Mkaa Endelevu unavyoibadili Kilosa kutoka ufyekaji msitu

07Dec 2017
Christina Haule
Nipashe
Mkaa Endelevu unavyoibadili Kilosa kutoka ufyekaji msitu
  • Halmashauri Moro yavutiwa, yafuata nyayo
  • Mazingira, uchumi wa jamii zanufaika pamoja

BAADA ya kuletwa mradi wa kuchoma mkaa kwa nia endelevu, kijijini Kitundueta katika Kata ya Mhenda wilayani Kilosa, mkoa wa Morogoro, sasa wanufaika wana ushauri kwa serikali iendelee kuwaunga mkono kwa mengi, katika mradi huo unaotarajiwa kumalizika mwaka 2019, baada ya kuanzishwa rasmi mwaka 2012

Mwananchi akiwa msituni akichoma mkaa

Pia, wanataka mradi huo utanuliwe kwa kuhusisha vijiji vingi zaidi, badala ya vichache vya mfano, ili ufike katika mtadao mpana zaidi.

Ni juhudi zinazoendeshwa na Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania, kwa ubia na wadai wengine wane wanaotetea sekta ya misitu.

Hao ni Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita), Shirika la Kuendeleza Nishati Asilia na Maendeleo (TaTEDO), na wafadhili wa Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo ya Uswisi (SDC).

Mradi huo umechukua baadhi ya maeneo teule ya mfano katika wilaya za Kilosa na Morogoro Vijijini, mkoani Morogoro, kwa kuandaa maeneo maalum ya msitu yanayogawanywa na mamlaka za husika za maliasili.

Mfumo huo unaofanywa kwa mzunguko wa miezi 24, uvunaji endelevu unafanyika kwa msitu kugawanywa katika vipande maalum na kisha miti hiyo huchomwa mkaa katika mbinu ya kisasa katika kipande teule walichopewa.

Baada ya kukamilisha uvunaji walivyoelekezwa na kuchoma mkaa, wanahamia kipande kingine, chini ya uratibu wa mamlaka inayohusika na maliasili, wakati huo kitalu cha awali kikiachwa kichipue na mzunguko wake unapofika tena, unakuwa imeshakomaa.

Wilayani Kilosa

Mmoja wa wachoma mkaa hao, Kulangwa Ganda, anasifu mradi umemfanya mwanakijiji au mkata mkaa mwenye elimu ya mkaa endelevu, ajue umuhimu wa kuhifadhi mazingira, kutokana na mazao yanayopatikana kurejesha faida kijijini, tofauti na ilivyokuwa awali, mradi haujafika.

“Zamani tulikata mkaa bila ya kufuata taratibu yoyote na wakati mwingine kuvunja sheria zilizopo, tukikamatwa na mkaa wote hata ukiuzwa kijiji chetu kilikuwa hakipati faida. Lakini kwa sasa kila gunia la mkaa linalouzwa, huacha Shilingi 10,000 kwenye ofisi ya kijiji kwa ajili ya shughuli za maendeleo” anasema Ganda.

Anasema uvunaji endelevu wa mkaa umesaidia kukomesha ujangili misituni, kwani wakiwa na uongozi kamili kwenye vikundi vyao, wameweka utaratibu wa kulinda misitu na kuwakamata wavunaji holela wa mazao ya misitu na kuwafikisha kwenye ofisi ya kijiji kwa hatua za kisheria.

Taji Mfanga ni Katibu wa Kamati ya Maliasili katika Kijiji cha Kitundueta wilayani Kilosa, anaiomba serikali kuangalia uvunaji mkaa kwa njia endelevu, akikumbusha unagusa maisha ya wengi, huku wakitunza mazingira inavyostahili.

Anaiomba serikali kutambua kuwa wananchi wanaendelea kuelimika na mkaa endelevu na wameanza kujua umuhimu wa uhifadhi misitu na mazingira, hivyo ikisimamisha uchomaji mkaa ni kudidimiza maisha ya Watanzania walioanza kuinuka kupitia uvunaji mkaa endelevu.

“Sasa mkata mkaa anaheshimika, tofauti na zamani. Sababu zamani alionekana kama jangili na mharibifu wa misitu, lakini sasa tunavuna, tunalinda misitu, huku tukiendelea kuvuna kwenye vitalu vingine vilivyowekwa kisheria na kusubiri kuvuna kwenye vitalu vyetu vichipue baada ya miaka 24,” anasema Mfanga.

Ofisa Maliasili Kilosa

Mkuu wa Idara ya Ardhi Maliasili na Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Ibrahimu Ndembo, anasema Mradi wa Mkaa Endelevu umeweza kushirikiana vyema na halmashauri hiyo katika hatua mbalimbali.

Ndembo anayekiri manufaa ya mradi huo, anataja maeneo ya manufaa kuwa ni mpango wa matumizi bora ya ardhi, ikitenganisha maeneo ya vijiji, hifadhi na ufugaji naye ufugaji nyuki, kwa mujibu wa sheria zinazosimamia misitu nchini.

Anasema, sheria na sera za misitu nchini zinataka mwananchi anufaike na rasilimali za misitu yake na kwamba hiyo ndiyo nia ya mradi huo inayomfanya mwananchi anufaike na rasilimali za misitu, ili aone umuhimu wa kutunza mazingira.

Ndembo anafafanua kuna vijiji vitano vinavyotekeleza mradi wa mkaa endelevu, pia halmashauri hiyo katika bajeti yake ya mwaka huu, imetenga vijiji vingine vitano viingizwe kwenye mradi na mpango wa matumizi bora ya ardhi na elimu ya mkaa endelevu.

“Kwa bajeti ya mwaka 2017/18, wilaya imetenga kiasi cha Sh. milioni 45, ili kuwezesha vijiji hivyo vitano na kwamba, kila kijiji kitatumia Sh. millioni l 9 kwa mpango wa matumizi bora aya ardhi” anasema Ndembo.

Hata hivyo amesisitiza wananchi kutunza misitu ili waweze kunufaika nayo moja kwa moja na kutimiza maana ya Sera ya misitu ya mwaka 1998.

Ndembo anaainisha dira ya halmashauri hiyo ni kuhakikisha vijiji 60 kati ya 130 vilivyopo katika wilaya hiyo, vinaingia kwenye mradi huo, ili kulinda na kuboresha mazingira yaliyopo.

Morogoro Vijijini

Baada ya kupata somo la kinachofanyika Kilosa kwa manufaa makubwa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Kibena Kingo, anakiri kuelekeza uzalendo mkubwa katika ushiriki wa miradi ya mkaa endelevu.

 

Huku akikiri kuwa na ushuhuda unaojitosheleza, Mama Kibena anasema, Mradi wa Mkaa Endelevu, umeonyesha njia sahihi ya kufanya ushiriki kamilifu wa wananchi katika utunzaji misitu, hivyo misitu inakuwa salama muda wote.

Anasema, ufuatiliaji wake binafsi kuhusu mradi huo ulioanzia wilayani Kilosa, ameona manufaa ya kupewa kipaumbele, kama njia ya kutekeleza Sera ya Misitu ya Mwaka 1998, inayowataka wananchi kushiriki kikamilifu kuhifadhi misitu, jambo linalotekelezwa na mradi huo Morogoro.

Katika Kijiji cha Mlilingwa kwenye halamashauri hiyo kunakotekelezwa mradi, Mwenyekiti Kijiji, Salum Ali anasema, wakati wakiwa katika hatua ya kujifunza kuhusu mradi wa mkaa endelevu, tayari wameshuhudia manufaa muhimu ya kimazingira, huku akisistiza iwe na elimu endelevu.

Hata hivyo, kuna malalamiko kutoka kwa Mwenyekiti Ali, akilalamika bado maeneo makubwa wastani wa hekta 11,000 ya wilaya hiyo yamechukuliwa na wawekezaji ambao hawayaendelezi,.

Hata hivyo, anasema baadhi ya maeneo hayo yamesharejeshwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, katika ziara yake hivi karibuni.

Katibu wa Wachoma Mkaa kijijini Mlilingwa, Ramadhani Mnenvu, anasema miaka mingi imepita tangu wawekezaji walipochukua ardhi hiyo, bila ya kuiendeleza.

Mwenyekiti Ali anasema tayari wameshapata maelekezo ya serikali kwamba, wanaweza kuirejesha katika himaya yao kwa nia ya kuiomba.

Ofisa Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania, Charles Leonard anasema licha ya nishati ya mkaa kudaiwa inaharibu mazingira sambamba na kuteketeza maliasili ya misitu, ikitumika vizuri ina manufaa makubwa katika maisha binafsi na miradi ya maendeleo kitaifa.

Anasema, takribani hekta 500,000 ya nishati hiyo kama ikitumika vizuri kwa kuwa na uvunaji endelevu, mkaa inaweza kusaidia kuingiza taifa kiasi kikubwa cha fedha.

Analaumu upotevu wa hekta hizo, umesababishwa na kutokuwepo sera madhubuti ya kusimamia nishati ya mkaa  na kwamba nishati ikitumika vizuri, wananchi wengi hususan wa kipato cha chini watanufaika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mjumita, Rehema Njaidi, anasema licha ya kuwa na sera isiyo madhubuti ya kusimamia misitu nchini, bado kuna njia sahihi ya mkaa endelevu kuwafikia wananchi, itakayotunza misitu.

 

 

Habari Kubwa