Moro wajipanga vilivyo kufuta tiba duni ya macho kwa wazee

16Mar 2017
Christina Haule
Morogoro
Nipashe
Moro wajipanga vilivyo kufuta tiba duni ya macho kwa wazee

UGONJWA wa macho ni tishio kubwa kwa jamii kubwa katika sehemu mbalimbali nchini na katika mikoa yote nchini, kuna watu wenye matatizo ya aina mbalimbali, ama shida katika kuona au kutoona kabisa.

Hilo ni tatizo linaloashiria hatari ya kuwepo idadi kubwa ya watu wenye matatizo ya aina hiyo na inahitaji juhudi za ziada kukabiliana nazo, kupitia njia mbalimbali kama vile tiba na ushauri.

Ni hali inayofikia sasa hatua hata bajeti ya serikali kupitia Halmashauri ni ndogo na kusababisha, viashiria vya ugonjwa huo kwa wananchi wa eneo husika, huku wanashindwa kupata tiba kwa wakati na wanaishia katika hitilafu wa uoni hafifu au kutoona kabisa.

Mratibu wa Shirika la Wazee Morogoro (Morepeo), Peter Mwita, anasema, Kitengo cha Macho (CMT) kupitia wizara yenye dhamana na afya nchini, kimetengewa na mgawo wa bajeti asilimia moja ambayo ni jumla ya Shilingi bilioni 800, katika kuhudumia hospitali, zahanati au vituo vya afya kitaifa.

Anasema, mtihani unaowaangukia wazee wanaohitaji huduma za bure za macho ni hasa changamoto inayojitokeza katika upatikanaji wa miwani na kilio chake ni bajeti kuongezwa.

Mwita anasema utafiti uliofanywa na shirika lake mkoani Morogoro, umebaini kuna watu 22,184 wenye hatari ya kuwa na uoni hafifu au upofu na kupitia mradi wa Mwangaza unaosimamiwa na shirika la Help Age International, ikishirikiana na Sight Savers na Hilton Foundation, wameamua kutoa elimu ya siku mbili kwa wadau husika.

Kwa mujibu wa Mwita, wadau hao ni Wakurugenzi, Wenyeviti wa Halmashauri na Madiwani wajumbe wa Kamati za Afya za Halmashauri za wilaya za Morogoro na Manispaa, lengo ni kuweka msukumo katika kuongeza bajeti ya kusaidia huduma za macho.

Mwita anasema tatizo la macho limekuwa likiwapata watu wengi na hasa wanawake,akitoa mfano wa Kamati za Afya za Halmashauri za wilaya hizo kwa namna nyingi zina wanawake wanaotumia muda mwingi kushughulikia uchumi wao, kutumia kuni zinazotoa moshi, pia wanakaa juani.

MRATIBU WA MRADI

Neema Kalolo, ambaye ni Mratibu wa Mradi wa Mwangaza, anasema tayari watoa huduma 382 kutoka vituo vya mkoa huo wameshafundishwa namna ya kutoa huduma za macho, ili kusaidia kukabiliana na changamoto ya uchache wa wataalamu kwenye eneo hilo la kitaaluma.

Anasema wakazi wa vijijini hujikuta wanaishia katika matatizo ya macho na hata upofu, bila sababu za msingi, ilhali ni linalotibika, Hivyo, ameiagiza jamii kutowaacha nyuma wenye uoni hafifu, bali wawapeleke hospitali kupata tiba.

Neema anasema mradi anaouhudumia huo umeshaanza na kwa sasa uko katika ujenzi wa Kituo cha Afya ya Macho Gairo, ambako hakuna kituo kinachotoa huduma za macho, mradi huo ukitarajiwa kugharimu shilingi milioni 42 na itakamilika Juni mwaka huu. Lengo lililopo ni kwamba, hadi kufikia mwaka 2020, jumla ya watu 110,000 wawe wameshapima macho yao.

Naye Ashrafu Mlanzi, ambaye ni Mratibu wa Macho mkoa wa Morogoro, anasema bado tatizo la takwimu linaendelea kuwa na walakini, hivyo anazishauri taasisi husika kuona umuhimu wa kuhifadhi takwimu sahihi.

Anasema, Hospitali na Vituo vya Afya vya Morogoro vinakabiliwa na uchache wa madaktari au wataalamu wa upasuaji macho na anatoa mfano kwamba, Wilaya za Kilosa na Mvomero, kila moja ina daktari mmoja; Morogoro (2), huku Kilombero na Ulanga hazina kabisa madaktari wataalamu hao.

Jingine analolalamikia Mlanzi ni kwamba, hadi sasa mkoa wa Morogoro una wataalamu watano tu wa kutoa miwani na sehemu kubwa ya wakazi hawafahamu kuwepo tiba au huduma hizo za macho zilizopo kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati jirani.

VIONGOZI MANISPAA MORO

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufani Morogoro (RMO), Jackob Frank, anatoa rai ya kuwekwa umuhimu wa kutenga bajeti za wazee kwa kila eneo hilo la macho, kwani wamekuwa wakipata shida kila wanapoenda kupata huduma na anaishauri Morpeo kushughulika na changamoto ambazo hospitali za wilaya zinapata katika tiba ya macho.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Kibena Kingo, anasema Halmashauri haikuwa na utaratibu wa kuingiza bajeti ya Afya ya Macho, kwenye bajeti kuu ya afya na baada ya kuona umuhimu wake, atashirikiana na Kamati ya Afya ya Wilaya.

Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Milikieli Mahiku, anakiri hawakuwa na utaratibu wa kuandaa bajeti ya macho pekee, bali walitenga bajeti ya afya bila ya kuzingatia upekee wa magonjwa ya macho na kuunganisha umuhimu wake katika uchumi wa jamii.

Anasema msimamo uliopo sasa ni kwamba, kwa kushirikiana na Kamati ya Afya ya Manispaa, wamekubali kutekeleza mpango wa huduma za afya ya macho kwa vitendo, kwa kutenga bajeti na kuiingiza kwenye mpango wa kila mwaka, ili kuepusha utegemezi uliopo unaozaa vikwazo.

Naibu Mkurugenzi wa shirika la Help Age International, Smart Daniel, anasema taifa lina changamoto ya kutambua walichowekeza kwa wazee kupitia mradi wake wa miaka mitatu na elimu inayotolewa ichukuliwe na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto na itumike inavyokusudiwa.

Habari Kubwa