Mkoa mpya unaokimbia kwa kasi kufikia maendeleo

06Jul 2019
Mary Geofrey
KATAVI
Nipashe
Mkoa mpya unaokimbia kwa kasi kufikia maendeleo

KATAVI ni miongoni mwa mikoa mipya iliyoundwa ndani ya muongo mmoja uliopita. Kipaumbele kwenye maeneo hayo mapya ni kuboresha uchumi na kujiletea maendeleo bila kujali uchanga au upya wa mkoa.

Ukiwa moja ya mikoa iliyo na fursa nyingi za kiuchumi umeendelea kujiimarisha kwenye kilimo, uhifadhi, ufugaji na usafirishaji bandarini, lengo ni kuwekeza na kufikia azma ya maendeleo endelevu.

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa Juma Homera, anakutana na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali kuzungumzia masuala ya maendeleo kwenye mkoa huo na jinsi ulivyojipanga.

Anausifu mkoa huo kuwa una fursa mbalimbali za kiuchumi ambazo wanazipigia debe kutekeleza kwa vitendo sera ya kukuza uchumi wa taifa kupitia uwekezaji wa viwanda

Anasema mambo wanayotilia mkazo ni kilimo, ufugaji, utalii na sekta ya bandari ambayo inategemewa kwa kiasi kukibwa kukuza uchumi wa wananchi wa mkoa huo kwa njia ya kusafirisha bidhaa zao kwenda nchi za Zambia na Demokrasia ya Kongo (DRC).

SEKTA YA KILIMO

Homera anasema katika sekta ya kilimo wanazalisha mazao matano ya kimkakati ambayo ni pamba, tumbaku, ufuta, korosho na uvunaji wa asali.

“Tunafanya kilimo kwa zaidi ya asilimia 90 kwa sababu wananchi wamejikita kwenye kulima kibiashara na chakula hasa katika halmashauri ya wilaya ya Mhimbwe ambao wanalima ufuta na mazao mengine bila kuweka mbolea kwa sababu ardhi yake haijachoka,” Homera anasema.

Anaeleza zaidi kuwa, wanazalisha mahindi tani 250,000 hadi 400,000 kwa mwaka na mpunga ni zaidi ya tani 350,000 kwa mwaka.

Anaeleza kuwa, katika mwaka 2019/20 wanatarajia kuzalisha ufuta tani 50,000 kwa sababu wana soko la uhakika hivyo wameweka mikakati kwa kila wilaya kuzalisha mazao ya kutosha pamoja na zao la pamba.

Kiongozi huyo wa mkoa anasema pia wana mpango wa kuanza kujikita kwenye korosho na tayari wamepanda zaidi ya hekari 6,000 za mikorosho.

“Kupitia zao hili tunaamini tutafanya biashara katika mkoa wetu baada ya miaka mitatu ambako tutakuwa tumefanikiwa kuvuna,” Homera anasema.

Anawataka wawekezaji wa mazao ya chakula na biashara kama ufuta, asali, pamba na nyama kwa sababu bidhaa hizo zinapatika kwa wingi.

Anasema pia kuna fursa za uvuvi katika mkoa huo hivyo wafanyabiashara wanapaswa kuwekeza katika sekta hiyo kwa sababu wanaelekea kwenye lengo kuu la kukuza uchumi.

SEKTA YA UHIFADHI

Hifadhi ya Katavi iko juu ya ukanda wenye mafuriko wa Ziwa Tanganyika na ina ukubwa wa takribani kilomita za mraba 4,471 hivyo ni hifadhi ya tatu kwa ukubwa nchini.

Anasema hifadhi hiyo ni maarufu kwa idadi kubwa ya viboko na mamba pamoja na wanyama wengine kama samba na chui.

Anasema wameweka mikakati ya kuendelea kuhifadhi misitu kuhamasisha Watanzania wote wa nje ya mkoa huo kufika katika hifadhi hiyo kwa ajili ya kutembelea.

Homera anawaeleza wadau kuwa, endapo wananchi watajitokeza katika kuona vivutio katika hifadhi hiyo wataongeza mapato ya mkoa huo na kukuza uchumi wa wake.

Asilimia kubwa ya wanaotembelea hifadhi hiyo ni wageni kutoka mataifa mbalimbali , anasema Mkuu wa Mkoa na kwamba pamoja na wanyama hao kuwa kivutio ndani ya hifadhi hiyo, kuna mti ujulikanao ‘Mti wa Mzimu wa Katabi.’

Anasema ni mti ambao vijiji vinavyopakana na hifadhi hiyo, vimekuwa vikiutumia kuomba mahitaji mbalimbali kwa mujibu wa imani zao.

Mzimu huo unatajwa kumaliza magonjwa ya mlipuko ambayo yamekuwa yakijitokeza katika maeneo hayo, pia umekuwa ukitumika kuleta mvua kunusuru maisha ya viboko na mamba wanaoiishi kwa kutegemea uwepo wa maji katika mto Katuma, anafafanua.

“Katika mti huo wa mkwaju kunakosemekana ndiko mzimu umehifadhiwa, ni mahali makabila mbalimbali ya mkoa huo kama vile Wabende na Wapimbwe, wamekuwa wakifanya matambiko kwa mzimu huo unaoaminika kuishi mahali hapo,” anasema.

Kadhalika anasema wana maporomoko ya Sikombe ambayo ni kivutio kikubwa na hifadhi hiyo ina mazingira bora.

Anasema pia wameweka mazingira mazuri ya kuelekea katika hifadhi hiyo kwa kujenga barabara za kisasa ambazo zitawezesha watu kufika hifadhini bila matatizo.

Katika kurahisisha usafiri na watalii kufika katika hifadhi hiyo, anasema wameshakamilisha uwanja wa ndege.

Homera anasema uwanja huo tayari umeshapata kibali cha kurusha ndege hivyo wakati wowote ndege zitaanza kutua kwa ajili ya kufungua milango ya watalii kuingia kwa wingi katika mkoa huo.

Kadhalika anasema tayari wameshanunua gari ya zima moto kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kuwa na uwanja wa ndege wenye vigezo vinavyotakiwa.

UCHUMI WA BANDARI

Mkuu huyo wa mkoa, anasema wana lengo la kuongeza mapato na kujenga bandari ya Karema ambayo itapokea mizigo kutoka Dar es Salaam na Kigoma kwa ajili ya kuivushwa kwenda nchi jirani za Demokrasia ya Kongo (DRC).

Homera anasema bandari hiyo pia itasaidia kupunguza shughuli za malori barabarani ambayo yanaharibu barabara kwa sababu bidhaa nyingi zitakazokwenda Kongo zitapelekwa kwa njia ya maji.

“Kuwapo kwa bandari hii kwa kiasi kikubwa kutasaidia kuokoa fedha ambazo zilikuwa zinatumika kurekebisha barabara zinazoharibiwa na malori,” anasema Homera.

MIRADI MINGINE

Anasema pia mradi wa barabara ya kutoka Mpanda Mjini kuenda Kigoma kupitia wilaya ya Tanganyika na ile ya Mpanda kuelekea Tabora ambayo itafungua uchumi wa mkoa huo.

Anasema pia serikali inajenga hospitali katika kila wilaya, vituo vya afya kila kata na zahanati katika vijiji mbalimbali vya mkoa huo kwa lengo la kusogeza huduma za matibabu karibu na wananchi.

Hospitali za wilaya zinajengwa Mlele na Tanganyika na kwamba zitakapokamilika zitasaidia kurahisisha huduma kwa wananchi.

Kuhusu biashara anasema wamewapatia wajasiriamali vitambulisho vya kufanyia biashara na wanaitikia vyema zoezi hilo.

Aneleza kuwa, wamewatumia wafanyakazi wa sekta za umma kufikisha vitambulisho hivyo kwa sababu wananchi walikuwa wakilalamika kukosa huduma hiyo.

“Tumeshawafikia wafanyabiashara wengi na tunaendelea kuwafuatilia, tunaamini kila mmoja akipata kitambulisho ataweza kutambulika na kufanya biashara zake kwa uhuru na nimeshaagiza marufuku kusumbuliwa,” anasema Homera.