Mlipuko wa Uviko 19 Ulaya kwingi warejea zuio, baadhi chanjo lazima

25Nov 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mlipuko wa Uviko 19 Ulaya kwingi warejea zuio, baadhi chanjo lazima
  • *Wapingaji waandamana ‘hatuzitaki zote’

MAAMBUKIZI ya virusi vya corona yanaongezeka kwenye nchi nyingi za Ulaya kwa kasi, wakati bara hilo linaelekea kwenye kipindi cha majira ya baridi.

Kasi kubwa ya mikasa iko juu zaidi Ulaya Mashariki na kusababisha baadhi ya nchi kufanya uamuzi. Wengi wanatafakari uamuzi iwapo zianzishe tena vizuizi vya kukabiliana na virusi corona kabla ya msimu wa Krismasi na jinsi ya kuwashawishi watu kupata chanjo.

Majadiliano hayo yanatokea huku majirani zao bara Asia, isipokuwa China zinafungua tena sekta ya utalii duniani
Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk. Hans Kluge, anasema kasi ya maambukizi sasa katika nchi 53 za bara Ulaya inaleta wasiwasi mkubwa, virusi vya corona vinasambaa haraka katika miezi ya baridi wakati watu wanakusanyika nyumbani.

Awali, kiongozi huyo wa WHO, alionya kuna shaka ya kuwa vifo 500,000 vinavyohusiana na COVID-19 ifikapo Februari ijayo. Mkurugenzi Kluge anafafanua:

''Kwa jumla, sasa kuna zaidi ya visa milioni 78 vilivyoripotiwa kwenye nchi za Ulaya, kuliko Asia Kusini na Mashariki, Mediterania Mashariki eneo la Magharibi ya Bahari ya Pasifiki na Afrika kwa pamoja. Kwa mara nyingine tena tuko kwenye kilele cha maambukizi,''

Bara la Ulaya kuna ongezeko la asilimia sita wiki mbili zilizopita kupitia mikasa milioni 1.8; Ujerumani yenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya imeripoti kuwapo maambukizi mapya 33,949 kwa siku, ikiwa ni ongezeko kubwa kushuhudiwa katika eneo hilo tangu kuzuka maradhi hayo.

Pia, kuna nchi kama Russia na Ukraine, janga hilo linazidi kuongezeka, nchini Austria kukiwapo rekodi ya juu zaidi, katika nchi kama Uingereza, maambukizi yameongezeka kwa kiwango cha juu zaidi.

Mataifa ya Hungary na Poland yenye uchumi mkubwa zaidi Ulaya Mashariki, nayo yamerekodi kiwa na mambukizi mpya yaliyovunja rekodi tangu ushuhuda wa Aprili, mwaka huu, hali kama hiyo ikitawala mataifa ya Croatia, Slovenia, Czech na Slovakia.

China, ambako ndiko mzizi wa tatizo, nako kuko katika tahadhari kubwa kwenye bandari za kuingia nchini humo katika juhudi za kupunguza hatari za maambukizi hayo.

HATUZA CHANJO

Serikali ya Ujerumani imetangaza vikwazo vya usafiri katika wilaya zake ambako kwa siku saba zilizopita, huku katika baadhi ya majimbo kunaanzishwa vikwazo vya safari kwa ambao hawajapata chanjo, hali kadhalika maeneo kama saluni, vyuoni na vituo vya elimu kwa watu wazima.

Aidha, mkusanyiko wa watu hataruhusiwa na jumla ya watu watano kutoka familia mbili tofauti ndio wataruhusiwa kujumuika pamoja kwa wakati wowote.

Katika matamasha ya kitamaduni na michezo, asilimia 25 tu ya idadi jumla inayokubalika ya mashabiki ndio wataruhusiwa na sheria za kinga zitazingatiwa.

Katika maduka, idadi ya wanaoingia ndani itadhibitiwa: mteja mmoja katika eneo la mita 10 za mraba.

Jimbo la Mashariki mwa Ujerumani, Saxony, limeshatangaza masharti mapya yatakayoanza wiki mbili na nusu zijazo, Desemba 12, kudhibiti maambukizi ya maaradhi Covid 19, ikiwamo kufungwa soko kubwa nchini humo.

Vilabu, baa, kumbi za mazoezi na au makumbusho pia yatafungwa. Michezo itaruhusiwa kufanyika bila ya mashabiki na marufuku ya kuwa nje usiku kati ya saa nne hadi saa 12.00 asubuhi.

Maofisa Afya wanasema, ongezeko la maambukizi katika jimbo la Saxony huenda ni kutokana na idadi ndogo ya watu waliochanjwa. Ni jimbo lililoko nyuma zaidi, nchini Ujerumani kwa waliopata chanjo.

AUSTRIA ‘KUMEKUCHA’

Austria imeanza rasmi kukabiliana na wimbi la nne la maambukizo ya virusi vya corona, siku moja baada ya miji kadhaa barani Ulaya kushuhudia maandamano makubwa ya umma.

Ni tangu Jumatatu wiki hii kutekeleza amri ya kuzuia baadhi ya shughuli muhimu za maisha, kukabiliana na idadi ya wanaopoteza maisha kila siku kutokana na COVID-19.

Baadhi ya hospitali zinaonya kwamba uwezo wa vyumba vyao vya wagonjwa mahututi unakaribia kufikia ukomo. Zuio la sasa limepangwa kudumu kwa siku 10, lakini upo uwezekano wa kuongezwa hadi siku 20, watu wanaruhusiwa tu kutoka majumbani wakiwa na sababu za msingi, kama vile kununua vyakula, kumuona daktari na kufanya mazoezi. 

Ni Ijumaa iliyopita, Waziri Mkuu wa Austria, Alexander Schallenberg, ametangaza rasmi chanjo dhidi ya virusi vya corona itakuwa ya lazima kuanzia Februari Mosi, mwaka ujao. Ni kama kipindi cha wiki 10 zijazo.

MAANDAMANO KUPINGA

Barani Ulaya, kulishuhudiwa maandamano ya maelfu ya watu siku ya Jumapili iliyopita, katika baadhi ya nchi wanaopinga uwezekano wa mataifa yao kutangaza marufuku kama hizo zilizoelezwa. 

Huko katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya (EU), Brussels, Ubelgiji waandamanaji walipaza sauti zao nje kupinga hatua mpya za vizuizi vilivyowekwa ya nchi yao, wakidai wanataka uhuru wao “kuishi bila kubaguliwa kwa sababu ya chanjo ya corona” wakiamini ni uhuru wao wa msingi katika maadili ya magharibi.

“Kuchomwa chanjo kwa kitu kisichofanyiwa majaribio vyema, kutoweza kufanya kazi unapotaka, kuwa utakapo, hayo siyo maadili yetu, huo sio uhuru, hivyo sivyo tunavyoishi, " anatamka mwandamanaji, Eveline Denayer mjini Brussels.

Maandamano kama hayo yamefanyika pia katika miji ya nchi za Ulaya zikiwamo Uholanzi, Denmark na Ujerumani.

Kwa mujibu wa taarifa za kimataifa.

Habari Kubwa