Mkakati mpya kulinda wanyama waibuliwa, ni kuwapima DNA

27Jan 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Mkakati mpya kulinda wanyama waibuliwa, ni kuwapima DNA

WANYAMAPORI ndani ya hifadhi wapo hatarini kuangamia kutokana vitisho mbalimbali kama kuongezeka kwa mahitaji ya makazi na uzalishaji mijini na vijijini, pia kukosa shoroba (njia) za kupita ili kufikia maeneo na kuchangamana na kuzaliana.

 

Ili kukabiliana na hatari hiyo serikali inakusudia kuwa na maabara ya upimaji na uhifadhi wa nasaba (DNA) za wanyamapori  ili kuwalinda na kuwahifadhi wanufaishe vizazi vya sasa na vijavo.

Ni kazi ambayo kwa  mara ya kwanza  itafanywa na  Maabara ya  Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA). Taasisi hiyo inatarajia kuanza kutoa huduma za kupima vinasaba vya wanyama, kwa  lengo la kuwatambua na kuwahifadhi wasiangamizwe.

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Fidelice Mafumiko, anasema na kueleza kuwa ni mafanikio yanayopatikana katika kipindi cha miaka mitatu ya uboreshaji wa huduma za mamlaka hiyo zinazojiri katika uongozi wa Rais John Magufuli.

VINASABA VYA WANYAMA

Meneja wa GCLA Kanda ya Kaskazini ambayo inahudumia mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga, Christopher Anyango, anasema akizungumzia mafanikio ya mamlaka wakati alipotembelewa na maofisa mawasiliano wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, anasema mpango huo wa miaka mitatu utaanza kutekelezwa hivi karibuni.

Anasema huduma hiyo ya kupima nasaba za wanyama itaanza baada ya kukamilika kwa ukarabati wa jengo jipya la GCLA mkoani Arusha unaogharimu Sh.milioni 950.

Anaeleza kuwa lengo ni kufungua maabara kubwa ya vinasaba vya wanyama kwenye jengo hilo ili kusaidia kufanya uchunguzi mbalimbali wa vinasaba vya wanyama itakapokuwa inahitajika badala ya kupeleka kwenye maabara za nje  ya nchi.

“Kufungua maabara kubwa ya vinasaba vya wanyama kwenye jengo hili linalokarabatiwa kutasaidia kufanya uchunguzi mbalimbali za vinasaba vya wanyama itakapokuwa inahitajika badala ya kupeleka kwenye maabara za nje ya nchini. Ikizingatiwa kuwa Kanda ya Kaskazini inashughulika sana na masuala ya utalii hasa wanyama pori," anasema Anyango.

Anasema mbali na huduma hiyo, pia maabara hiyo itafanya uchunguzi wa sampuli mbalimbali zinazofanyika katika maabara ya GCLA makao makuu jijini Dar es Salaam.

Anataja huduma hizo ni upimaji wa sayansi jinai, sumu au toksikolojia, chakula, dawa, mazingira na viumbe wadogo -mikrobiolojia.

“Tunaishukuru serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Afya kwa kutenga  bajeti ya Sh. milioni 950 kwa mwaka wa fedha wa 2018/19 kukamilisha jengo la maabara ya Kanda ya Kaskazini lililokuwa limesimama kwa muda mrefu,” anasema Anyango..

Anaeleza kuwa lengo ni kusogeza huduma za kimaabara karibu na wananchi ambazo kwa sasa zinafanyika kwenye Kanda ya Ziwa mkoani Mwanza au jijini Dar es Salaam ni kuhakikisha wananchi wanaotakiwa kupata huduma wanapata.

MAFANIKIO

Aidha, Anyango anasema kuongeza usajili wa  kampuni zinazotumia kemikali kutoka 100 kwa miaka tisa hadi kufikia kampuni 180 kwa miaka mitatu ni moja ya mafanikio ya miaka mitatu ya uongozi wa Rais Magufuli katika maabara hiyo ya kanda, tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007.

Anaeleza kuwa imeongeza huduma ya kutoa vibali vya kemikali kutoka 389 kwa miaka tisa hadi kutoa vibali 3,637 kwa mwaka miaka mitatu.

“Katika kipindi cha miaka mitatu tumefanikiwa kukusanya sampuli 12,932 kwa kutoka sampuli 412 kwa miaka tisa ya nyuma tangu kuanzishwa kwa maabara hiyo ya kanda,”anasema Anyango.

Anaeleza zaidi kuwa pia ofisi 10 kwenye kiwanja cha kiwanja cha mamlaka na  kuhama kutoka kituo cha afya Themi walipokuwa na ofisi ndogo za vyumba vitatu.

Anasema faida walizopata baada ya kuhama ofisi ni kuboresha huduma kwa kuwa na nafasi kubwa ya kufanya kazi.

Kuongezwa kwa watumishi wa kada nyingine na kupanua baadhi ya huduma na kuongeza vitendea kazi na kuongezewa gari  kwa ajili ya kazi za kanda hiyo.

Anasema pia wanaimarisha usimamizi na udhibiti wa kemikali zinazopita mipakani na kuweka kipaumbele cha kuzitunza ili kulinda mazingira.

“Afya na mazingira inaweza kuathiriwa na matumzi mabaya ya dawa hizi kama vile kemikali bashirifu na zinazotumika kutengeneza milipuko,” anaisema Anyango.

Anasema lengo ni kusimamia na kudhibiti vema matumizi ya kemikali hizo na kwamba serikali kupitia mamlaka hiyo imeimarisha utekelezaji wa sheria ya kemikali za viwandani na nyumbani namba tatu ya mwaka 2003 sura namba 182.

Anasema kwa sasa waajiriwa wa mamlaka wamepelekwa mipakani kusimamia na kudhibiti uingizaji na utoaji wa kemikali.

“Hii inatokana na ukweli kwamba katika Kanda ya Kaskazini mwaka 2015/16 tulikuwa na mtumishi wa mamlaka mmoja  kwenye mpaka wa Namanga ikilinganishwa na mwaka 2018/19 ambapo tuna watumishi nane. Kabla ya hapo maofisa afya ambao pia walikuwa hawatoshi ndiyo walikuwa wanasimamia mipaka hiyo,” anasema Anyango.

Aidha, anaeleza kuwa katika kutoa huduma za mamlaka kwenye kanda ilibainika kuwa mkoa wa Tanga una wadau wengine na mamlaka na walikuwa wanapata changamoto ya kufuata huduma hizo Arusha au  Dar es Salaam.

Anasema kuwapo kwa mamlaka hiyo mkoani Arusha bado ilionekana kutokuwa na msaada kwa wakazi wa mkoa wa Tanga hivyo walilazimika kufungua dawati.

“Serikali ya awamu ya tano ilitambua changamoto hiyo na iliamua kusogeza huduma zaidi kwa wananchi wa Tanga kwa kufungua ofisi na inahudumia mpaka wa Horohoro,” anasema Anyango.

Anataja huduma nyingine zinazopatikana Tanga ni kukusanya sampuli zote zinazohitaji uchunguzi na kuziwasilisha kwenye maabara ya mkemia.

Anyango anasema pia wanafanya ukaguzi wa kemikali kwenye viwanda na kusimamia ukaguzi wa bidhaa zinazoingia na kutoka katika mpaka wa Horohoro.

Anaeleza mafanikio mengine ya kanda hiyo ni kufanya ukaguzi kwenye mipaka yote inayofanyia kwa sasa kwa muda wa masaa 24 kila siku.

“Mipaka yote kwa sasa ina waajiriwa wa mamlaka na kabla ya mwaka 2016 wastani wa kampuni 100 zilikuwa zinakaguliwa kwa mwaka lakini kwa sasa tunafikisha kampuni 150 kwa mwaka,” anasema.

 MPAKA WA NAMANGA

Kwa upande wa Msimamizi wa Kituo cha Ukaguzi Namanga cha GCLA Michael Benard, anasema bidhaa za kemikali zinazoingia na kutoka nchini lazima wazikague Namanga  pamoja na kuhakiki vibali vya usafirishaji wake.

Anasema kuwa mwaka 2016 walikagua mizigo ya kemikali 1,300 ikiwa 750 ya mizigo hiyo ilifuata utaratibu wa sheria sawa na asilimia 57 ya mizigo iliyofuta sheria.

Anasema pia mwaka 2017 walikagua mizigo ya kemikali 1,450 ikiwa 1,120 ya mizigo hiyo ilifuata utaratibu wa sheria sawa na asilimia 77.2 ya mizigo iliyofuta sheria na mwaka 2018 mizigo 1,320 iliyofuata utaratibu 1237 sawa na asilimia 93.7.

CHANGAMOTO

Aidha,  pamoja na mafanikio changamoto hazikosekani , kwa mfano katika mpaka huo kuna njia nyingi za panya ambazo jitihada za kudhidhibiti zinafanywa kwa kushirikiana na vyombo vya dola na mamlaka nyingine kama Shirika la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).

Anasema pia wananchi wamekuwa wakipitisha kemikali bila kuzingatia sheria ya kuingiza bidhaa hizo nchini.

“Tunapoona mtu kaingia na bidhaa chache ambazo ni kemikali mfano sabuni ya unga na mafuta ya taa, tunampa elimu tu na wale ambao wamebeba kwa ajili ya biashara tunamwelimisha na kushikilia mzigo wake mpaka akamilishe taratibu za kujisajili,” anasema Benard.

 

 

Habari Kubwa