Mnada wa Vingunguti ulivyogubikwa na msuguano wa wachinja mifugo

04Mar 2016
Efracia Massawe
Dar
Nipashe
Mnada wa Vingunguti ulivyogubikwa na msuguano wa wachinja mifugo

UNAPOZUNGUMZIA eneo la Vingunguti Jijini Dar es Salaam sehemu kubwa ya umaarufu wake uko katika machinjio ya mifugo.

Mbuzi na kondoo wakiwa machinjioni Vingunguti, ambako kuna mgogoro wa wachinjaji. (PICHA NA MTANDAO)

Katika kufanikisha jukumu hilo, kuna watu mahsusi ambao wanawajibika na kuchinja na kuuza nyama mnadani Pugu.
Ili kujiweka sawa katika jukumu hilo, wafanyabiashara wanaohusika na uchinjaji, pia kunadi mifugo katika machinjo hayo, wameunda chama maalum kiitwacho Chama cha Wafanyabiashara wa Mifugo na Mazao yake Vingunguti (Uwamivi Society).

Chombo hicho kilichoanziswa mwezi Septemba mwaka 2012, hadi sasa hakijawa imara katika kutekeleza majukumu yake na kuwaunganisha wanachama wake.

Lengo lilikuwa kuwatambua na kuwaunganisha walengwa wazalishaji na wauzaji mifugo na mazao yao, ili kubadili maisha yao.

Hiyo inaendana na kushirikiana na serikali na taasisi husika za umma na binafsi, katika kuanzisha na kukuza uwezo wa kujiajiri.

UFA KATIKA CHAMA
Licha ya simulizi nzuri ya msingi wa kuanzishwa chama, wafanyabiashara wakuu wa nyama za ng’ombe, mbuzi na kondoo bado wanatofautiana na kuzua mvutano mkubwa baina yao.

Kuna madai kwamba baadhi ya viongozi wanawashinikiza wafanyabiashara kuchinja ng’ombe wawili tu kwa siku, ambayo inadaiwa kuwa kinyume na agizo la Manispaa ya Ilala, mfanyabiashara kuchinja ng’ombe kulingana na mahitaji wa wateja wake.

Wanachama hao wa Uwamiv wanalalamika kuwa wanatozwa kila mmoja Sh. 1,000 kwa siku zinazodaiwa kutunisha mfuko wa chama na kununulia vitendea kazi muhimu.

Inaelezwa kuwa makusanyo hayo yanatunisha Sh. 150,000 kwa siku pesa ambazo zimekuwa zikikusanywa tangu mwaka 2011, lakini matumizi yake hayaonekani.

Katika kuboresha makusanyo hayo, mwaka 2012 chama hicho kilijenga meza maalumu ya kubeba bidhaa za wafanyabiashara ndogo na ndiko makusanyo yalikofanyika.

Utaratibu husika unaeleza kuwa kila mwanachama mpya anawajibika kutoa kiingilio cha Sh. 20,000 na namna ya kuchinjia

Sh.70, 000, inayofanya gharama zote kuwa Sh. 90,000. Ni gharama zinazoelezwa kuwafikia wanachama hai 150.
Je, madai hayo yana usahihi? Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya llala, Isaya Mngurumi anasema:“Kama leo wanalazimishwa kuchinja ng’ombe wawili hilo ni kosa na haliko katika katiba yao, kwa sababu kama mahitaji ya nyama ni makubwa kwa nini wapangiwe kiasi cha kuzalisha bidhaa?

“Nawashauri watafute katiba ya chama chao waisome kwa makini watafute ufumbuzi haraka bila hivyo watakatana mapanga.”

WAFANYABIASHARA WALALAMIKA
Wafanyabiashara hao wanadai kuwa kila siku kupitia machinjio, wanazalisha damu pipa 20 yenye thamani ya Sh. mil.18 na kwa mwaka inakadiriwa kufikisha bilioni 216.

Alex Peter ni miongoni mwa wafanyabiashara anaodai kuwa katika kipindi cha miaka minne, kuna kiasi cha Sh. bilioni 864 hazijatolewa ufafanuzi, licha ya kuwapo kilio chao cha kila mara.

Anasema kero hiyo ni miongoni mwa changamoto iliyowashawishi kujiengua na chama hicho, lakini bado wameendelea kushinikizwa kuchinjwa ng’ombe wawilii kwa siku, badala ya 10 waliokuwa wakiwachinja awali.
“Ninaona kama wananigandamiza, kwa sababu natakiwa kuwahudumia wateja wangu nyama isiyopungua ng’ombe 10 kila siku.

“Hivyo, wanaponizuia na kunishinikiza nichinje ng’ombe wawili tu, huko ni kukatisha malengo na mafanikio kwa mfanyabiashara,” anasema Peter.

Anasema mazingira ya mgogoro yamekuwa na athari katika bei ya nyama inayouzwa machinjioni hapo, badala ya kuuzwa kwa bei kati ya Sh. 5,300 au Sh.5, 400, bei hiyo imepaa hadi Sh. 6,000 machinjioni hapo.

Mfanyabiashara mwingine, Leonard Japhet, anasema baada ya kuibuka ufa, uongozi wa Uwamiv, uliwatengea eneo walilotakiwa kulipa Sh. milioni moja kwa siku.

VIONGOZI WANENA
Mwenyekiti wa chama hicho – Uwamiv, Anatory Zuber ni kwamba haoni changamoto ya kuzua mgogoro kati yao, kwa sababu dhamira ya chama ni kuhakikisha wadau wanalize bidhaa zao kwa wakati.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Mngurumi, anawashauri wanachama wanapohisi kufanyiwa mambo kinyume na katiba, wajitoe katika chama.

Mngurumi anasema mgogoro unachipua, alikutana na uongozi na wadau hao na kwa pamoja walikubaliana kuchinja ng’ombe kulingana na orodha ya wateja na sio vinginevyo.

Anasema kikao kilichofanyika Januari mwaka huu, waliafikiana kila mfanyabiashara mwenye wateja awahudumie kulingana na uwezo wake.

Mngurumi anasema kuwa, chama hicho kilisajiliwa kikiwa na vitengo vinne ambavyo ni ; wanunuzi wa mifugo ndani na nje ya Dar es Salaam; kuchinja na kuuza nyama (wachinjaji); na eneo linalohusika na kuchuna ngozi, mbolea, damu, pembe, mifupa, kwato, na uchunaji.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: +255 753 390772 au barua pepe: [email protected]

Habari Kubwa