Msimu mpya EPL, kuna jipya gani?

12Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Msimu mpya EPL, kuna jipya gani?

PAZIA la Ligi Kuu ya England msimu wa 2019/2020 limefunguliwa rasmi Ijumaa.

Msimu uliopita 2018/2019, ulikuwa ni moja ya misimu bora na wenye ushindani wa hali ya juu. Je, mambo yatakuwaje kwenye msimu huu mpya.

Mshindi wa Ligi Kuu msimu uliopita Manchester City na mshindi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya Liverpool, walimaliza kwa kupishana kwa pointi moja tu katika ligi.

Liverpool ilimaliza msimu ikiwa na pointi 97, ambazo ni nyingi kuwahi kukusanywa na mshindi wa pili. Jurgen Klopp atataka kuhakikisha anampiku Pep Guardiola safari hii.

Msimu wa 2019/19 Liverpool na Manchester City walibadilishana nafasi ya kileleni zaidi ya mara kumi kwenye mbio za kuwania ubingwa wa EPL na kuonyesha uhasama wa aina yake huku wakicheza kandanda ya kuvutia na kasi ya kusisimua.

Uhasama huo bila shaka utaendelea tena msimu huu na ushahidi ni mchezo wa Ngao ya Jamii ambao ulichezwa kama fainali kwenye Uwanja wa Wembley, kila upande ukitaka kushinda mechi hiyo. Kwa Liverpool na City, unaweza kusema huu si msimu mpya kwao bali ni mwendelezo wa msimu uliopita.

Liverpool walipoteza mchezo huo kwa matuta, baada ya kukosa mkwaju mmoja wa penalti, lakini tulipata nafasi ya kuona kionjo cha jinsi msimu utakavyokwenda kwa timu hizi mbili ambazo ni kama 'wababe wapya' katika Ligi Kuu ya England ambayo ilikuwa ikitawaliwa na Manchester United, Chelsea na Arsenal katika robo karne iliyopita.

Lakini sasa mtaani kuna 'vichwa' vipya, na katika takriban miaka kumi iliyopita, tunashuhudia kilele cha EPL kikianza kutawaliwa na waliokuwa 'wanyonge'.

Man City, Liverpool na Tottenham wameingia kwenye picha na hakuna dalili zozote zinazoonyesha kuwa wataondoka hivi karibuni.

EPL ambayo kwa miaka mingi ikifahamika kuwa na “Top 4" sasa imebadilika na kufika “Top 6" kwa sababu ya ushindani ambao umeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, hasa kutokana na kuingia kwa wababe wapya.

Nafasi tatu za juu, kama msimu uliopita, wengi wanatarajia kugombewa na Tottenham, Man City na Liverpool. Nafasi tatu zilizosalia za top 6 zinatazamiwa kugombewa na Arsenal, Chelsea na Manchester United.

Lakini kama tulivyoshuhudia msimu uliopita, nafasi hizo 'hazijathibitishwa' kwa sababu kuna timu kama Everton na Wolverhampton ambazo kwa jinsi zilivyocheza zinaweza kutikisa na kuingia ndani sita bora.

Je, Solskjaer ataweza kuiongoza Man United mpaka kuchukua ubingwa msimu huu? Ama mashabiki wataendelea kusubiri?

Licha ya kuwa msimu huu fedha nyingi hazijatumika kwenye usajili ukilinganisha na misimu miwili iliyopita, utakuwa msimu mgumu hasa kwa makocha wapya katika timu za juu- kama vile Frank Lampard, Ole Gunnar Solskjaer na hata Unai Emery ambaye unaweza kusema ndio kwanza anaunda kikosi chake baada ya miaka zaidi ya 20 ya Arsene Wenger.

Kwa upande wa chini wa msimamo, katika miaka kumi iliyopita, timu mbili kati ya tatu zinazopanda daraja hufanikiwa kusalia kwenye ligi.

Ni mara tatu tu katika historia ya Ligi Kuu ya England ambapo timu zote tatu zilizopanda daraja zilifanikiwa kuepuka kushuka daraja katika msimu ambao zilipanda.

Msimu huu teknolojia ya maamuzi kwa njia ya video, VAR, itatumika kwa mara ya kwanza na hivyo kuongeza chachu katika ligi hii maarufu na yenye ushindani duniani.

Na sheria nyingine kadhaa pia zitatumika, ikiwamo ya kudhibiti makocha 'wakorofi' kwa kuonyeshwa kadi za njano kama onyo na pia sheria ya wachezaji wanaobadilishwa hutakiwa kutoka uwanjani haraka kuepuka kupoteza muda.

Msimu ni mpya, na EPL miaka yote hushangaza wengi kwa kuleta kitu kipya, lakini kwenye karatasi unaweza kubashiri nani ana nafasi kubwa ya kuwa bingwa, na nani ana nafasi kubwa ya kushuka daraja.

Hata hivyo, burudani itakuwa katika timu zile ambazo zinataka kwa udi na uvumba kurejesha 'heshima' zake.

Habari Kubwa