Mtaalamu: Ukiwa hivi, basi una tatizo

10Oct 2019
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Mtaalamu: Ukiwa hivi, basi una tatizo

MATATIZO ya afya ya akili ni changamoto inayowakumba watu wa rika tofauti, kuanzia vijana hadi watu wazima. Sababu kubwa ni kwenda kinyume na mtazamo na matendo sahihi.

Mtaalamu wa afya ya akili, John Ambrose, akizungumza katika ofisi za Nipashe. PICHA: SABATO KASIKA.

Afya ya akili, kitaalamu ina uhusiano na ustawi wa mwili, kwamba inaufuatilia mwili kwa karibu, hata unapopata tatizo, akili inakuwa makini kuuhami kupitia mifumo yake.

Wakati mtu ana shida ya afya ya akili, inamaanisha hana nafasi ya mwamko sahihi ya kuutetea mwili kwa madhara au unapokuwa hatarini. Hapo, kitaalamu kuna sababu nyingi zinazoigusa afya ya akili.

Leo dunia inaadhimisha Siku ya Afya ya Akili. Mtaalamu wa akili na jamii kutoka taasisi ya kijamii iitwayo, Psychosocial Health and Entrepreneurship Development Skills (PHEDES), John Ambrose, alipozungumza na Nipashe ana mengi ya kujuza.

Ambrose anasema, suala la afya ya akili ni muhimu na lina mtazamo, fikra na matendo ya kipekee. Mtu akitenda kinyume na mpangilio rasmi uliopo, huyo anatafsiriwa kuwa na tatizo la afya ya akili.

Umri

Anasema, kila umri una mtazamo, fikra na matendo yake na vyote vikienda kinyume na usahihi uliopo, jibu ni kwamba kuna tatizo la afya ya akili, ambalo ni muhimu likafanyiwa kazi liishe.

"Takwimu za dunia zinaonyesha, tatizo la afya ya akili linafanya vijana wa umri wa kati ya miaka 15 hadi 29 kupoteza maisha, kwamba kila baada ya sekunde 40 kuna mtu hufariki duniani kwa kujinyonga," anasema Ambrose.

Anaeleza vijana katika umri wa balehe wana mengi ya hatari, hivyo ni muhimu wakapewa elimu maalum inayohusu makuzi na afya ya akili, ili iwaweke sawa mbali na madhara yanayowazunguka.

Mtaalamu huyo, anafafanua kuwa ni umri ambao hata kijana akichapwa na mzazi wake, kwa sababu ya kufanya vibaya masomoni, anaamua kujiua.

"Hilo ni tatizo la afya ya akili, kutokana na mtazamo wake kwenda kinyume na kutawaliwa na mihemko ambayo ni hatari kwa maisha yake, hivyo ni muhimu kuelimishwa jinsi ya kuishinda hali hiyo," anasema.

Katika hulka hiyo, analitaja lingine la umri wa miaka 29 hadi 40, ambalo linachangamkia maisha hata kwa kuiba au kuomba rushwa, lengo likiwa ni kufanikiwa haraka.

Anasema, kichocheo cha hali hiyo ni afya mbaya ya akili. Anasema, kuna haja ya kuwasaidia vijana wa umri huo kuacha dhuluma na tamaa za maisha na wazingatie maadili kazini watimize ndoto zao kwa haki.

"Unaweza kukuta wengi wao wanafungwa kwa sababu ya kutokuwa wastahimilivu katika kutafuta maisha. Hii yote inatokana na mtazamo ambao ni hasi na kimsingi unatokana na tatizo la afya ya akili," anasema.

Anasema, pia afya ya akili inaingia katika ndoa; kuoa au kuolewa, elimu na kazini. Katika hilo, wapo wanaokosea kuchagua wachumba, wanaotoa ngono waahiriwe au kufanikiwa mtihani.

"Unapoona mtu anakwenda kinyume ili kutimiza lengo lake, basi ujue hilo linatokana na mtazamo wake wa kwenda kinyume ambao msingi wake unatokana na tatizo la afya ya akili," anasema.

Ambrose anasema, hilo pia liko kwa watu wazima, ambao mtazamo wao husababisha wasifikie malengo kwa kutofanya maamuzi sahihi kuanzia nyumbani hadi kazini na kujikuta wanakwama.

Mtaalamu huyo anasema, asasi yake ya Phedes inafanya kazi ya kuelimisha saikolojia katika maeneo mbalimbali nchini, kuanzia kwa mtu binafsi na ofisi, lengo ni kuwasaidia Watanzania kuepuka tatizo la afya ya akili.

"Pale tunapoona tatizo linahusu madaktari, tunawashahuri wahusika kwenda hospitalini kupata huduma zaidi, lakini kama ni suala saikolojia, basi tunatoa elimu na tumesaidia watu wengi tu.

Anaeleza, suala la afya ya akili, kimsingi ni ukamilifu wa hisia, saikolojia na uhusiano wa jamii ikihusisha mtazamo wa mtu, fikra, matendo na tabia yake vinakuwa sawa.

"Sisi tunataka watu wajitambue na watambue wajibu wao ili wawajibike na kutekeleza majukumu yao ipasavyo, kwa maana ya kutokuwa na matatizo kwenye afya ya akili," anasema.

Anataja afya ya akili ni nyenzo muhimu inayomkalilisha mwanadamu dhidi ya maradhi ya ubongo na ustawi wake kiujumla, unaotegemewa kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja.

Ambrose anataja ujumbe wa maadhimisho ya mwaka huu yanayofanyika leo ni 'Zuia Ukatili, Zuia Kujinyonga' ikiadhishwa maeneo mtambuka kupitia Siku ya Afya ya Akili Duniani, ambayo ni kila siku kama ya leo.

Mtaalamu huyo anataja ulingo mwingine wa maradhi hayo kwamba: "Mtu anapotumia dawa za kulevya hadi kufikia kutojitambua na kufanya mambo yasiyofaa kwenye jamii, basi ujue kuwa hilo nalo ni tatizo la afya ya akili. Wahusika wanatakiwa kusaidiwa kisaikolojia."

Habari Kubwa