Moringe, mjukuu wake Baba wa Taifa ayakumbuka makonzi yalimwadabisha

14Oct 2021
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Moringe, mjukuu wake Baba wa Taifa ayakumbuka makonzi yalimwadabisha

KATIKA kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Yapo mengi yanaendelea na jana huko Geita, kulikuwapo na mjadala maalum.

Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere (wapili kulia) akicheza bao, enzi ya uhai wake. PICHA: MTANDAO

Watu wa kada mbalimbali wa wanazungumzia wanavyomfahamu Mwalimu Nyerere, miongoni mwao akiwa mjukuu wake, Moringe Magige Nyerere.

Mtu anapotamka tu jina la Moringe, ambalo ni nguzo nyingine ya taifa, marehemu Edward Moringe Sokoine, inaibua maswali.

Hapo ndipo mhusika analitolea ufafanuzi kwamba: "Watu wengi wamekuwa wakiuliza jina hili kwamba nilipewaje? Nilipewa kama kumbukumbu yake hasa baada ya kuondokewa na mmoja wa wasaidizi wake (Mwalimu Nyerere) wa karibu serikalini."

Moringe ambaye sasa ni mtu mzima na mtumishi wa umma, anaiambia Nipashe kuwa, alizaliwa miezi minne tangu kutokea kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Hayati Moringe Sokoine, Aprili 12, mwaka 1984 huko Morogoro, kwa ajali ya gari.

Mjukuu huyo wa Baba wa Taifa, yuko wazi kuhusu hulka aliyoifahamu kutoka kwa babu yake kwamba ‘ni kipenzi chake’ na ndio sababu hakusita kumpatia zawadi ya jina hilo mzaliwa huyo wa Monduli, abaki kuwa kumbukumbu ya kudumu ndani ya familia ya Nyerere.

MAK0NZI KWETU

Kwa sasa, Moringe anajitambulisha ni Ofisa Mwandamizi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), jijini Dar es Salaam, akiwa na ufafanuzi namna babu yake alipenda kumwadhibu kwa ‘makonzi’ pale anapoenda kinyume katika nidhamu ya maisha nyumbani.

“Babu hakutulea vibaya, bali alipenda maendeleo yetu, ndiyo maana alitupiga makonzi pale tulipomkosea, hasa wajukuu ambao walikuwa na utundu wa kitoto, waliyapata kisawasawa," anasema Moringe.

Mjukuu huyo wa Baba wa Taifa, anasema babu yao alikuwa nao karibu kuhakikisha wanaepuka makundi yasiyofaa na kwamba anajigamba ndiyo malezi yamemfanya leo kuwa mtu mwema kwenye jamii.

"Kwa ujumla ni kwamba babu alitupenda na aliipenda familia yake, kwani pamoja na makonzi, tulikuwa tunakula naye chakula, pia wakati akiwa amepumzika tulikuwa tukimtania na kucheka naye," anasimulia.

Moringe anasema baadhi ya wanaamini kuwa mababu huwapenda wajukuu hawawakanyi wanapofanya makosa, lakini Moringe anakana hilo lilikuwa kinyume kwa babu yake, nafasi ya msamaha kwa makosa haikuwapo, kuachiwa watakavyo.

PENYE SHULE?

Kama ambavyo baadhi ya wazazi na walezi wanaojua umuhimu wa elimu hufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni, anasema Baba wa Taifa naye alifanya hivyo kwa wajukuu wake aliokuwa anaishi nao Butiama.

"Babu hakuwa na mzaha na elimu, alikuwa akifuatilia maendeleo yetu shuleni, kwani kila mwisho wa muhula alikuwa akitukusanya na kukagua matokeo ya kila mmoja wetu ili kujiridhisha kama tunafanya vizuri," anasema.

Mjukuu huyo anataja masomo ya Hisabati na Kiingereza kuwa ndiyo alikuwa akiwahimiza wayakazanie kwa kuwa ndiyo msingi mzuri wa kujua masomo mengine kirahisi kwa kuwa yako kwenye lugha ya Kiingereza.

"Kimsingi, alijua bila kuwa na msingi mzuri wa lugha ya Kiingereza, inakuwa vigumu kuyaelewa kwa ufasaha masomo mengine, ndiyo maana alitukazania na mimi nimeona umuhimu wa kile alichosisitiza," anasema.

Anafafanua kuwa pamoja na hayo, aliwafundisha kuhusu maisha ya kawaida mara baada ya kujitegemea, kwa kuepuka kujipatia mali kwa njia isiyo halali au kujionyesha kwa kuwa wanatoka kwenye familia hiyo maarufu nchini.

"Tunapoadhimisha kumbukumbu ya miaka 22 ya kifo cha Baba wa Taifa, binafsi ninamkumbuka kwa mengi aliyokuwa akifanya nyumbani, hasa baada ya kustaafu, kwani wakati wa uongozi wake nilikuwa sijazaliwa," anasema.

"Ukifuatilia historia ya babu utagundua kwamba hakuwa mtu wa kujilimbikizia zisizo za halali, hivyo hata watoto na wajukuu zake alitamani tuishi maisha kulingana na kile tunachokipata kihalali," anasema.

UBISHI KWENYE BAO

Moringe anasema, babu yake alikuwa na rafiki binamu, aliyemtaja kwa jina la Nyang'ombe ambaye walikuwa wakicheza naye bao kila mara na hakutaka kuzongwa na mjukuu anapokuwa anacheza.

"Wakati akicheza bao na rafiki yake, sisi tukiwa wadogo tulikuwapo tunashuhudia, lakini hakutaka kuzongwa na wajukuu wakati anacheza, alitaka kuelekeza umakini kwenye bao ili asifungwe," anasema.

Anasema, kama ilitokea mtoto akakatiza na kusababisha ashindwe kuelekeza akili kwenye bao, alimpiga makonzi, na kwamba ilibidi wawe makini wasumsumbue anapokuwa kwenye mpambano wa bao.

"Yaani ukikatiza mbele yake wakati anacheza bao lazima upate konzi, kwani alitaka kama unashuhudia mechi yao, basi ukae utulie uone anavyopambana na Nyang'ombe hadi mwisho wa mchezo," anasema.

Anaongeza kuwa wakati mwingine Baba wa Taifa na rafiki yake walicheza hadi usiku hali ambayo iliwafanya (wajukuu) kuchoka kushindwa kuendelea kuwashuhudia na kuamua kwenda kulala.

Kwa mujibu wa Mzee Nyang’ombe Waribo katika simulizi yake miaka 20 iliyopita, kijijini kwake Muryaza umbali wa kilomita saba kutoka Butiama, Mwalimu Nyerere alikuwa mbishi katika mchezo huo na mbwembwe nyingi kumkosoa mpinzani wake, ambao ni marafiki tangu utotoni.

Anasema hakuwa tayari kwenda kulala, kuna wakati hadi saa sita usiku, hasa pale anapofungwa mchezoni, hata wanapoenda kupumzika, ananuia kurudiana siku inayofuata na inapotokea kafungwa siku hiyo, anaamua kesho yake kurudiana.

Nyang’ombe, ambaye sasa ni marehemu, ana simulizi kwamba inapotokea Mwalimu ana safari siku inayaofuata na ameshafungwa, wakati huo mara nyingi akitumikia kamati inayohusika na ukombozi Afrika, alinuia hata alipokanyaga tu kijijini Butiama, alituma gari kumfuata Nyang’ombe wapambane tena.

Ni ushindani ambao Nyang’ombe anauhadithia kuwa, Mwalimu Nyerere alitamba, hasa alipotoka safari akinukuu aliyomkejeli nayo kimchezo “nimetoka Lagos (Nigeria) unapajua wewe?” Anasema huku akifafanua kuwapo mbwembwe za kuwanunulia soda mashabiki waliojaa kutazama mpambano huo wa kijiji.