Mkapa alikuwa rafiki mkubwa wa Sir Andy Chande

01Aug 2020
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam
Nipashe
Mkapa alikuwa rafiki mkubwa wa Sir Andy Chande

RAIS mstaafu wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa, ambaye alifariki Julai 23, mwaka huu alikuwa mtu aliyeijenga sekta binafsi ambayo aliamini kuwa ndiyo injini ya ukuaji wa uchumi.

Katika makala hii Mwandishi anaeleza namna Mkapa alivyopenda na kuwa karibu na mfanyabiashara mashuhuri ambaye sifa zake zilienea kitaifa na kimataifa tangu miaka ya 60 kutokana umahiri wake kwenye uendeshaji wa biashara zake na uongozi, Andy Chande.

Hayati Mkapa ambaye alizikwa kijijini kwake Lupaso Jumatano ya Julai 29 wiki hii, alipenda kuwa karibu na wafanyabiashara wakubwa, kuwapa moyo na kuwawekea mazingira bora ya kustawisha biashara zao akiamini kwamba sekta hiyo ni muhimili pacha kwa maendeleo ya uchumi.

Mmoja wa wafanyabiashara ambao Mkapa aliwapenda na kuwaona kwamba ni injini ya ukuaji wa uchumi alikuwa mtu kutoka Bukene mkoani Tabora, Sir Andy Chande mwenye asili ya Asia.

Chande ambaye kwa sasa naye ni marehemu amekuwa mfanyabiashara maarufu na mtumishi wa umma na alikuwa mfanyakazi asiyechoka katika vikundi vinavyotoa msaada hapa nchini na mataifa mbalimbali ulimwenguni.

Mkapa enzi za uhai wake akiwa madarakani na hata baada ya kustaafu, amekuwa mtu wa katibu wa Andy Chande, wamefanya mengi, wameshirikishana mengi kiasi cha Mkapa kuandika utangulizi kwenye Kitabu chake kinachoelezea maisha yake kitwacho Shujaa katika Afrika Safari kutoka Bukene.

Kwenye utangulizi wa kitabu hicho, Mkapa anamwelezea Sir Andy Chande kuwa mwanachama wa klabu ya Round table na Rotary aliyetunukiwa nishani ya ushujaa na dola ya kiingereza.

Alisimulia kuwa simulizi yake kwa Chande inajaribu kutoa picha ya maisha ya mtu na vile vile vituko vya wakati huo, yote mawili kwa ufasaha kabisa.

Kwenye andiko lake la utangulizi kwenye Kitabu hicho, Mkapa anasema mwanzo wa karne ya ishirini dunia ilishuhudia kuhamia Afrika Mashariki kwa wahindi waliokuwa raia wa Uingereza baadhi yao kusaidia ujenzi wa reli za Afrika Mashariki na wengine kujenga mtandao wa biashara eneo hilo.

Mkapa anasema mmoja wao, Keshavji Chande baada ya kujitumbukiza kwenye safari ya hatari ya meli kutafuta utajiri, alianzisha kitu ambacho wakati ule wa robo ya pili ya karne kilionekana chombo kikubwa sana cha biashara, kampuni iliyoitwa ‘Chande Industries Limited’.

Anasema mwanawe Jayantilah Keshvji Chande maarufu kwa jina la mkato JK au Chande akiwa ndiye nguzo ya kampuni ile ya familia, ingawa kwa muda mfupi mno kutokana na kunaswa katika wimbi la kutaifishwa mali katika miaka ya ‘60’.

Mkapa anasema kwenye kitabu hicho, bila kukata tamaa aliendelea mpaka akawa mtu mashuhuri katika uendeshaji wa kampuni za viwanda na za biashara ambayo haikuwa yake tena bali sehemu ya kampuni ya biashara na viwanda yaliyomilikiwa na serikali ya Tanzania.

“Maelezo tunayoyaona humu kuhusu kipindi kile kabla ya Uhuru yamesheheni vituko, mivutano kati ya watu na matarajio ya mafanikio katika uchumi. Wazazi wa JK alikuwa wamebobea katika fani ya uhasibu, kukisia miradi inayoleta faida, kujitahidi kwa moyo wote kujenga uhusiano mwema na wakulima waliowauzia mazao na kununua mali iliyosindikwa au iliyoingizwa kutoka nje ya nchi,” alisimulia Mkapa kwenye kitabu hicho.

Mkapa alisimulia kwenye utangulizi wa kitabu hicho kuwa ingawa hakuzipenda taratibu za elimu zilizokuwa na ubaguzi wa rangi, Chande aliitumia vema nafasi aliyopewa na familia iliyompenda sana, akitumia uzoefu wake akisaidia kuhakikisha kuwa mipango katika kipindi kile cha mpito iliwashirikisha watu wote na wa rangi zote.

Alisema miaka sita baada ya Uhuru wa Tanganyika ilikuja wimbi la kutaifishwa kwa shughuli muhimu za uchumi, shughuli zote za viwanda na biashara za familia ya Chande na za watu wengine zilitaifishwa na serikali.

“Ni uvumilivu na uzalendo wa mkubwa wa familia ya Chande, siyo tu kwamba walikiri hatua hiyo iliyochukuliwa na serikali lakini vile vile walikubali kwa moyo mmoja kusimamia mabadiliko ya kumiliki sehemu ya uchumi wa nchi. Kwa kuujua vema uwezo wa Chande katika biashara Rais Nyerere alimkabidhi kwa miaka mingi uenyekiti wa bodi za mashirika mengi ya umma,” inasema sehemu ya andiko la Mpaka kwenye kitabu cha Andy Chande.

Kwenye kitabu hicho, Mkapa alisema kuwa Chande alikuwa mtu mwenye vipaji vingi, habari ya maisha yake haitakamilika bila kutaja mambo aliyoyapenda na kwamba mengi ya mambo hayo na madaraka aliyokuwa nayo yanashangaza kwelikweli.

Mkapa alifafanua kuwa alimfahamu Chande kwa mara ya kwanza kwa ari yake katika masuala ya elimu alipomweka kwenye bodi ya shule ya Shaaban Robert na baadaye akagundua kuwa alikuwa mtu mashuhuri kwenye shule ya viziwi kwani alikuwa mtu asiyepumzika kwenye shughuli za kusaidia jamii siyo kwa kuchangia tu bali kwa kuwahamasisha kwa moyo wake wote.

Alipozungumzia ndoa ya Chande na mke wake Jayli, Mkapa alisema Chande aliipenda sana familia yake na miaka 50 ya ndoa yake mapenzi yao yalianza kwa hofu lakini yakaishia kwenye pingu za uhusiano na mapenzi makubwa.

“Ukizungumza na mmoja wao utatambua jinsi alivyo na mapenzi makubwa mno kwa mwenzake, pamoja na mapenzi yao, wote wawili kwa watoto wao watatu wote wa kiume,” inasema sehemu ya andiko la Mkapa kwenye utangulizi wa Kitabu cha Chande kilichoandikwa wakati huo wote wawili wakiwa hai.

Mkapa alisema Chande alitambuliwa na kupewa heshima na vyombo vya taifa na vya kimataifa heshima ambayo yeye Mkapa alisema Hayati Chande alistahili na kwamba anafurahi kuhusishwa na kutambuliwa kwa sifa na heshima anayopewa Chande kwani ni Mtanzania mashuhuri mwenye sifa za kimataifa.

Andy Chande alizaliwa Mombasa Kenya mwaka 1928 ingawa wazazi wake walikuwa wakiishi Bukene Tabora na alifariki dunia mwaka 2017 akiwa na miaka 89.

Habari Kubwa