Mkurugenzi jiji Dar afunguka siri kung’ara tuzo bora ya afya kimkoa

25Nov 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mkurugenzi jiji Dar afunguka siri kung’ara tuzo bora ya afya kimkoa
  • Upanuzi, ujenzi mpya sasa kila kona
  • Sh. Mil 750 ya simu yaipa kituo afya

HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam, inayoundwa na Wilaya ya Ilala ikiwa na majimbo matatu ya uchaguzi; Ilala, Ukonga na Segerea, ndani yake kuna kata 36, imeongoza kufanya vizuri kwenye eneo la afya.

Inatajwa ni zao la tathmini ya viashiria vya utoaji huduma bora za afya mkoani Dar es Salaam na katika shindano lililofanyika hivi karibni, ikishirikisha Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam ambazo ni: Manispaa za Temeke, Kinondoni, Kigamboni na Ubungo, tuzo ikiangukia kwa jiji la Dar es Salaam.

Tuzo ya pili ilishirikisha hospitali za rufani za Mkoa Dar es Salaam; Temeke; Mwananyamala ya Kinondoni; na Amana jijini Dar es Salaam, iliyotwaa ushindi.

Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri, anaeleza mipango ya kuendelea kutoa huduma bora ya afya kwenye jiji hilo, ikiwamo ujenzi wa zahanati na vituo vya afya pembezoni mwa jiji, ili kurahisisha huduma kwa wananchi.

“Mkutano wa mwaka wa tathimini hiyo ya huduma za afya umekuwa na lengo la kuona hali ya utoaji huduma za afya na kuweka mikakati ya kuboresha zaidi huduma hizo katika hospitali za rufani za Mkoa za Mwananyamala, Temeke na Amana, pamoja na vituo vya afya na zahanati,” anasema Shauri.

Anataja vigezo vilivyyoshindanishwa ni: Utoaji huduma bora ya mama na mtoto; utawala na fedha utoaji dawa; maabara; vifaa tiba; mazingira bora; lishe na ustawi wa jamii.

Shauri anasema, utaratibu unaofanywa na Mkoa wa Dar es Salaam wa kuwa na tathmini ya mwaka na kupanga mikakati ya kuboresha utoaji huduma bora, katika sekta ya afya ni chachu kwao kuendelea kufanya vizuri katika utoaji huduma bora kwa wananchi.

Hata hivyo, anazitetea halmashauri zingine za mkoa Dar es Salaam, kwamba zinafanya vizuri, ila kuna maeneo maeneo Jiji la Dar es Salaam, limewazidi.

ZAHANATI/ VITUO AFYA

Shauri anasema, kwa kutumia mapato ya ndani, wanajenga zahanati na vituo vya afya vipya, huku ujenzi huo ulioanza kwenye mwaka wa fedha 2019/2020 na mwaka uliopo, mradi huo ni wa zahanati na vituo vya afya vitano.

Anataja zahanati tatu zimeshakamilika na zimeanza kutoa huduma, akizitaja kuwa ni: Lubakaya iliyopo Kata ya Zingiziwa, Luhanga na Mbondole katika kata ya Msongola.

Pia, anavitaja vituo vya afya viwili, Mzinga kinachojengwa katika kata ya Mzinga ambayo ni ghorofa mbili, kikiwa kimekamilika hatua ya boma.

Kingine ni Kituo cha Afya Gulukakwalala, katika kata ya Gongolamboto inayomaliziwa, majengo manne yamekamilika na tano linamaliziwa.

Shauri anataja mradi mingine inayojengwa kwa bajeti ya ndani ni zahanati tano zinazofanyiwa upanuzi kuwa vituo vya afya, ambazo ni Zingiziwa, Kinyerezi na Majohe na Kituo cha Afya Kipunguni.

Shauri anahidi wataendelea kutoa huduma ya afya kwa wazee kama sera ya taifa inavyoelekeza wasio na uwezo kuanzia miaka 60, wanapaswa kutibiwa bure na wawe na dirisha lao la huduma ya dawa, vivyo hivyo huduma ya mama na mtoto.

FEDHA ZA SIMU

Shauri anasema, serikali hivi sasa kupitia fedha za tozo ya mitandao ya simu, imeshatoa Sh. Milioni 750 kwa ajili ya ujenzi mpya wa Kituo cha Afya Mchikichini; huku kukiwapo upanuzi wa vituo vya afya vya Segerea na, Kiwalani, vikiongezewa majengo,

"Lengo la serikali ni kuboresha huduma za afya pale walipo wananchi, hivyo kwa uwepo wa vituo vya afya wananchi watapata huduma ya upasuaji, utra-sound, x-ray, upimaji na kulazwa," anafafanua Shauri.

HOSPITALI YA KIVULE

Kupitia Mapato ya Ndani, Mkurugenzi anasema Halmashauri ya Jiji Dar es Salaam, inajenga jengo la ghorofa mbili kwa ajili ya Huduma za haraka na bima ya afya, kwenye Hospitali ya Kivule, ikitengewa Sh. bilioni mbili katika mwaka wa fedha uliopo 2021/2022. Hadi sasa uko hatua ghorofa ya kwanza.

Shauri anasema, nyumba za watumishi zinajengwa kwenye zahanati za Luhanga na Mbondole kila moja nyumba moja, zote zikiwa na uwezo wa kuishi familia mbili zipo katika hatua za umaliziaji.

Anasema zahanati zinazojengwa pembezoni mwa jiji, kwa sasa zinaenda sambamba na nyumba za watumishi, ili kuwapa motisha wahudumu wa afya waishi jirani na maeneo yao ya kazi, pia kuleta tija katika utoaji huduma.

WAHUDUMU AFYA

Shauri anasema watumishi wa afya jijini Dar es Salaam wako 1,095, ilhali mahitaji halisi ni 1,430, ikimaanisha upungufu wa watumishi 335 au walipo ni asilimia 76 pekee (robo tatu).

Hata hivyo, anafafanua wapo kwenye jitihada za kuomba watumishi wa afya wa kada mbalimbali kila mwaka, kwani bado ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali unaendelea, hali inayofanya kuwapo idadi ya kutosha kuhusu wanaokidhi hitaji hasa madaktari, matabibu wauguzi na wataalamu maabara.

Anatoa takwimu za madaktari waliopo ni nusu, kwa maana 41 kati ya hitaji la 80; matabibu 110, kati ya hitaji la 130; wauguzi waliopo ni 440 na wanaohitajiwa ni 540; hali kadhalika wataalamu maabara 74 kati ya hitaji 90.

WANUFAIKA WALONGA

Diwani wa Kata ya Mzinga, Job Isaack, anasema Kituo cha Afya Mzinga kitawasaidia wananchi wa kata hiyo na jirani kupata huduma ya afya, kwani huduma zote muhimu zitapatikana hapo.

"Ujenzi wa Kituo cha Afya Mzinga Magole unaendelea, na matarajio ni katika kipindi hiki cha mwaka 2020-2025 kitakuwa kimekamilika kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wa Kata ya Mzinga na kata jirani, kwani kitakuwa na ghorofa mbili kukidhi huduma zote muhimu kwenye masuala yote ya afya," anaeleza diwani.

Anafafanua kuwa awamu ya kwanza, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeshapeleka jumla Sh. milioni 305, huku kituo kikitengewa bajeti ya Sh. bilioni 1.2 hadi kukamilika kwake.

Mkazi wa kata ya Mzinga, Said Ndembo, anasema kupata Kituo cha Afya Mzinga ni neema kubwa sababu wamekuwa wanadumiwa na kata jirani za Kitunda, pia Buza iliyopo katika Manispaa ya Temeke, hivyo hatua hiyo mpya inawaondolea wananchi, hasa wanawake na watoto.

Ndembo anaushukuru uongozi wa Kata ya Mzinga Isaack, kwa kukaa na Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) kuwasilisha wazo la kuwapo kituo hicho cha afya.

Habari Kubwa