MSIJE TAIFA Simba, Yanga zinavyotoa vipigo Dar

10Feb 2016
Adam Fungamwango
DAR
Lete Raha
MSIJE TAIFA Simba, Yanga zinavyotoa vipigo Dar

MSIJE Taifa. Hivi ndivyo inavyoonekana Simba na Yanga zinaziambia timu za mikoani kutokana na kutoa vichapo vya mbwamwizi kwa timu nyingi zinapokanyaga kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

NGOMA

Mpaka sasa uwanja huo ndiyo unaoongoza kwa kuruhusu magoli 66 ambayo ni mengi zaidi kuliko uwanja mwingine wowote ule nchini unaochezewa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini asilimia 95 ya magoli yote hayo hufungwa timu za mikoani zinapokuja kucheza jijini.

Ushindi wa magoli 4-0 ilioupata Yanga dhidi ya JKT Ruvu mwishoni mwa wiki na 5-1 ilioupata Simba hivi karibuni, ni muendelezo tu wa vipigo vikali inavyotoa kwa timu nyingi inapokanyaga uwanja huo.

Nadhani kama kungekuwa na uwezekano wa kukataa uwanja, timu nyingi za mikoani zingekataa kucheza kwenye uwanja huo kwa kuhofia vipigo kikubwa.

Inavyoonekana kuwa Uwanja wa Taifa ni hatari zaidi kwa timu za mikoani kuliko hata timu zenyewe za Simba na Yanga.
Hii ni kwa sababu timu hizo kongwe zinaonekana kuwa butu zinapokwenda kwenye viwanja vingine zaidi ya hicho.
Hupata wakati mgumu na kushindwa kucheza soka la kujiachia kama zinavyofanya kwenye Uwanja wa Taifa, badala yake zinashinda kwa tabu, sare au kuambulia vipigo.

Simba na Yanga hazijaweza kufunga magoli zaidi ya mawili kwenye viwanja vya mikoani hadi sasa msimu huu.
Mwandishi wa makala haya amekusanya matokeo ya mechi za Simba na Yanga ambazo zilitoa kipigo kikubwa kwenye uwanja wa Taifa msimu huu, lakini pia mechi za mikoani ambazo zimeonekana kuwapa tabu, huku ushambuliaji ukiwa butu.

Mechi za Yanga Taifa

1. Yanga 3-0 Prisons
Prisons ya Mbeya ilikanyaga kwenye uwanja wa Taifa Septemba 16 mwaka jana na kupokea kipigo cha mabao 3-0, yaliyofungwa na Mbuyu Twite, Amissi Tambwe na Donald Ngoma kwa mkwaju wa penalti.

2. Yanga 4-1 JKT Ruvu
Mechi ya Jumapili iliyopita si ya kwanza kwa JKT Ruvu kukumbana na dhahama ya Yanga inapokuwa Taifa. Ilikutana na kipigo cha mabao 4-1 kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Septemba 19 mwaka jana. Yalikuwa ni magoli ya Tambwe aliyefunga mawili, Ngoma na Thabani Kamusoko, Michael Aidan akiifungia JKT.

3. Yanga 4-1 Toto Africans
Toto African nayo ikaingia kwenye anga za Yanga kwenye uwanja wa Taifa Oktoba 21 mwaka jana na kukutana na kipigo cha mabaoa 4-1. Magoli hayo yalifungwa na Juma Abdul, Simon Msuva aliyefunga magoli mawili na Tambwe.

4. Yanga 4-0 Stand United
Stand United nayo ilikuja kwenye Uwanja wa Taifa Desemba 19 mwaka jana, nayo ikazabuliwa mabao mabao 4-0 yaliyowekwa kwenye 'kamba' na Tambwe aliyefunga 'hat-trick' na Kamusoko.

5. Yanga 3-0 Mbeya City
Mbeya City nayo pamoja na kukuruka iliondoka na kipigo cha mabao 3-0 Desemba 26 mwaka jana, Tambwe akifunga mawili na Kamusoko moja.

6. Yanga 5-0 Majimaji
Januari 21 mwaka huu, Majimaji nayo ikatia pua Taifa na kukandikwa mabao 5-0, Tambwe kama kawaida, akifunga 'hat-trick', Ngoma na Kamusoko wakifunga goli moja kila mmoja.

7. Yanga 4-0 JKT Ruvu
Mechi hii ilichezwa Februari 6 mwaka huu, Msuva akifunga mawili, Isofou Boubacar na Ngoma kila mmoja akifunga bao moja, Yanga ikaondoka na ushindi wa mabao 4-0.

Mechi za Simba Taifa

1. Simba 3-1 Kagera Sugar
Achana na mechi ya wiki iliyopita Simba iliposhinda bao 1-0, kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa uwanja wa Taifa Kagera Sugar ilikubali kipigo cha mabao 3-1. Ilikuwa na 'hat-trick' ya Hamisi Kiiza na la kufutia machozi la Mbaraka Yusuph, mechi ikichezwa Septemba 20 mwaka jana.

2. Simba 6-1 Majimaji
Majimaji ndiyo timu iliyoathirika zaidi na uwanja wa Taifa, kwani ilifungwa mabao 6-1 na Simba, ukiacha 5-0 za Yanga. Ilikuwa ni Oktoba 31 mwaka jana, Ibrahim Ajibu akipiga 'hat-trick', Kiiza akifunga mawili na moja la Mohamed Hussein 'Tshabalala' na la kufutia machozi la Ditram Nchimbi.

3. Simba 4-0 African Sports
African Sports nayo ilikanyanga Taifa na kukumbana na kisago cha mabao 4-0 dhidi ya Simba, mechi ikichezwa Januari 30 mwaka huu, magoli ya Kiiza mawili, Hassan Kessy na Haji Ugando.

4. Simba 5-1 Mgambo Shooting
Mgambo Shooting haikusalimika na homa ya Taifa, ilipobabuliwa mabao 5-1 dhidi ya Simba, yakifungwa na Kiiza mawili, Mwinyi Kazimoto na Ajibu. Mechi ilichezwa Februari 3 mwaka huu.

MIKOANI BUTU

Mechi za Yanga mikoani

1. Yanga 2-0 Mtibwa Sugar
Yanga ilishinda 2-0, mabao ya Malimu Busungu na Ngoma Septemba 30 mwaka jana uwanja wa Jamhuri Morogoro.

2. Yanga 2-2 Mwadui FC
Ililazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Mwadui Oktoba 28 mwaka jana, mabao yote yakifungwa na Ngoma, Bakari Kigodeko na Paul Nonga wakiifungia Mwadui kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga.

3. Yanga 2-0 Kagera Sugar
Oktoba 31 mwaka jana ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar yaliyoifungwa na Deus Kaseke na Ngoma uwanja wa Ally Hassan Mwinyi Tabora.

4. Yanga 0-0 Mgambo Shooting
Ilibanwa kwenye uwanja wa Mkwakwani na kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya Mgambo Shooting Desemba 12 mwaka jana.

5. Yanga 1-0 African Sports
Ilipata bao kwa tabu katika dakika ya tano ya nyongeza kwenye mechi dhidi ya African Sports lililochezwa Desemba 16 Mkwakwani Tanga na kuondoka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Kamusoko.

6. Yanga 0-2 Coastal Union
Ilikuwa ni Januari 30 mwaka huu, ilipopata kipigo cha kwanza kwenye Ligi Kuu Mkwakwani kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union yaliyofungwa na Miraji Adam na Juma Mahadhi.

7. Yanga 2-2 Prisons
Iliponea chupuchupu ugenini Sokoine Mbeya kwa kutoka sare ya mabao 2-2 Februari 3, kwa magoli ya Tambwe na Msuva, Jeremiah Juma na Mohamed Mkopi wakiifungia Prisons.

Mechi za Simba mikoani

1. Simba 1-0 African Sports
Septemba 12 mwaka jana ilishinda bao 1-0 dhidi ya African Sports Mkwakwani Tanga lililofungwa na Kiiza.

2. Simba 2-0 Mgambo
Kwenye uwanja huo huo, ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Mgambo yaliyofungwa na Jastice Majabvi na Kiiza, Septemba 16.

3. Simba 1-0 Mbeya City
Ikashinda tena kwa tabu bao 1-0 dhidi ya Mbeya City Sokoine Mbeya Oktoba 17 kwa bao la Juuko Murshid.

4. Simba 0-1 Prisons
Ikachapwa bao 1-0 dhidi ya Prisons Oktoba 21 mwaka jana Sokoine Mbeya, lililofungwa na Mkopi.

5. Simba 1-1 Toto Africans
Desemba 19, ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kwa goli la Danny Lyanga, na Evarist Benard akisawazisha.

6. Simba 1-1 Mwadui
Iliponea chupuchupu Kambarage, Shinyanga kwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mwadui kwa bao la Brian Majegwa akisawazisha goli la Nizar Khalfan Desemba 26.

7. Simba 1-0 Kagera Sugar
Februari 7 Ibrahim Ajibu aliipatia Simba bao pekee iliichapa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.