Mratibu Afya: Mti shamba yaua sana wajawazito, kuiacha ubishi mkubwa

14Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Mwanza
Nipashe
Mratibu Afya: Mti shamba yaua sana wajawazito, kuiacha ubishi mkubwa
  • * Watafuna, kupeana kwa siri wodini
  • * Majani bangi…;chanzo wakunga, bibi
  • *Sasa? Operesheni upekuzi, kutajana
  • *Elimu yaanzia wodini hadi mazikoni

“MIMEA wanayotumia kutengeneza dawa za kuongeza uchungu wajawazito, wanataja kuwa ni mizizi ya bangi na majani yake, mmea wa mgagani pamoja na magome ya miti shamba na wakati mwingine huweka sehemu za siri,” anatamka Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto, Mkoa wa Mwanza, Secilia Mrema.

Sehemu ya Wodi ya Kinamama katika Hospitali ya Rufani Sekou Toure, jijini Mwanza katika picha tofauti. PICHA: MTANDAO.

Na Anthony Gervas, MWANZA

Ni mazungumzo maalum na Nipashe katika Ofisi za Mganga Mkuu wa Mkoa Mwanza, ilipofahamishwa kwamba dawa za kienyeji ni tatizo linalochangia madhara makubwa kwa wajawazito wakati wa kujifungua hospitalini.

Simulizi hiyo ya undani wenye madhara, Inataja mlolongo wa mambo, ikiwamo uelewa mdogo kuhusu kufahamu wa hatari za dawa hizo, ambao Secilia anadadavua kwa kina kuanzia hali halisi hadi picha kamili iliyokoo mkoani humo.

Madhara yakoje?

"Tunapompima mama mjamzito wakati wa kujifungua tunakuta amechanika mfuko wa kizazi, anatokwa damu nyingi na mtoto amefia tumboni, wakati vipimo vinaonyesha hana magonjwa ya aina yeyote yaliyoweza kusababisha madhara hayo,

"Lakini, tunapomkamata na kumhoji, anakiri kutumia dawa za kienyeji ambazo hazina kipimo na kusema wanatumia mizizi na majani ya mmea wa bangi, mmea wa mgagani na magome ya miti shamba,kwa madai zinaongeza uchungu aweze kujifungua haraka,” anaeleza hali inayotawala.

Pia, anasema baadhi ya kinamama hao, wamekuwa wakikamatwa na wataalamu wa afya katika vituo vya afya na hospitali wakiwa na dawa hizo, wanaozitumia kwa kificho wakati wanapolazwa wodini kusubirii kujifungua.

“Katika Mkoa wa Mwanza tangu Januari mwaka huu hadi sasa, idadi ya kinamama 139 wamefariki dunia kutokana na sababu za madhara ya dawa hizo wakati wa kujifungua,” anasema na kuongeza:

“Kati yao, kinamama 39 wamefariki dunia kwa kutokwa damu nyingi na kinamama 10 wamefariki dunia kutokana na kuchanika mfuko wa kizazi.”

Mratibu Secilia anasema, watoto waliofia tumboni wakati wa kujifungua, mama zao ni zaidi ya 500 na magonjwa mengine nayo yanayochangia madhara hayo, akiyataja baadhi yanayohusiana na zinaa, shinikizo la damu, malaria na kisukari.

Wanaokiri wodini

“Tunapowakamata wodini wakiwa na dawa hizo, wanakiri. Hapohapo tunachukua hatua ya kuwanyang'anya na kuanza kuwaelimisha kufuata taratibu za huduma bora za afya, ikiwamo kuhudhuria kliniki katika vituo vyetu vya afya.

"Wakati mwingine tunapowakamata wodini wamelazwa wakisubiri kujifungua, wanatajana kuwa wanagawiana kwa siri na wenzao ndani ya wodi, huku wakitumia kwa siri kupitia chai. Staili zingine, wengine huziweka sehemu za siri, lengo wanadai zinawahisha uchungu kujifungua haraka,” anaeleza.

Secilia anaeleza kwa sasa wamekuwa wakichungana wodini wenyewe na wanapobaini jambo wanatoa taarifa kwa wauguzi, baada ya kupata elimu kuhusiana na madhara husika.

Mratibu huyo anaeleza kwamba, wajawazito hao wanapokamatwa wodini na kuhojiwa walikozipata,huwataja ndugu wa karibu wenye nafasuiza uzazi na ulezi; bibi, shangazi, wakunga wa asili na waganga wa kienyeji, ambao ndio chanzo kikuu.

Madarasa

Secilia anasema uchungu wa kutumia dawa za kitaalamu kwa mjamzito wakati wa kujifungua, inapokuwa mimba ya kwanza huchukua muda wa saa 12, lakini inapokuwa mimba ya pili, huchukua muda kuanzia saa sita hadi nane.

Aidha, anaeleza kwamba Idara ya Afya, imeanzisha timu ya wataalamu wa afya kuhakikisha wanatoa elimu kwa kinamama hao, ili waachane na matumizi ya dawa hizo kupitia vyombo vya habari, vikao vya halmashauri na vikao vya kata.

Vilevile, mratibu huyo anasema elimu hiyo inatolewa kupitia mkusanyiko wa msiba baada ya maziko, ikiwa mjamzito amepoteza maisha kutokana na matumizi ya dawa hizo, kwa kuwakusanya wananchi waliopo msibani na kuwaelezea kuhusu madhara hayo.

Elimu nyingine anaitaja kupitishwa kwenye vikao vya kata, vituo vya afya, zahanati, wakunga na waganga wa kienyeji, wakiwataka wafuate taratibu za kutumia dawa rasmi za serikali, kupitia taratibu rasmi kama vile kwenye vituo vya afya.

Familia

Wanafamilia na ndugu ndiyo wanatajwa zaidi kuhusika na utengenezaji dawa za kienyeji kwa ajili ya kuongeza uchungu kwa mjamzito, lengo ni kwamba asikae muda mrefu wodini kusubiri kujifungua kwa machakato wa kitaalamu.

Secilia anasema, ni kawaida mjamzito anapokuwa katika mimba ya kwanza anajifungua baada ya kuwapo katika uchungu wa saa 12, lakini kwa mimba ya pili anatakiwa uchungu kukaa kuanzia saa sita hadi nane.

Angalizo lake linalochukua sura ya onyo, ni kwamba mjamzito hapaswi kutumia dawa yoyote ambayo hajaandikiwa na daktari na akifanya hivyo tayari amesajiingiza katika hatari ya afya yake.

Kliniki je?

Mratibu huyo anasema, ni kanuni na sheria kwamba mjamzito anatakiwa kuhudhuria kliniki zote kama alivyoelekezwa katika kituo cha afya kila mwezi, ili kupata huduma iliyo sahihi hadi hatua ya kujifungua.

“Kwa sasa asilimia 93 ya kinamama wajawazito wanakwenda katika vituo vya kuhudhuria kliniki zao, lakini wanaofuata taratibu hadi mwisho ni asilimia 76, “anasema.

Mwanza ilivyo

Mratibu Secilia, anasema Mkoa wa Mwanza, una jumla ya vituo vya afya 52; kati yake vipo vituo 14 vipya vilivyoanzishwa na serikali kwa ajili ya kutoa huduma za upasuaji kinamama wajawazito wakati wa kujifungua na vingine vinane vya zamani, vinavyoendelea na huduma hiyo.

“Mkoa wa Mwanza tumeanzisha mkakati kabambe wa kufundisha watumishi 20 wa afya, kwa ajili ya kufanya utafiti kuhusu matumizi ya dawa hizo, kujua moja kwa moja asilimia za madhara yake,” anasema.

Rai yake ni umma wa wajawazito uache kutumia dawa tofauti na ufuate ushauri wa daktari au mtaalam wa afya kutoka katika vituo vya afya na hospitali, kwa vile hazina kipimo.

Alhamisi wiki ijayo, simulizi ya ushuhuda.

Mwandishi anapatikana kwa barua pepe: [email protected] na simu(+255) 0682 86 92 44.

Habari Kubwa