Mkono wa serikali uwafikie wabunifu wasiorasmi vijijini

23Mar 2019
Reubeni Lumbagala
Dar es Salaam
Nipashe
Mkono wa serikali uwafikie wabunifu wasiorasmi vijijini

DIRA ya Maendeleo ya Tanzania inaelekeza kuwa ifikapo mwaka 2025, Tanzania iwe ni nchi ya viwanda na ya uchumi wa kati.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, picha mtandao

Juhudi kubwa zinaendelea kufanywa na serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha kuwa azima hiyo inafanikiwa.

Uchumi wa viwanda unategemea sana mchango wa wabunifu ambao ni nyenzo muhimu katika kufanikisha jitihada hizo. Kama wabunifu waliopo katika shule, vyuo na wale waliopo mitaani watatumika kikamilifu, ni dhahiri mwelekeo wa nchi utakwenda vizuri na kufika kule dira inapotaka.

Wabunifu wengi hutumia sayansi na teknolojia, hivyo, serikali ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha masomo ya sayansi yanawekewa mkazo na umuhimu wa kipekee ili wanafunzi wengi wasome masomo hayo kwa lengo la kutoa mchango kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Kama wanafunzi wengi shuleni na vyuoni watasoma sayansi ambayo ni nguzo muhimu katika uchumi wa viwanda, kasi ya ubunifu itaongezeka na suala la kufikia uchumi wa kati litapata msukumo mpya.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) zishirikiane ili kuhakikisha wanafunzi waliopo katika shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati na vikuu wanahamasishwa kuwa wabunifu wa vitu mbalimbali ili kuchangia jitihada za kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa viwanda.

Machi 7 mwaka huu, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, alitoa wito kwa wanafunzi na wabunifu kuibua kazi mbalimbali ili kusaidia maendeleo ya uchumi wa viwanda. Waziri Ndalichako alitoa wito huo katika kilele cha Mashindano ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, ambapo kauli mbiu ya mashindano hayo ilikuwa ni “kukuza ujuzi na ubunifu kwa uchumi wa viwanda”.

Kauli mbiu hii inaonyesha umuhimu wa kupata ujuzi kwanza ili utumike katika kubuni vitu mbalimbali na hatimaye kuchangia katika maendeleo ya viwanda. Hivyo basi, ni vyema Watanzania ambao ni wadau muhimu wa kuijenga nchi kujielekeza katika kutafuta maarifa na ujuzi katika taasisi mbalimbali zinazotoa elimu ili waitumie kubuni zana, mashine na mitambo mbalimbali kufanikisha kufikia mafanikio ya uchumi wa viwanda.

Katika mashindano hayo, Ndalichako, anawahakikishia washindi kuwa wataendelezwa ili waweze kukuza tafiti na ubunifu wao kuchangia maendeleo ya nchi. Pia anatoa wito kwa wabunifu kubuni vitu vitakavyorahisha shughuli mbalimbali.

“Ninatoa wito kwa wabunifu kujikita kwenye kuangalia namna gani wanarahisisha shughuli zinazofanyika katika mazingira yao. Ikumbukwe ubunifu hauna umri na hauchagui kwa sababu mwisho wa siku mkono unaenda kinywani.”

Njia mojawapo ya kukuza ubunifu ni kuandaa mashindano ya ubunifu kwa wanafunzi katika sayansi na teknolojia kwenye shule zote za msingi, sekondari hadi vyuoni hapa nchini. Wale watakaoandaa kazi bora zaidi watambuliwe na wapewe zawadi na vyeti maalum kutambua uwezo wao kiubunifu.

Mashindano hayo pia yanaweza kuvuka mipaka kwa kushindanisha ubunifu kutoka shule moja na nyingine au chuo na kingine ili kukuza ubunifu zaidi miongoni mwa wanafunzi.

Nje na taasisi za elimu, wapo wabunifu waliopo mitaa na vijijini ambao serikali haiwatambui na baadhi yao hawana elimu au wana viwango vidogo, lakini wamejaliwa vipaji vikubwa vya kubuni vitu mbalimbali. Hawa nao wanapaswa kupewa kipaumbele kikubwa katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Katika halmashauri ni wakati wa kuanzisha dawati maalum la kupokea kazi mbalimbali za wabunifu ili waweze kuendelezwa na kazi zao zichangie katika maendeleo ya nchi. Kwa kutowapa fursa za kutambua wabunifu nje na mifumo rasmi ya kiserikali, nchi itapoteza wataalamu wengi wenye ubunifu unaohitajika sana katika kipindi hiki muhimu.

Wabunifu wakithaminiwa kwa kuendelezwa na kuwezeshwa katika tafiti zao, wengi watashawishika kujikita katika kubuni vitu mbalimbali. Ni wakati wa Tanzania kuwa na uwezo wa kutengeneza mashine zake yenyewe zikatazotumika viwandani badala ya kuziagiza kutoka nje ya nchi.

Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi (Veta) na Idara za Masomo ya Sayansi na Teknolojia katika vyuo vikuu nchini zipewe ruzuku ya kutosha itakayofanikisha utekelezaji wa utafiti na uvumbuzi wa mitambo mbalimbali inayohitajika kufikia maendeleo ya viwanda.

Utamaduni wa kutiana moyo pamoja na kupongezana miongoni mwa wabunifu upewe msukumo mkubwa ili wagunduzi hawa wasikatishane tamaa katika kazi zao.

Kama nchi Watanzania washirikiane katika kuhakikisha kazi za kibunifu zinaendelezwa ili nao wachangie maendeleo ya viwanda na hatimaye kufikia uchumi wa kati.

Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
Maoni: (+255) 764 666349.

Habari Kubwa