogo huko ndiyo anagundua ufisadi. Kitendo cha kumpa fedha kidogo kudidimiza ofisi hii, nakwambia utumbuaji majipu utaishia mwaka huu, rais hatakuwa na majipu ya kutumbua tena walamvijiou upele kama bajeti yake haitaongezwa," anasitiza.

Mbunge wa Sumbawanga mjini, Aeshi Hilal, anasema fedha alizopewa CAG hazionyeshi dhamira ya serikali kumaliza mafisadi nchini kwani amepewa fedha za mishahara na kuendesha ofisi na siyo kufuatilia fedha za miradi.

Hilal ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), anasema fedha za miradi ya maendeleo ya Sh. trilioni 11.82, ambayo imeongezeka kutoka Sh. trilioni 5.92, mwaka 2015/16, haziwezi kusimamiwa na ofisi ambayo serikali imeinyima fedha.

Hoja nyingine zilizoshika kasi ni Wabunge na kamati ya bajeti kutaka ongezeko la Sh. 50 katika kila lita ya mafuta ili zielekezwe kwenye huduma ya maji vijijini, hoja ambayo ilikataliwa na serikali kwa madai kuwa wananchi wanapaswa kufurahia maisha kwa kipindi ambacho bei ya mafuta iko chini.

Nyingine ni ongezeko la kodi ya mitumba kutoka dola za marekani 0.2 hadi 0.4 kwa kilo, huku kukiwa na lengo la kupiga marufuku biashara ya mitumba nchini, lakini serikali imekataa kwa kueleza kuwa inaimarisha viwanda vya nguo nchini.

Eneo jingine ongezeko la usajili na uhamisho wa umiliki wa pikipiki kutoka sh 45,000 hadi 95,000, ambayo serikali imegoma kuliondoa, pamoja na ile ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye Huduma za Utalii.

Eneo jingine ni kuondoa kodi ya mazao na kuweka kwenye mazao yaliyosindikwa, ambayo wabunge walipinga kuwa itauwa kazi za wajasiriamali wadogo ambao wanataka kuwekeza kwenye usindikaji, lakini serikali imebaki na msimamo wake.

Pia, wabunge hao walipinga hatua ya serikali kutoza kodi kwenye miamalamya simu bila kuwalinda wananchi, kwa kuwa maouni hizo hazitakubali kupata hasara bali zitalinda faida yake kwa kuwaongezea gharama wananchi.

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, aliwasilisha mrekebishonsaba kwneye sheria ya fedha iliyopitishwa juzi kwa hati ya dharura, lakini hakuna lililochukuliwa na serikali bali sheria ilipita kwa kadri serikali ilivyoiandaa.

Bunge la mwaka huu ni tofauti na mengine ambayo kelele za wabunge zinapokuwa nyingi hukubali kufanya marekebisho ya baadhi ya malendekezo yao, mathalani bajeti ya mwaka jana waliongeza pensheni ya wazee kutoka sh 100,000 hadi 150,000 kwa mwezi.

Habari Kubwa