Mpiga filimbi Maria

16Sep 2020
Ani Jozen
Dar es Salaam
Nipashe
Mpiga filimbi Maria
  • *Msichana tishio anayeongoza kuung’oa udikteta wa Belarus

PENGINE ni nadra kuwaona kinamama wakiongoza mapinduzi kwenye mataifa yao, hata hivyo zama zinabadilika Maria Aleksandrovna Kolesnikova sasa ni kiongozi wa kumtoa rais ikulu.

Mwanasiasa huyo ambaye ni mwanamuziki tena mpiga filimbi kitaaluma aliyezaliwa miaka 38 iliyopita ni tishio kwa ikulu ya nchi yake, baada ya kushiriki kikamilifu kwenye maandamano yasiyokwisha ya kuing’oa serikali ya kiimla ya Belarus.

Maria Kolesnikova anasikika duniani kote akiwa mjumbe na kinara wa kamati ya uratibu ya maandamano ya kumng’atua madarakani Rais Alexander Lukashenko wa Belarus.

Mtawala huyo alitangazwa kuwa mshindi kwa asimilia 80 ya kura wakati takriban kila mpiga kura aliyekuwa anaongea na mwenzie au anafahamu hisia zilizopo katika mtaa wake au mji alikuwa na uhakika kuwa Lukashenko hakupata watu waliompgia kura.

Kiongozi anayetakiwa kuondoka ikulu amedumu madarakani tangu mwaka 1994 akiwa ni masalia ya Urusi ya zamani iliyokuwa ikijulikana kama Muungano wa Jamhuri za Kisovieti – USSR.

CHIMBUKO LA MARIA

Msichana huyo alizaliwa Aprili 24, 1982 na kukulia jijini Minsk, mji mkuu wa Belarus na kitovu cha maandamano hayo kwa mujibu wa taarifa zinazosambazwa hivi sasa mitandaoni, anataka kuingia ikulu.

Maria anatokea kwenye familia yenye uwezo kifedha, kwani wazazi wake ni wahandisi kitaaluma na alisoma katika shule binafsi alipomaliza sekondari, akaanza kujifunza muziki akibobea kwenye kupiga filimbi.

Alianza kushirikii katika maonyesho ya kikundi cha muziki cha taifa cha National Academic Concert Orchestra cha nchi hiyo na kumaliza masomo yake kama mpiga filimbi na muongozaji orchestra.

Alipofikisha miaka 25 Chuo Kikuu cha Muziki na Sanaa za Maonyesho cha Stuttgart nchini Ujerumani, akiwa amefaulu katika muziki wa zamani na wa kisasa mwaka 2012.

Kuanzia wakati huo Maria akaanza kuratibu miradi ya ushirikiano wa kitamaduni kati ya Ujerumani na Belarus na mwaka 2017 akashiriki kuanzisha kikundi cha fani na sanaa.

Hadi mwaka jana alikuwa Mkurugenzi wa Sanaa wa Klabu ya OK 17 ya jijini Minsk.

Mwaka 2020 ulikuwa wa uchaguzi akaanza kuongoza kwaya tofauti.

KUINGIA SIASA

Mei mwaka huu anajitosa kwenye kampeni ya kutiania urais ya Viktar Babaryka na kuteuliwa kuwa meneja wake. Babaryka alikamatwa na kupigwa marufuki kushiriki uchaguzi mkuu, hivyo Kolesnikova na Veronika Tsepkalo wakajiunga na kampeni ya Sviatlana Tsikhanouskaya, mwanamke mgombea urais ambaye alianza kupata umaarufu kwa kuchukua nafasi ya mumewe aliyezuiliwa kushiriki uchaguzi pia.

Sviatlana Tsikhanouskaya ni mwanamama kijana pia mwenye miaka 37 na mwalimu wa zamani wa Kiingereza, hali inayomfanya apate urahisi wa kujieleza katika vyombo vya habari vya kimataifa wakati alipokimbilia nje ya Belarus.

Licha ya kwamba alikuwa hajulikani kisiasa alipoingia ulingoni kuziba nafasi ya mumewe Mei mwaka huu, wanaompinga Rais Lukashenko hawakupata taabu kuelekeza kura zao kwake ndiyo maana ‘ushindi wa kishindo’ wa Lukashenko ulipotangazwa maandamano yalianza mara moja.

HARAKATI ZAIDI

Ilikuwa ni suala la kuangaliana machoni na kujua kuwa hakuna hata mtu mmoja aliyepiga kura kumuunga mkono Lukashenko, kati ya watu 10 au 20 wanaoongea na siyo rahisi kupata watu wanaosema kuwa idadi inayoweza kukaribia nusu ya wapiga kura ilimuunga mkono.

Hivyo maandamano yakaanza kutaka uitishwe uchaguzi mwingine ambao utakuwa huru, haki wenye unaoaminika, unaosimamiwa na waangalizi kutoka nchi za Ulaya.

Ni wakati wa kuelekea kupiga kura ambako Maria Kolesnikova alijiunga na kamati ya watu saba ya uendeshaji wa kampeni ya Tsikhanouskaya.

Kuanzia Agosti 20, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Belarus akafungua kesi ya jinai dhidi ya wajumbe wa kamati hiyo ya uendeshaji maandamano, baada ya matokeo ya ‘ushindi wa kishindo’ kutolewa.

Maelezo ni kuwa kamati ‘inajaribu kukamata mamlaka ya nchi, kuhatarisha usalama wa taifa.’

Mwanzoni mwa mwezi huu, Maria Kolesnikova ameunda chama kipya cha siasa akikiita Razam yaani ‘Pamoja’ au Rassemblement kwa Kifaransa, kujiendesha nje ya kamati ile ya chama kilichoshiriki uchaguzi mkuu.

Ilieleweka ni jitihada kubadilisha majina kuondoa kisingizio kuwa chama kilichoshiriki uchaguzi kinadai kuwa kimeshinda hivyo kinaendesha maandamano kutwaa mamlaka ya nchi.

Inakuwa ni kikundi kipya cha siasa kisicho na uhusiano na upigaji kura au wagombea katika uchaguzi mkuu ila kinasisitiza urudiwe.

Hatua hiyo, haikumwondolea masahibu ya kisiasa Maria Kolesnikova kwani polisi sasa wanatafuta viongozi wa waandamanaji na hakuna cha chama kipi cha siasa au kamati ya matayarisho.

Wiki iliyopita Septemba 7, Maria Kolesnikova akakamatwa na polisi waliovaa kininja ili kuficha nyuso, akiwa jijini Minsk, familia yake ikatoa taarifa vyombo vya usalama na katika vyombo vya habari kuwa hajulikani alipo ila siku iliyofuata akakamatwa karibu na mpaka wa Ukraine, vyombo vya usalama vikadai kuwa alikuwa akijaribu kutoroka alfajiri saa 10 akiwa na wasaidizi wawili wanaume.

Taarifa hizo hata hivyo zilikanushwa na ikaelezwa kuwa alichana hati yake ya kusafiria wakati utawala huo ukitaka kumsukuma nje ya mpaka aingie nchi nyingine inavyoelekea kwa madai kuwa ni raia wa Ukraine zaidi.

Wasaidizi wake wengine wawili katika kamati hiyo ya uratibu wa maandamano walikamatwa Septemba 9 na watu hao hao wanaoficha nyuso zao na Jumamosi iliyopita Septemba 12, mwanamama Maria Kolesnikova alihamishwa kutoka kituo cha kizuizini cha Minsk kupelekwa kituo kingine kinachosemekana ni cha muda, huko Zhodino.

Mizunguko na jitihada hizo za dola zinaonyesha mpiga filimbi huyo sasa ni kiongozi halisi, siyo tu kwamba ni mwanakamati katika kampeni ya Tsikhanouskaya ila ni kiongozi mwenza kikamilifu.

Ndiyo mgongano kimantiki wa ukandamizaji, kuwa unavyozidi kuswaga viongozi waliopo, ndiyo unazidi kuunda wengine wenye nguvu na kukubalika zaidi kiasi kwamba hata waliokuwa wanaamini utawala una nia njema, wanapatwa na shaka.

MITANDAO

Habari Kubwa