Mjamzito, mnyonyeshaji na safari inayowatetea kwa mlo, afya mwili

06Aug 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Mjamzito, mnyonyeshaji na safari inayowatetea kwa mlo, afya mwili

KILA Agosti Mosi hadi 7 ya mwaka, Tanzania huungana na nchi nyingine duniani, kuadhimisha wiki ya unyonyeshaji, inayolenga kukumbusha jamii vitu muhimu katika unyonyeshaji maziwa ya mama.

Maziwa ya mama yanatajwa kitaalamu kuwa ni muhimu kwa afya na makuzi ya mtoto, licha ya umuhimu huo, bado kunatajwa kasoro katika unyonyeshaji, ikiwamo kuzingatia lishe bora.

Hata hivyo, suala la ulaji vyakula bora kwa mjamzito na mama anayenyonyesha imekuwa tatizo kwa jamii, hali inayowasababisha watoto kukosa virutubisho muhimu kwenye ukuaji na kinga asilia dhidi ya maradhi.

Takwimu za mwaka wa fedha 2015/2016 (TDHS) na zingine 2018 (TNNS) zinaonyesha asilimia 43 ya watoto nchini wanayonyeshwa hadi kufikia umri miaka miwili.

Takwimu zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), zinaonyesha takribani watoto milioni 7.6 duniani hawanyonyeshwi kila mwaka.

OFISA LISHE

Ofisa na Mratibu wa Lishe kwa Kinamama, Watoto na Vijana kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Tufingene Malambugi, anasema mjamzito anayenyonyesha anashauriwa kupewa vyakula mchanganyiko vinavyomtosha.

Anashauri umuhimu wa jamii kutambua na kuzingatia lishe bora kwa mjamzito, akifafanua: “Hii itamuwezesha mama kujenga afya bora katika mwili wake na mtoto, kutoa maziwa ya kutosha kwa ajili ya mtoto wake pia kuweza kuhudumia familia yake.”

Malambugi anasema mjamzito na anyonyeshae, wote wanapaswa kuzingatia milo mitatu inayojitosheleza kila siku, pia vitafunwa au milo midogo muda wa kati mara mbili kwa siku.

Hata hivyo, anafafanua kwa mama anayenyonyesha, anahitaji milo mingi midogo na akifafanua: “Mama ale vyakula vya mchanganyiko vinavyopatikana kwa urahisi. Mama ale mboga za majani na matunda kwenye kila mlo, matunda yenye rangi ya njano na mboga za majani yana virutubisho zaidi.”

Malambugi anashauri mlo mwingine unaopaswa kuepukwa iwezekanavyo, ni kunywa chai au kahawa na milo inayofanana nayo, lengo ni kuzuia kufyonzwa mwilini madini ya chuma, hali inayochangia upungufu wa damu.

“Ni vyema kunywa chai au kahawa saa moja kabla au moja baada ya kula, kunywa maji yaliyochemshwa ya kutosha kila siku angalau (glasi nane au lita moja na nusu), mama apate muda wa kupumzika angalau dakika 30 kila siku wakati wa mchana.

“Mama aepuke kunywa pombe na kuvuta sigara wakati wa ujauzito na wakati wa kunyonyesha, mama mjamzito aepuke kula vitu ambavyo si chakula kama vile udongo, mkaa au chaki ambavyo vinaweza kuleta madhara katika mwili,” anaelimisha.

“Mama anayenyonyesha, aepuke kupika mboga za majani kwa muda mrefu ili kuzuia upotevu wa virutubishi,” anaendelea
Malambugi anakumhusha haja ya kila wakati wa kuandaa chakula kuendane na haja ya kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka.

“Weka vyombo na sehemu ya kutayarishia chakula katika hali ya usafi, pika nyama, samaki na mayai mpaka viive kabisa ili kuepuka maambukizi.

“Osha mboga mboga kabla ya kuzikata, kisha zipikwe mara moja kwa muda mfupi na kuliwa mara moja kwa muda mfupi, ili kupata virutubishi. Osha vizuri matunda na mboga mboga zinazoliwa,”anasema.

UPANGAJI MLO

Malambugi anasema mjamzito au anayenyonyesha anapaswa kupata milo mitatu kamili na vitafunwa walau mara mbili kwa siku, zikiwamo viazi, mihogo na ndizi mbichi na magimbi.

Pia, anaorodhesha nafaka kama vile mahindi, mtama, mchele, ulezi na ngano, sambamba na nyama, maharage, njegere, karanga, mbaazi, fiwi na dengu.

“Vyenye asili ya wanyama ni kama vile nyama za aina zote, mayai, maziwa, samaki, dagaa, ndege aina ya kuku, bata, njiwa na wadudu wanaoliwa kama vile senene na kumbikumbi. Vyakula hivi vina utomwili au protini kwa wingi kwa ajili ya kujenga mwili,”anasema.

Mtaalamu huyo anataja matunda kama embe, ndizi mbivu, papai, pera, chungwa, ubuyu, nanasi, pesheni parachichi na zambarau, ubuyu, ukwaju na matunda ya asili, yana vitamin inayolinda mwili na kusaidia ufanyaji wake kazi katika mifumo mbalimbali.

Pia, anataja mboga za majani kama vile mchicha, majani ya maboga, kisamvu, matembele, bamia yana madini na Vitamini yanayosaidia kulinda mwili usishambuliwe na magonjwa, ikiasadiana na lishe kama karoti, nyanya chungu, matango, mlenda, boga na biringanya.

Mengine katika orodha hiyo inajumuisha sukari na mafuta, ambayo yanapoongezwa kwenye mboga zingine huboresha ufyonzaji wa baadhi ya vitamin, hali kadhalika nguvu mwilini.

FAIDA ZILIZOPO

Mlo wa mafuta yanatajwa kuongeza uzito usiopungua kilo 12 kwa mlaji wakati wa ujauzito kila mwezi, inazuia upungufu wa damu na kuboresha ukuaji mtoto kimwili na kiakili. Anafafanua: “Mahitaji ya chakula na virutubishi ni makubwa mama anaponyonyesha kuliko wakati wa ujauzito.”

Lishe bora, pia ina manufaa ya kupunguza uwezekano wa kupata mtoto mwenye uzito pungufu, kujifungua kabla ya wakati au kupata mtoto mfu.

“Mahitaji ya chakula na virutubishi huongezeka katika kipindi cha ujauzito, kwa ajili ya mtoto aliye tumboni na mama mwenyewe. Lishe bora wakati wa ujauzito husaidia ukuaji mzuri wa mtoto aliye tumboni na kuutayarisha mwili wa mama kwa ajili ya kunyonyesha,” anasema.

Maatalamu huyo anainisha upungufu wa damu, unavyochangia kupunguza uwezekano wa mama kuzaa mtoto mwenye uzito pungufu na akajifungua kabla ya wakati au hata kupata mtoto mfu, haki inapokuwa mbaya zaidi.

KAULI YA WAHUSIKA

Mkazi wa Chinyambwa, Sara Mazengo, anasema akina mama wengi hasa wajawazito na wanaonyonyesha wamekuwa wakila vitu ambavyo havina virutubisho kwa watoto.

Anashauri wataalamu lishe kutoa elimu ya kila mara, hali itakayochangia kinamama kunyonyesha watoto kwa kufuata maelekezo ya wataalam kupitia maziwa ya mama na si kuwapa vitu vingine.

“Unajua kinachosababisha mama anampa mtoto uji au maziwa ya ng’ombe kabla ya kutimiza miezi sita ni kutokana na kwamba anaona mtoto hashibi kutokana na wepesi wa maziwa na huu unatokana na vyakula ambavyo anakula. Sasa hii elimu ya vyakula ni muhimu, maana ukuaji mtoto unachangiwa na vitu vingi,” anasema.

Habari Kubwa